Dar es Salaam. Serikali imetenga kiasi cha Sh15.9 trilioni kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2024/2025.
Kati ya fedha hizo, Sh12.3 trilioni ikijumuisha Sh1.1 trilioni za ruzuku ya maendeleo kwa ajili ya elimu ya elimumsingi bure na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ni fedha za ndani na Sh3.6 trilioni ni fedha za nje.
Akiwasilisha mpango huo leo bungeni Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali itaongeza ushirikiano na ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza na kugharamia miradi ya maendeleo kupitia njia bunifu na mbadala za ugharamiaji.
Njia hizo ni pamoja na kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo tunakubaliana kuwa ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi wa taifa letu.
Profesa Mkumbo amesema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25 utajielekeza katika maeneo matano ya kipaumbele ambayo ni kuchochea Uchumi shindani na shirikishi Ili kuweza kufikia malengo na shabaha.
Maeneo mengine ya kipaumbele ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma na kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.
Waziri amebainisha kuwa mpango huo umejielekeza pia katika kukamilisha na kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya miundombinu wezeshi katika sekta ya uchukuzi, usafiri na huduma za usafirishaji na sekta ya nishati, sekta ya mawasiliano na sekta ya maji.
Maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele ni ukamilishaji wa baadhi ya miradi ikiwemo ujenzi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR), miundombinu ya bandari, viwanja vya ndege, mtandao wa barabara za lami na madaraja, ufufuaji wa Shirika la Ndege Tanzania, kukamilisha mradi wa kufua umeme wa Maji wa Julius Nyerere – MW 2,115.
Ukamilishaji wa njia za kusafirisha umeme na vituo vya kupozea umeme, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima (Uganda) hadi bandari ya Tanga eneo la Chongoleani na kuongeza kasi ya ujenzi na upanuzi wa Mtandao wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa ili kuharakisha mabadiliko ya kidijitali na mapinduzi ya nne ya viwanda nchini.
Profesa Mkumbo ameeleza kuwa utekelezaji wa Mpango wa mwaka 2024/25 katika usimamizi wa uchumi jumla unalenga kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.4 mwaka 2024 kutoka asilimia ukuaji halisi wa asilimia 5.1 ya mwaka 2023.
Pia kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 – 5.0 katika muda wa kati.
“Malengo mengine ni kuhakikisha mapato ya ndani yanafikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2024/25 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 15.4 mwaka 2023/24, kuongeza mapato ya kodi kufikia asilimia 12.9 ya Pato la Taifa mwaka 2024/25 kutoka asilimia 12.6 mwaka ya 2023/24.
“Kuwa na nakisi ya bajeti ikijumuisha misaada isiyozidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.” Imeeleza sehemu ya taarifa ya mpango huo.