Dar es Salaam. Jumla ya watu 7,639 wamepoteza maisha kwa ajali za barabarani katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2019 hadi Mei 2024.
Katika kipindi hicho, ajali za barabarani zilizotokea zilikuwa 10,093 na majeruhi walikuwa 12,663, miongoni mwao wakipata ulemavu wa kudumu.
Takwimu hizo zimetolewa leo, Alhamisi, Juni13, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema ajali hizo zinaongezeka kutokana na baadhi ya Watanzania kutokuheshimu sheria za barabarani na hawana nidhamu na matumizi ya vyombo vya moto wala alama za barabarani.
“Madhara yake tunapoteza nguvu kazi ya nchi yetu kutokana na ajali za barabarani ambazo zinatuondolea watu wanaotegemewa katika jamii zetu, wakati mwingine kwa uzembe unaoweza kuepukika,” amesema.
Akifafanua kuhusu ajali hizo, amesema za magari binafsi zilikuwa 3,250 ambazo zilisababisha vifo 2,090 na majeruhi 3,177.
Amesema mabasi yalipata ajali 790 zilizosababisha vifo 782 na majeruhi 2,508, daladala ajali 820 zilizoua watu 777 na kujeruhi 1,810.
Kwa upande wa taksi, ajali zilikuwa 93 zilizosababisha vifo 97 na majeruhi 173 wakati magari ya kukodi kwenye sherehe, misiba, na shughuli maalumu) yalikuwa na ajali 326 na jumla ya vifo 263 na majeruhi 302.
Katika kusisitiza hilo, Dk Mwigulu amesema: “Idadi hii kubwa ya majeruhi na vifo vya watu kutokana na ajali utadhani nchi iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Jambo Hili Halikubaliki.”
Amesema ilivyo sasa wengi huona usumbufu na wakati mwingine mpaka wanaweka chuki na uadui wanapokumbushwa kuhusu usalama wao na Jeshi la Polisi wawapo barabarani.
“Unavunja sana sheria barabarani, hata magari ya Serikali hivyo hivyo, wakati mwingine tunawagonga waenda kwa miguu,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amesema “ni wakati sasa jambo hili kuazimiwa na jamii nzima ya Watanzania kwa kuweka mtazamo wa kuchukia ajali. Hatuwezi kuendelea kushuhudia nguvu kazi yetu ikipukutika kirahisi tu kama nyumbu anavyouawa mbugani.”
“Askari barabarani (trafiki) msiwe na huruma hata kidogo kwa wazembe wote wanaokiuka sheria hata kama gari ina usajili wa namba za Serikali.”
Amesema kama sheria zilizopo ni rafiki sana, makosa yote ya ajali barabarani yaondolewe kwenye inayoitwa ‘traffic case’ (makossa ya barabarani), ipelekwe kwenye makosa makubwa zaidi.
“Ikiwezekana huu uwe ni uuaji kama uuaji mwingine, kwa maana mtu anayekufyatulia risasi kwa kukusudia ana uhakika kuwa atakujeruhi au kukuua na hata anayefanya uzembe na vyombo vya moto ana uhakika wa kukujeruhi au kuua kwa makusudi kabisa,” amesema.