Marufuku kutumia fedha za kigeni kulipia huduma Tanzania

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imepiga marufuku ya malipo ya huduma kwa kutumia fedha za kigeni kuanzia Julai Mosi 2024 huku akieleza mwongozo wa suala hilo utatolewa baadaye.

Hatua hiyo inatangazwa ili kuondoa usumbufu ambao wanakutana nao baadhi ya watu wanaohitaji huduma kuhangaika kutafuta fedha za kigeni hasa katika kipindi hiki ambacho zinapatikana kwa tabu.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akisoma hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali katika mwaka 2024/2025.

Dk Mwigulu amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokabiliwa na upungufu wa fedha za kigeni katika mwaka 2023/24 ilisababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo: athari za Uviko–19; vita vinavyoendelea nchini Ukraine na katika ukanda wa Gaza; mabadiliko ya tabianchi.

Pamoja na sababu hizo, baadhi ya Watanzania pia wanakuza tatizo la upungufu wa dola kwa baadhi ya watu kudai malipo au kufanya malipo ya bidhaa na huduma zinazotolewa ndani ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni yaani.

Amesema hali hiyo inawafanya Watanzania wahangaike kuitafuta fedha ya kigeni kununua huduma zinazotolewa ndani ya nchi yao badala ya kuwafanya wageni wahangaike kuitafuta shilingi ya Tanzania wanapotaka huduma ndani ya nchi.

Amesema jambo hilo linasababisha kuongezeka kwa mahitaji yasiyo ya lazima ya fedha za kigeni na kuwanyima fursa watu wanaohitaji fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia bidhaa na huduma muhimu kutoka nje ya nchi.

“Kitendo cha kuuza bidhaa au huduma za ndani kwa kutumia fedha za kigeni ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, ambacho kinabainisha kwamba Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali pekee kwa malipo ya ndani ya nchi,” amesema Mwigulu na kuongeza.

“Kuanzia Julai 1, 2024, naelekeza wadau wote wa ndani, taasisi za umma, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa na watu wote waliopo nchini Tanzania wenye tabia ya kuweka bei kwenye huduma au kuuza bidhaa kwa fedha za kigeni kuacha mara moja na kuhakikisha bei za bidhaa na huduma hizo zinatangazwa na kulipwa kwa Shilingi ya Tanzania.

Alitumia nafasi hiyo kuzitaka taasisi zote za Serikali zinazotoza ushuru, ada na tozo mbalimbali kwa fedha za kigeni kurekebisha kanuni zao ili tozo hizo zilipwe kwa shilingi.

“Hata mgeni akija na fedha za kigeni ni vyema akaibadilisha kuwa fedha ya kitanzania ili aweze kupata huduma. Tunafanya kila malipo kwa fedha za kigeni, halafu shilingi ikishuka thamani tunajiuliza tumekosea wapi,” amesema Dk Mwigulu.

Aliwataka watanzania na wadau wote waliopo nchini kuacha kununua/kulipia vitu vilivyomo nchini kwa fedha za kigeni, hususan vifaa vya kielektroniki, ada za shule/chuo, kodi za nyumba, viwanja, na bidhaa au huduma mbalimbali kwa fedha za kigeni.

“Naielekeza Benki Kuu pamoja na vyombo vingine vinavyohusika kuendelea kudhibiti suala hili, kufuatilia kwa ukaribu ili kubaini wote wanaoendelea kufanya makosa hayo, na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema Dk Mwigulu.

Related Posts