Dar es Salaam. Mawaziri wa Fedha wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),leo wamewasilisha bajeti kwenye mabunge ya mataifa yao, huku Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ikikadiria ukuaji wa uchumi kwenye ukanda huo kutoka asilimia 3.5 mwaka jana hadi asilimia 5.1 mwaka huu na asilimia 5.7 mwaka 2025.
EAC inaundwa na nchi nane ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan Kusini na Somalia. Hata hivyo, jana, nchi zilizowasilisha bajeti zao kwa wakati mmoja ni Kenya, Tanzania na Uganda.
Nchi hizo zilikubaliana kuwasilisha bajeti zao siku moja, hata hivyo nchi nyingine bado hazijaanza kufuata utaratibu huo kutokana na sababu tofauti.
Katika bajeti zilizowasilishwa jana, Kenya imeendelea kuongoza kwa kuwa na bajeti kubwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku Uganda ikichukua nafasi ya pili ikifuatiwa na Tanzania katika nafasi ya tatu.
Akiwasilisha bajeti ya Serikali ya Kenya, Waziri wa Fedha, Njuguna Ndung’u amesema wanatarajia kutumia Dola 31.1 bilioni (Sh81.28 trilioni) kwa mwaka wa fedha 2024/25 iliyopanda kutoka dola 28.89 bilioni (Sh75.76 trilioni) zilizoidhinishwa Juni mwaka jana.
Bajeti ya Kenya ya mwaka 2024/25 inalenga kukabiliana na deni la Taifa, huku ikilinda kuimarika kwa uchumi wake na ukuaji wake ukikadiriwa kuwa asilimia 5.5 mwaka 2024 na 2025.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni, Ndung’u amesema nakisi ya fedha inatarajiwa kuwa asilimia 3.3 ya pato la Taifa, ikilinganishwa na nakisi iliyofanyiwa marekebisho ya asilimia 5.7 mwaka 2023/24.
Ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuwiana na matarajio ya wizara ya asilimia 5.5 mwaka huu kutoka asilimia 5.6 mwaka 2023.
“Serikali itapunguza kasi ya uchukuaji wa mikopo mipya ya kibiashara ya nje na kufanya shughuli za usimamizi wa mikopo kwa kubadilishana madeni na masuluhisho mengine ya kiubunifu,” amesema.
Jumla ya deni la Taifa la Kenya linafikia wastani wa asilimia 68 ya Pato la Taifa kwa mwaka wa fedha 2023/24, na linatarajiwa kushuka hadi asilimia 64.8 mwaka 2024/25, kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB).
Waziri wa Fedha wa Uganda, Matia Kasaija amewasilisha bajeti bungeni akieleza kwamba Serikali ya Uganda kwa mwaka wa fedha 2024/25, imepanga kutumia Sh72.136 trilioni za Uganda (dola 19.2 bilioni)
Kasaija amesema bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 imeelekezwa kwenye vipaumbele saba muhimu ambavyo ni; kuwekeza kwa wananchi wa Uganda kupitia elimu, afya na maji, usafi wa mazingira.
Eneo jingine lililopewa kipaumbele ni amani na usalama wa watu wa Uganda. Amesema eneo hilo limetenga jumla ya Sh9.107 trilioni, ikijumuisha nyongeza ya asilimia 25 ya mishahara ya wanausalama wote katika cheo cha nahodha na chini yake.
Vilevile, bajeti imeelekezwa kwenye matengenezo ya barabara zote, ujenzi wa barabara chache za kimkakati, pamoja na ukarabati wa Reli ya Kimeta na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambapo kwa pamoja zimetengewa Sh4.989 trilioni.
Waziri Kasaija amebainisha kwamba watawekeza katika mipango ya uzalishaji mali, ikiwa ni pamoja na kilimo cha biashara, uongezaji thamani, mfuko wa mikopo ya kilimo, utalii, utafiti unaozingatia sayansi na ujuzi wa vijana, programu ya kukuza mauzo ya nje na mengineyo ambapo kwa ujumla imetengwa Sh2.641 trilioni.
Akiwasilisha bajeti, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh49.35 trilioni (dola 18.9 bilioni), sawa na ongezeko la asilimia 11.2 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24.
Amesema ongezeko la bajeti kwa kiasi kikubwa limetokana na kugharamia deni la Serikali ambalo limeongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi, kuongezeka kwa viwango vya riba na kuiva kwa mikopo ya zamani, ajira mpya na ulipaji wa hati za madai.
Maeneo mengine yaliyosababisha kuongezeka kwa bajeti hiyo ni uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2025 na maandalizi ya michuano ya mpira wa miguu ya mataifa ya Afrika (Afcon) ya mwaka 2027, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa viwanja.
“Mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa Sh34.61 trilioni, sawa na asilimia 70.1 ya bajeti yote na asilimia 15.7 ya pato la Taifa. Kati ya mapato hayo, mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakadiriwa kuwa Sh29.41 trilioni, mapato yasiyo ya kodi yatakayokusanywa na wizara, taasisi na idara zinazojitegemea Sh3.84 trilioni na mapato yatakayokusanywa na mamlaka za serikali za mitaa Sh1.36 trilioni,” amesema Dk Mwigulu.
Ameongeza kuwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo, inakadiriwa kuwa Sh5.13 trilioni.
Amesema Serikali inakadiria kukopa Sh6.62 trilioni kutoka soko la ndani ambapo Sh4.02 trilioni ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Sh2.60 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Wakati nchi nyingine zikiwasilisha bajeti zao bungeni, Serikali ya Rwanda imetangaza mabadiliko ya Waziri wa Fedha ambapo Waziri Mkuu, Edouard Ngirente alimtangaza ofisa wa Takwimu, Yusuf Murangwa kuwa Waziri mpya wa Fedha akichukua nafasi ya Uzziel Ndagijimana.
Hata hivyo, wakati akiwasilisha mpango wa maendeleo ya Taifa, Mei 25, mwaka huu, Ndagijimana amesema Rwanda inapanga kuongeza matumizi yake kwa asilimia 11 hadi kufikia bajeti ya dola 4.43 bilioni (Sh11.58 trilioni) katika mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai.
Jumla ya dola 1.006 bilioni (Sh2.632 trilioni) katika rasimu ya bajeti ya 2024/25 itatokana na mikopo ya nje, Ndagijimana alisema bila kutoa maelezo juu ya aina gani ya mikopo ambayo Serikali inazingatia.
‘’Kwa ujumla dola 2.942 bilioni (Sh7.7 trilioni) zitatokana na mapato ya ndani na nyingine dola 552.7 milioni (Sh1.445 trilioni) zitatokana na misaada kutoka nje,’’ aliongeza alipokuwa akiwasilisha rasimu ya bajeti bungeni.
Ndagijimana amesisitiza makadirio ya ukuaji wa uchumi wa Serikali wa asilimia 6.6 mwaka huu, asilimia 6.5 mwaka 2025, asilimia 6.8 mwaka unaofuata wa 2026 na asilimia 7.2 mwaka 2027.
Uchumi uliongezeka kwa asilimia 8.2 mwaka jana, na kuvuka lengo lake la awali la ukuaji wa asilimia 6.2.
“Hali ya ukuaji wa Rwanda bado ni kubwa, licha ya mazingira magumu yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, mfumuko wa bei duniani, mvutano wa kisiasa baina ya mataifa, miongoni mwa changamoto nyingine,” amesema Ndagijimana.
Kwa upande wa Burundi inayozalisha madini ya nikeli, itaongeza matumizi kwa asilimia 16 hadi faranga 4.3 trilioni (dola 1.5 bilioni) katika mwaka wa fedha 2024/25 na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 17 kwa kutoza kodi zaidi na kuanzisha mpya kama vile kwenye mafuta ya mawese.
Hata hivyo, nchi hiyo itategemea misaada ya kigeni kuziba pengo lake la ufadhili wa faranga 456 bilioni.