Wanaume na hatari ya saratani ya koo

Dar es Salaam. Iwapo unapenda vilevi, ikiwemo pombe kali, nyama choma, sigara, pilipili na mapenzi ya kwa njia ya mdomo, unajiweka hatarini kupata ugonjwa wa saratani ya koo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, tafiti zinaonyesha wanaume wana uwezekano wa kupata saratani ya koo mara tatu zaidi ya wanawake.

Saratani hii ambayo hutokea nyuma ya ulimi, inatajwa kuwa hatari zaidi licha ya kuwepo kwa baadhi ya wagonjwa kutibiwa na kupona, changamoto yake kubwa hubainika mtu akiwa katika hatua za juu za ugonjwa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Emmanuel Lugina anasema katika saratani za kichwa na shingo, saratani ya koo la kumezea chakula inachukua nafasi ya saba kati ya zinazowaathiri Watanzania.

Anasema saratani hiyo inaweza kugawanywa katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni lile linalohusishwa na kirusi cha ‘human papiloma virus’ (HPV) na kundi la pili ni lile ambalo saratani ya koo haina uhusiano na kirusi hicho.

“Hii saratani ya koo inayohusishwa na HPV inatokea zaidi kwa vijana. Na inasababishwa na hiki kirusi cha HPV. Kirusi hiki kinasambazwa kupitia kunyonyana ulimi na sehemu za siri wakati wa kujamiiana,” anasisitiza Dk Lugina.

Anataja kundi la pili ni saratani ya koo ambayo haina uhusiano na koo na haina uhusiano na HPV.

Anasema aina hiyo ya saratani inatokea zaidi kwa wazee baada ya kutumia sigara na pombe kwa miaka mingi.

“Tafiti zinaonyesha ukitumia pombe na sigara kwa miaka zaidi ya 20, unakuwa hatarini kupata saratani hii ya koo na huwa inawapata zaidi wanaume,” anasema.

Daktari huyo bingwa anasema kati ya wagonjwa wanne wanaougua saratani hiyo, watatu huwa ni wanaume.

Anasema hiyo ni kutokana na matumizi makubwa ya sigara na pombe miongoni mwa wanaume.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Kinga katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Crispin Kahesa anasema asilimia 90 ya wagonjwa wa saratani ya koo wana historia ya uvutaji sigara, unywaji pombe kali na kula aina za vyakula vilivyochomwa, ikiwamo nyama na samaki, ulaji wa pilipili, ndimu, ‘chilisosi’ na unywaji wa vitu vya moto kupita kiasi.

“Ongezeko ni kubwa, asilimia 90 ya wagonjwa tuliowapokea hapa wana historia ya kutumia vilevi vikali, sigara, pilipili kwa wingi na aina nyingine na vitu vinavyosababisha saratani hii,” anasema Dk Kahesa.

Daktari bingwa wa saratani kutoka Aga Khan, Nuru Saleh anasema saratani hiyo hutokea nyuma ya ulimi na mara nyingi husababishwa na virusi vya HPV.

Anasema virusi hivyo vikifika pale huweka makazi na kuanza kubadilisha mazingira ya zile seli ambazo vimezikuta na kusababisha saratani eneo hilo.

“Saratani ya koo inawapata zaidi watu wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea, lakini hii saratani inayosababishwa na virusi inawapata zaidi vijana, hasa wa kiume. Kuvuta sigara, aina za magonjwa ya kwenye vinasaba yanaweza kusababisha hiyo saratani.”

Anataja vichochezi kuwa ni ngono ya mdomo, pombe kali, sigara, kula vitu vya moto sana iwe ni maji, chai, maziwa yanakwangua ile ngozi ya juu laini na baadaye kutengeneza vidonda vinavyoweza kugeuka na kuwa saratani.

Dk Lugina anazitaja dalili za saratani ya koo kuwa ni pamoja na kupata shida wakati wa kumeza chakula, maumivu wakati wa kumeza, kusikia kama umekwamwa na donge kooni.

Akielezea kinga ya ugonjwa huo, anasema ni kuepuka matumizi pombe na sigara.

“Wanaume kwa wanawake wanatakiwa kuepuka kunyonyana sehemu za siri na kunyonyana mate na watu usiofahamiana nao,” anasema.

Dk Lugina anasema chanjo ya HPV wanayopewa watoto wa kike kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi, itawapunguzia pia hatari ya saratani ya koo.

Pamoja na hayo, anataja tiba ya saratani kuwa ni upasuaji kuondoa uvimbe na kisha kupewa tiba mionzi na tiba kemia.

“Hii saratani huwatokea zaidi wanaume kutokana na matumizi makubwa ya pombe na sigara miongoni mwa wanaume, ikilinganishwa na wanawake.

Kwa mara ya kwanza mwaka 1983 hadi 1992, Taasisi ya Afya ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ilifanya utafiti na kubaini kuwa kati wagonjwa 546 waliopimwa, kulikuwa na wastani wa wagonjwa 116 wanawake, huku 430 wakiwa ni wanaume.

Utafiti huo ulifanywa na Dk Henry Mwakyoma kwa kushirikiana na Dk N Mbebati, Dk M Aboud, Dk J Kahamba na Dk C Yongolo uliokamilika Juni 1, 1994, ambao ulibaini ukuaji wa saratani ya koo Kanda ya Kaskazini kwa watu wenye umri kati ya miaka 50-59.

Watu wenye umri kuanzia miaka 21 hadi 90 walishiriki na wagonjwa wengi walikuwa wenye umri wa miaka 50-59, hali ambayo ni tofauti na sasa ambapo ni kuanzia miaka 30 hadi 50.

Related Posts

en English sw Swahili