Yaliyojiri safari ya kwanza treni ya umeme Dar-Morogoro

Dar/Morogoro. Ilikuwa safari ya dakika 114 zenye bashasha, abiria zaidi ya 600 wakiwa kwenye mabehewa 14 ya treni ya umeme iliyoanza safari ya kwanza leo Juni 14, 2024 ikiongozwa na nahodha, Ahazi Mfupa.

Treni iliondoka Dar es Salaam saa 12:01 asubuhi na kuwasili Morogoro saa 1:55 asubuhi.

Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema safari hiyo imehusisha mabehewa 14, matatu yakiwa ya daraja la juu.

 “Tumekuja na abiria kama 600 hadi 700, mabehewa mengi yalikuwa yamejaa, ingawa hadi yote 14 yajae tungefika 1,000,” amesema Kadogosa katika mahojiano na Mwananchi Digital.

Katika stesheni ya SGR Dar es Salaam, abiria walianza kuwasili saa 11.00 asubuhi. Kila aliyesafiri kabla ya kuingia ndani treni alikaguliwa kwa kutumia skana.

Ilipofika saa 11.30 asubuhi, kulitolewa tangazo kuwataka abiria wanaosafiri waendelee kuingia ndani ya treni.

Matangazo yaliendelea hadi dakika tano kabla ya safari kuanza.

Ilipofika saa 12.01 asubuhi treni ilianza safari kuelekea Morogoro.

Ilipofika Kituo cha Pugu, ilisimama kwa dakika mbili na kupakia abiria wachache waliokuwa kituoni hapo.

Baadhi ya abiria wakiwa ndani ya treni iliyoanza safari ya kwanza kutoka Jijini Dar es Salaam kwenda Morogoro.

Mbali na kituo hicho, pia ilisimama kwa dakika mbili kwenye vituo vya Soga na Ngerengere kabla ya kuwasili stesheni ya Kihonda.

Tofauti na wakati wa safari ya majaribio Februari 27, 2024 iliyotumia saa 2.20, leo ikiwa ni safari ya kwanza ya abiria treni hiyo imetumia saa 1:55 kufika Morogoro.

Maswali ya wengi ilikuwa ni namna ya kukata tiketi. Kadogosa amesema abiria anaweza kukata kwa njia ya mtandao au dirishani kwenye ofisi za TRC.

Japo kulikuwa na sintofahamu ya nauli, Kadogosa amesema Sh13,000 kwa daraja la kawaida ni nauli rafiki.

“Hii ni treni ya Watanzania, zimewekwa nauli rafiki watu kuzimudu,” amesema.

Vyakula, vinywaji marufuku

Katika usafiri huo, hairuhusiwi kuingia na kinywaji chochote wala chakula.

Mmoja wa wahudumu katika treni hiyo, Zuhura Milala amesema kila kitu kinapatikana ndani ya treni na kwenye stesheni.

Japo katika safari ya leo, waliotumia vinywaji walikuwa wachache, ikielezwa huenda ni kutokana na wengi kutokuhitaji kutokana na muda waliosafiri na mabehewa mengi hakuna aliyeulizia.

Nahodha aliyeendesha treni hiyo, Ahazi Mfupa amesema hakuwa anafahamu kama yeye ndiye atakayekabidhiwa jukumu hilo hadi siku chache kabla ya safari.

“Tuko manahodha waandamizi wengi, nilichaguliwa mimi na mwenzangu mmoja kuendesha treni hii, nashukuru Mungu safari yetu imekuwa nzuri na tumefika kwa muda tulioutarajia,” amesema.

Mfupa amesema wametembea kwa mwendo wa juu wa kilomita 155 kwa saa ingawa treni hiyo uwezo wake wa juu ni kilomita 160 kwa saa.

Wakizungumzia usafiri huo, baadhi ya abiria wamesema imekuwa na mwanzo mzuri.

“Huduma tuliyoipata leo ikiwa endelevu ni usafiri mzuri, maana abiria unafika unapokewa vizuri na kila hatua ya safari mnaelezwa,” amesema Noela Alphonce, mkazi wa Dar es Salaam.

Abiria mwingine, Albert John amesema aliposikia treni inaanza safari leo, aliamua kukata tiketi na kusafiri.

“Sikutaka nisimuliwe, nimeamua kutumia tu pesa yangu kuja na kurudi ili nijionee mwenyewe usafiri huu ulivyo,” amesema.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile aliwahimiza Watanzania kutumia vema usafiri huo kwa usafi na ulinzi kwa kuwa ni kitu chao.

Related Posts