BODI YA TAWA KUJA NA MIKAKATI KABAMBE YA KUIBORESHA HIFADHI YA PANDE

Na Beatus Maganja, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko amesema Bodi anayoiongoza imejipanga kuja na mipango madhubuti ya kuifanya Hifadhi ya Pande iliyopo Jijini Dar es Salaam kuwa kivutio kikubwa kwa watu waishio ndani na nje ya Jiji hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara iliyofanyika Juni 13, 2024 hifadhini humo, Semfuko amesema Bodi yake imedhamiria kuwafanya watanzania waione Hifadhi ya Pande kuwa ni sehemu ya kipekee kwa ajili ya kustarehe na kupumzisha akili zao, na kwa kuanzia imeanzisha bustani wa wanyamapori hai ndani ya hifadhi hiyo ambao wako huru kutembea “free roaming” ikiwa na wanyamapori mbalimbali kama vile nyumbu, pundamilia, swala n.k

Katika hatua nyingine amebainisha mikakati ya kuendelea kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo sambamba na kuongeza aina mbalimbali za vivutio vya utalii ikiwemo wanyamapori aina ya twiga na faru lakini pia kuongeza kasi ya kuitangaza hifadhi hiyo ambapo amesema hivi karibuni TAWA imekuwa ikiwatumia wasanii wa “Bongo Movie” katika kusaidia kutangaza hifadhi ya Pande.

Aidha ametoa wito kwa wawekezaji wote nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo hifadhini humo kama vile ujenzi wa kumbi za mikutano, sehemu za kuchezea watoto na “eco lodge” huku akisisitiza fursa bado zipo.

Naye Prof. Suzanne Augustino mjumbe wa Bodi ya TAWA amesema kwa kuhifadhi Pori la Akiba Pande TAWA inaunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa akihamasisha utalii nchini na amewataka watanzania wote wanaoshindwa kwenda kutalii katika hifadhi zingine kutokana na umbali watembelee hifadhi ya Pande ili kujionea vivutio vilivyopo.

Awali akitoa taarifa ya utendaji wa Kanda, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ya TAWA Sylvester Mushi amesema kutokana na umakini wa kikosi cha Askari wa mbwa na kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wamefanikiwa kudhibiti utoroshaji wa nyara za Serikali uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere ( JNIA ) wakiwemo wadudu aina ya nge 383, wadudu aina ya “Beatle” 261, Kobe hai 7, vichwa vya fisi 10, vichwa vya pimbi 3 na vichwa vya ndege aina ya Korongo 3 na bunduki 2 ambazo zilikamatwa Pori la Akiba Wami Mbiki

Kwa upande wake Kamanda wa Pori la Akiba Pande Dorothy Massawe ameishukuru Mamlaka kwa kuboresha miundombinu ya utalii ambapo amekiri kuwa imekuwa chachu ya ongezeko la mapato na idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo

Related Posts