Morogoro. Vyama vya Wakulima wa Miwa (Amcos) katika Bonde la Kilombero vimetakiwa kuongeza uzalishaji wa miwa kutoka tani 20 kwa heka hadi tani 60 kwa heka ili kufanikisha upanuzi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero. Wito huu umetolewa na Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro, Kenneth Shemdoe, katika warsha iliyofanyika leo Alhamaisi Juni 13, 2024.
Shemdowe amesisitiza umuhimu wa kulima kwa kutumia mbinu za kisasa na kitaalamu.
Amesema upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero unahitaji uzalishaji mkubwa wa miwa, hivyo viongozi wa Amcos na maofisa kilimo wanapaswa kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi ya kilimo chenye tija.
Ameongeza kuwa maboresho katika mbinu za kilimo yanaweza kuongeza mavuno kutoka tani 20 hadi 60 au 70 kwa heka moja.
“Katika jitihada za kufikia malengo haya, benki ya NMB imechukua hatua muhimu kwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh1.56 trilioni tangu mwaka 2016 kwa lengo la kusaidia wakulima na mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo,” amesema Shemdowe.
Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango amesema benki hiyo inaunga mkono sekta ya kilimo ambayo inaajiri asilimia 80 ya Watanzania.
“Kutokana na hilo, ndiyo maana benki ya NMB inaendelea kutoa elimu ya fedha na mafunzo ya biashara kwa vyama 1,550 vya wakulima wa miwa na mazao mengine kupitia NMB Foundation,” amesema Shango.
Mwanachama wa Harambee Amcos, Kuludhumu Mholele amesema mikopo inayotolewa na NMB, imekuwa msaada mkubwa kwa wakulima kwa kuwawezesha kuongeza nguvu katika shughuli za kilimo.
Katibu wa vyama vya Wakulima wa Miwa Kilombero, James Mayunga amekiri kuwa mikopo hiyo imeboresha hali ya kiuchumi ya wakulima.
“Na kwa upanuzi wa kiwanda cha sukari Kilombero, kwetu sisi ni ahueni kubwa kwa sababu utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo,” amesema Mayunga.