Na. OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Rais Samia anawategemea wajumbe wateule wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kumaliza changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu nchini.
Mhe. Mchengerwa amesema hayo, mara baada ya kuwaapisha wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) aliowateua Juni 03, 2024 kwa mujibu wa kifungu 6 (1) cha Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu, sura 448, ikiwa ni baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumteua Prof. Masoud Muruke kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo.
“Mhe. Rais anatarajia mtakwenda kumaliza kero za walimu nchini, hatutegemei kusikia kero yoyote ya mwalimu awe amenyima haki ya kupandishwa daraja au kupata mshahara, hivyo mshirikiane na Katibu Mkuu TAMISEMI kumaliza changamoto za walimu,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, ni dhamira ya Rais Samia pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuona walimu wote nchini wanatendewa haki katika ngazi zote zilizopo chini ya mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa.
“Prof. Muruke Mhe. Rais amekuamini na sisi tunakuamini pia hivyo wewe na wajumbe waliochini yako mjipange kwani tunawategemea mkafanye maboresho ya kusimamia haki na stahiki za walimu ambao ni muhimu sana katika maendeleo ya taifa letu,” Mhe. Mchengerwa amehimiza.
Ameongeza kuwa, anategemea wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) watamshauri Katibu Mkuu TAMISEMI namna bora ya kushughulikia changamoto zinazowakabili walimu ikiwa ni pamoja na masuala ya yanayohusu nidhamu na maadili ya utendaji kazi ya walimu.
Mhe. Mchengerwa amewaapisha wajumbe 8 wa Tume ya Utumishi wa Walimu ambao ni Bi. Mariam Mwanilwa, Bw. Huruma Mageni, Bi. Khadija Mcheka, Bi. Mariam Haji, Bi. Bahati Mgongolwa, Bw. Agrey Mleli, Bi. Jane Mtindya na Bw. Lameck Mahewa.