MUNICH, UJERUMANI: MICHUANO ya Euro mwaka huu inaanza kesho, ambapo itapigwa Ujerumani, huku jumla ya timu 24 zikitarajiwa kushiriki.
Hii inakuwa ni mara ya 17 kwa michuano hii kufanyika huku Hispania na mwenyeji Ujerumani yakiwa ndio mataifa yaliyoshinda mara nyingi zaidi (3), tangu mwaka 1958.
Mara zote ambazo michuano hii inapigwa huwa kuna baadhi ya matukio ya kushangaza yanayotokea, ambayo hubaki kwenye vitabu vya historia ya soka milele.
Leo tumekuletea mambo matano ya kukumbukwa zaidi yaliyowahi kutokea kwenye michuano ya Euro tangu kuanzishwa kwake.
KUZALIWA KWA PENALTI YA PANENKA
Kipindi hiki michuano ya ilikuwa ikichezwa katika maeneo tofauti hadi hatua ya nusu fainali ambapo timu ndio zilikutana eneo moja kwa ajili ya kucheza nusu fainali na fainali yenyewe.
Mwaka huu zilikutana Ubelgiji ambapo kulikuwa na Yugoslavia, Czechoslovakia, Uholanzi, Ujerumani ya Mashariki. Czechs na Ujerumani zikapita kwenda fainali.
Katika fainali Czechoslovakia iliongoza kwa mabao 2-0 ndani ya dakika 20 za mwanzo za mchezo kabla ya Ujerumani kusawazisha.
Mchezo ukaenda kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
Uli Hoeneb wa Ujerumani alikosa katika piga nikupige na Antonin Panenka akaenda kufunga na kuipa Czechs ubingwa.
Penalti aliyopiga Panenka ilikuwa ni mara ya kwanza kuonekana kwenye soka na tangu hapo mastaa wengi wakawa wanaiga upigaji huo na rasmi ikabatizwa jina la Panenka ambaye ndio mwanzilishi.
UBINGWA WA MAAJABU WA UGIRIKI
Wakati inaenda katika michuano ya mwaka huu, Ugiriki ilikuwa imefuzu mara moja tu michuano ya nyuma ya hapo, nayo ilikuwa ni mwaka 1980 ambapo iliishia hatua ya makundi ikiburuza mkia kwa pointi moja tu.
Haikuwa inapewa nafasi ya kufanya vizuri kabisa na hilo lilizidishwa na aina ya kundi walilokuwepo ambapo mbali ya mwenyeji Ureno, walikuwa na Urusi na Hispania.
Walianza kuonyesha maajabu katika mchezo wao wa kwanza baada ya kuichapa Ureno mabao 2-1, kisha ikatoa sare na Hispania na ikapoteza mbele ya Urusi.
Katika robo fainali iliitoa Ufaransa kisha nusu ikaenda kuichapa Jamhuri ya Czech Republic.
Ikakutana na mwenyeji Ureno kwenye fainali na ikashinda kwa bao 1-0.
BAO LA MAAJABU LA VAN BASTEN
Licha ya kufika fainali mbili za Kombe la Dunia katika miaka ya 1970 na kutoa wachezaji kama Johan Cruyff na Johnny Rep, Uholanzi haikuwahi kushinda taji hilo.
Iliingia katika michuano ya mwaka 1980 iliyofanyika Ujerumani ya Magharibi ikiwa kama moja ya timu iliyopewa nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa.
Walianza vizuri kwenye makundi baada ya kuichapa England na Jamhuri ya Ireland, huku
Marco van Basten akiwa shujaa kwenye mechi dhidi ya England alipofunga hat-trick, akaenda tena kufunga bao la ushindi katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya wenyeji.
Fainali ilikutana na Umoja wa Kisovieti.
Dakika ya 32, Ruud Gullit akaifungia Uholanzi bao la kwanza kabla ya Van Basten kupigilia msumari wa pili ulioacha watu vinywa wazi huku ikiripotiwa kwamba ni moja kati ya bao bora kuwahi kufungwa katika mchezo wa fainali ya Euro.
ICELAND ILIPOISHANGAZA DUNIA
Licha ya kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014, Roy Hodgson aliendelea kuhudumu kama kocha wa England na akaliongoza taifa hilo katika michuano ya Euro 2016.
Katika michuano hii England iliingia na vijana mbalimbali waliokuwa kwenye moto kama Raheem Sterling, Eric Dier na Marcus Rashford wakiongozwa na wakongwe kama Joe Hart na Wayne Rooney.
Iceland ambayo haikuwa imewahi kufuzu hapo kabla, iliingia katika michuano ya mwaka huu kama timu isiyopewa nafasi ya kubwa.
Lakini ilishangaza watu wengi baada ya kupita hatua ya makundi na kutinga 16 bora. Pia hapa ilionekana kuwa shughuli yao ndio imeisha kwani ilipangwa na England.
Dakika ya nne tu baada ya mchezo kuanza England ilijipatia bao kupitia penalti iliyopigwa na Rooney, lakini Iceland ikasawazisha dakika ya sita kupitia Kolbeinn Sigporsson kisha dakika ya 18, Skandinavia akafunga bao lapili.
Hadi mchezo unamalizika Iceland ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1 na kufanikiwa kufuzu robo fainali.
Hakuna aliyeamini kutokana na ubora ambao England ilikuwa nao kabla ya kuingia katika michuano hiyo.
DENMARK ILIKUWA BINGWA BILA KUFUZU
Katika mechi za kufuzu michuano ya Euro mwaka 1992, Denmark ilipangwa pamoja na Austria, Faroe Islands, Northern Ireland na Yugoslavia ambapo mshindi mmoja tu ndio alitakiwa kufuzu michuano hiyo iliyofanyika Sweden.
Lakini ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi lao lililoongozwa na Yugoslavia ambayo ndio ilifuzu.
Hata hivyo, siku 10 kabla ya michuano kuanza Yugoslavia iliondolewa baada ya vikwazo walivyowekewa na Umoja wa Mataifa sambamba na vita iliyokuwa inaendelea huko Ulaya maeneo ya Balkans.
Denmark ikapewa nafasi ya Yugoslavia ikiwa na muda mchache wa kujiandaa.
Hakuna aliyefikiria kwamba taifa hili linaweza kufanya chochote, lakini mwisho wa mashindano ndio waliibuka kuwa mabingwa baada ya kuichapa Ujerumani mabao 2-0 katika mchezo wa fainali.