Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imependekeza ongezeko la Sh382 kwa kila kilo moja ya gesi asilia inayotumika katika magari kwa ajili kuongeza mapato yatakayotumika kufanya matengenezo ya barabara.
Kutokana na ongezeko kilo moja ya gesi asilia itauzwa Sh1932 kutoka Sh1550 ya awali.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/2025.
Dk Mwigulu amesema hatua hiyo pia imefkiwa ili kuleta usawa kwani magari yanayotumia mafuta tayari yanachangia mapato kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.
“Mapato yatakayotokana na chanzo hiki yatapelekwa Mfuko wa Barabara. Hatua hii inatarajia kuongeza Mapato ya Serikali kwa Sh9.5 bilioni,” amesema Dk Mwigulu.
Pia Dk Mwigulu amependekeza utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya barabara katika kipindi ambacho kutakuwa na punguzo la bei ya mafuta ya petroli sokoni.
Amesema badala ya bei hizo kushuka fedha hizo zitatolewa kwenye mfuko wa barabara huku akifafanua utaratibu huo utatekelezwa na Kamati maalumu itakayoundwa.
Amesema kamati hiyo itaundwa na mawaziri wenye dhamana ya fedha na nishati.
“Hii italenga kupendekeza kiasi kitakachotengwa kwa kuzingatia wastani wa bei iliyopo sokoni. Mapato yatakayotokana na utaratibu huu yatapelekwa Mfuko wa Barabara,” amesema Dk Mwigulu.