KUELEKEA SIKU YA KIMATAIFA YA MTOTO WA AFRIKA SERIKALI, WADAU WAFUNGUKA KUHUSU MAADILI, ULINZI WA MTOTO

* Ubalozi wa Ufaransa, Serikali na Wadau kuwakutanisha watoto, kusikiliza maoni yao Juni 16

Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam

KATIKA Kuadhimisha siku ya kimataifa ya mtoto wa Afrika inayoadhimishwa Juni 16 kila mwaka, Wazazi na jamii kwa ujumla wametakiwa kushirikiana katika ulinzi wa mtoto kwa kuhakikisha wanatenga muda wa kuzungumza na watoto na kufahamu changamoto wanazopitia ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili na kuwasaidia kufikia malengo yao kwa maendeleo ya baadaye.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika kituo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Ufaransa nchini ‘Alliance Francaise’ jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo kutoka ATD Dunia ya Nne Tanzania ambao ndio waandaji wa maadhimisho hayo Agatha Makombe amesema;

“Shirika limeandaa maadhimisho haya ikiwa ni sehemu ya njia ya kupaza sauti na kuonesha utetezi wetu kwa watoto, Tunafanya kazi na watoto wanaoishi kwenye mazingira ya umasikini uliokithiri na mwaka huu tumejikita katika elimu jumuishi kwa mtoto ambayo lazima izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi na kwa upande wa wazazi na jamii wanatakiwa kushirikiana bega kwa bega na watoto kwa kuhakikisha mustakabali wao unakuwa mzuri.” Amesema.

Akifafanua kauli mbiu ya mwaka huu ya ‘Elimu Jumuishi kwa Watoto Kuzingatie Ujuzi, Maadili na Stadi za Kazi; Wajibu wa Wazazi na Jamii Katika Kumsaidia Mtoto katika Kufikia Malengo yake kwa Maendeleo ya Baadaye.” Bi. Agatha amesema, wamejikita katika nyenzo ya elimu kwa kuwa humpatia mtoto mwanga, ujuzi na maarifa ya kuweza kutambua alipo na namna ya kupambana dhidi ya hali iliyopo kwa ubora wa baadaye.

Amesema, Jamii ikumbuke na kupasa sauti kwa watoto na kuhakikisha wanapata elimu inayoendana na sayansi na teknlojia itakayomwezesha kwenda sambamba na soko la ajira kwa kuajiriwa au kujiajiri pamoja na kutumia vifaa vya teknolojia ikiwemo kompyuta.

Amesema, ATD imekuwa ikifanya utetezi katika maeneo mbalimbali kwa watoto wanaoishi katika umasikini uliopitiliza pamoja na matatizo mbalimbali ikiwemo magonjwa adimu kwa kuhakikisha wanapata elimu ili mtoto apate haki msingi ya elimu ili kuweza kumkomboa kifikra.

“Pia tumekuwa tukitoa elimu ya teknolojia kwa watoto juu ya namna bora ya kutumia mitandao bila kuleta athari hasi kwa watoto hao, ikiwemo namna ya kujikomboa kiuchumi, kifikra na mitazamo kupitia mitandao ya kijamii.” Amesema.

Pia ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Asasi mbalimbali katika kuhakikisha mtoto wa Afrika anakombolewa katika utumwa wa kifikra na uchumi na nyanja mbalimbali ili kuweza kujenga jamii iliyo bora.

Akizungumzia maadhimisho hayo amesema Kuwa Juni 16, mwaka huu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge ataongoza maadhimisho hayo yatakayohusisha makundi mbalimbali ya watoto, Asasi za kiraia, Ubalozi wa Ufaransa, UNICEF na wanajamii katika Hoteli ya Nefaland jijini humo ili kujadili na kusikiliza changamoto kutoka kwa watoto wenyewe na kupata suluhu dhidi ya changamoto hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Ubalozi wa Ufaransa amesema, maadhimisho hayo yataangazia jukumu la wazazi na walezi pamoja na jamii kwa ujumla katika maendeleo ya mtoto kupitia elimu.

“ Majadiliano yataangazia masuala ya ujuzi, maadili pamoja na stadi za kazi na hii ni pamoja na kuhimiza jamii kuwaongoza watoto katika kutafikia mafanikio yao hapo baadaye.” Ameeleza Mandy.

Aidha ameeleza kuwa, Maadhimisho hayo kwa mwaka 2024 yatawakutanisha makundi mbalimbali ya watoto na kupitia mjadala wa wazi maoni yao yatasikilizwa na kufanyiwa kazi kwa watoto nchini kote kupitia makundi hayo huku masuala ya upendo wa wazazi na walezi kwa watoto, mmomonyoko wa maadili, utandandawazi na matokeo yake, malezi kwa watoto pamoja na suluhu ya kuboresha huduma na ulinzi kwa watoto vitajadiliwa ili kuhakikisha watoto wanakuwa salama.

Vilevile Mratibu wa kitengo cha Maendeleo ya Jamii anayehusika na Dawati la mtoto kutoka Manispaa ya Kinondoni Clara Urasa amesema, katika kumwendeleza mtoto dawati hilo humsaidia mtoto katika shughuli za shule na jamii kwa ustawi wao kwa kuhakikisha analindwa katika kufikia ndoto zao.

Amesema, kupitia mabaraza ya watoto, majukwaa na klabu za watoto wamekuwa wakitoa elimu mbalimbali kuhusiana ma malezi, utu wema, uongozi na maadili ili kuwalinda dhidi ya mabadiliko ya teknolojia katika makuzi yao.

Aidha amesema wanazingatia muongozo wa Taifa unatoa mweleko wa namna ya kuwafundisha watoto dhidi ya mmomonyoko wa maadili na kumfanya mtoto aweze kusimama katika haki zake.

Adela Alex ambaye ni mtoto na mwanaharakati wa haki za watoto amewaomba wazazi na jamii kutenga muda wa kuzungumza na watoto ili kujua changamoto zinazowakabili na hiyo na pamoja wazazi kuepuka migogoro ya kifamilia ili kumlinda mtoto dhidi msongo wa mawazo inayotokana na migogoro anayoishuhudia ndani ya familia hali inayopelekea baadhi ya watoto kujidhuru au kubadilika kitabia.

Maadhimisho hayo yameandaliwa na Shirika linalopambana na umaskini uliokithiri ATD Dunia ya Nne Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ufaransa pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo TASODEC, TAYOBECO, No Limit Foundatiom na Adela Foundation.
 

Mratibu wa kitengo cha  Maendeleo ya Jamii anayehusika na Dawati la mtoto kutoka Manispaa ya Kinondoni Clara Urasa akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani,) na kueleza kuwa katika kumwendeleza mtoto dawati hilo humsaidia mtoto katika shughuli za shule na jamii kwa ustawi wao kwa kuhakikisha analindwa katika kufikia ndoto zao. Leo jijini Dar es Salaam.
 

Ofisa anayeshughulikia masuala ya Asasi za kiraia kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini Bi. Mandy Martel akizungumza wakati wa kikao hicho na kueleza kuwa maadhimisho hayo yataangazia jukumu la wazazi na walezi pamoja na jamii kwa ujumla katika maendeleo ya mtoto kupitia elimu. Leo jijini Dar es Salaam.
 

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo kutoka ATD Dunia ya Nne Tanzania ambao ndio waandaji wa maadhimisho hayo Agatha Makombe akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa ATD wataendea kumtetea mtoto na kumjenga kwa maendeleo ya baadaye. Leo jijini Dar es Salaam.
 

Adela Alex (kulia,) ambaye ni mtoto na mwanaharakati wa haki za watoto akizungumza katika mkutano huo ambapo amewaomba wazazi na jamii kutenga muda wa kuzungumza na watoto ili kujua changamoto zinazowakabili. Leo jijini Dar es Salaam.


 

Matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo.

Related Posts