Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Iringa imemuachilia huru Dotto Kisinga, aliyekuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumwingilia kingono binti yake mwenye umri wa miaka sita, baada ya kubatilisha hukumu iliyomtia hatiani.
Dotto alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya Iringa baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kujamiiana kinyume na kifungu cha 158 (l) (a) na 161 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, alitenda kosa hilo Aprili 15, 2023, wakati mama wa mwathirika alipokwenda mashine kusaga unga na ndugu zake wa kiume walipokuwa wamekwenda kucheza.
Hata hivyo, Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Ilvin Mugeta, Jumanne Juni 11, 2024, kufuatia rufaa aliyoikata Dotto, imemuondolea hatia hiyo baada ya kutilia shaka ushahidi wa upande wa mashtaka hasa wa mtoto mwathirika.
Kwa mujibu wa ushahidi katika kumbukumbu za Mahakama, mtoto huyo anaishi na wazazi wake na ndugu zake wengine wawili wa kiume.
Mtoto huyo aliibua taarifa za kuingiliwa na baba yake Aprili 17, 2023, mbele ya Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashari ya Wilaya Iringa anayeshughulikia dawati la wenye uhitaji maalumu wakiwamo watoto, Gladness Amulike ambaye ni shahidi wa kwanza upande wa mashtaka (SMI).
Siku hiyo, Amulike alifika Shule ya Msingi Ulata kutoa elimu kuhusu usalama wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia, akiwa na askari polisi G.3553, CPL Salum, (SM3) katika kesi hiyo.
Baada ya kutoa elimu hiyo, ndipo mtoto huyo (SM2) alijitokeza na kueleza kuwa baba yake humwingilia kingono na ameshafanya hivyo mara sita na kwamba wakati mwingine hufanya hivyo mchana watu wanapokuwa hawapo nyumbani.
Alidai kuwa, mwaka 2022 alimuingilia mara tatu na alimtishia asiseme chochote.
Hata hivyo, alimfahamisha mama yake juu ya tukio hilo lakini hakuchukua hatua ingawa kutokana na athari hizo za kuingiliwa alikuwa akimtibu majeraha ya kutoka damu sehemu yake ya siri.
Amulike baada ya kuwahoji watoto wawili wa kiume na wao walikiri kulawitiwa.
Mtoto huyo alifanyiwa uchunguzi na Daktari Kelvin Prosper Maro ambaye alibainisha kuwa, alikuwa na dalili za kuingiliwa kwa vile sehemu yake ya siri ilikuwa wazi na bikra haikuwepo, lakini hakuona michubuko.
Hivyo, mtuhumiwa alitiwa mbaroni na kisha akapandishwa kizimbani na kusomewa shtaka hilo.
Mbali na mshtakiwa katika ushahidi wake kupinga ushahidi wote wa upande wa mashtaka, mama wa mtoto huyo ambaye ni shahidi wa pili wa utetezi (SU2) alikana kuambiwa na mtoto wao kuingiliwa na babake wala kumtibu kwa dawa za kienyeji.
Mahakama ya Wilaya ilipuuza ushahidi huo akieleza kuwa, utetezi haukutikisa ushahidi wa mashtaka badala yake iliridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka na ikamtia hatiani na kumhukumu kutumikia adhabu hiyo ya kifungo cha maisha jela.
Rufaa na hoja zilizotolewa
Hata hivyo, Dotto alikata rufaa akipinga hukumu yote yaani hatia na adhabu, huku akitoa sababu tisa za rufaa ambazo hoja ya msingi alidai kuwa mashtaka dhidi yake hayakuthibitishwa bila kuacha shaka ya msingi.
Siku ya kusikiliza rufaa hiyo, mrufani, Dotto alieleza kwamba hajui kusoma wala kuandika, hivyo aliomba maelezo yake ya maandishi aliyoandaliwa na wenzake gerezani yapokewe na Mahakama iyatumie kama hoja zake kuunga mkono sababu zake za rufani.
Hoja yake kubwa ilikuwa kwamba hakuna ushahidi kuwa tukio lilitendeka Aprili 15, 2023 kama inavyodaiwa kwenye hati ya mashtaka.
Wakili wa Serikali, Winfrida Mpiwa alieleza kuwa jamhuri inaunga mkono rufaa hiyo kwa kuwa shtaka halikuthibitika kwa kuwa katika ushahidi wake, mtoto mwathirika hakueleza tarehe ya tukio, bali tarehe ya tukio ilitajwa na shahidi mpelelezi ambaye ushahidi wake ni wa kuambiwa.
Alieleza kuwa, pale ambako tarehe na muda wa tukio vimetajwa katika hati ya mashtaka, lazima vithibitishwe katika ushahidi na kwamba katika kesi hiyo, ushahidi huo haupo.
Jaji Mugeta amekubaliana na hoja ya mrufani kwamba tarehe ya tukio iliyotajwa kwenye hati ya mashtaka haikuthibitishwa na kwamba kutothibitisha tarehe ya tukio maana yake shtaka halikuthibitishwa.
Amesema shahidi wa kwanza na wa tatu wa upande wa mashtaka walijaribu kueleza tukio lilivyotendeka, lakini akasema ushahidi wao ni wa kuambiwa na mwathirika au ndugu zake wa kiume ambao hata hivyo hawakuletwa mahakamani kutoa ushahidi.
Jaji Mugeta amesema kinachosikitisha maelezo mazuri ya mashahidi hao kuhusu tukio lilivyotendeka, muda na mahali, hayako katika ushahidi wa mwathirika.
“Kama mwathirika (SM2) aliweza kuyasema haya yote kwa SM3 (mpelelezi) na mengine mengi kwa SMI (ofisa ustawi wa jamii), inasikitisha kwamba hakuyasema mahakamani. Habari za muda wa tukio, usiku au mchana, kutishiwa na kutibiwa na mama yake kwa dawa za kienyeji hazipo,” amesma Jaji Mugeta.
Hivyo, amesema ushahidi wa mashahidi hao kuhusu tukio kwa kuwa ni wa kuambiwa, haukubaliki chini ya kifungu cha 62 cha Sheria ya Ushahidi.
Jaji Mugeta amesema hakimu aliyesikiliza kesi hiyo alipuuza ushahidi wa mama wa mwathirika huyo aliyekana kuambiwa taarifa za mtoto huyo kuingiliwa wala kumtibia kwa dawa za kienyeji, bila hata kueleza ni ushahidi upi wa utetezi na kwa nini anaona ushahidi wa mashtaka haujatikiswa.
Hivyo, Jaji Mugeta amesema anakubaliana na hoja ya mrufani kuwa utetezi wa mrufani haukuzingatiwa kwa sababu hukumu inayolalamikiwa haina uchambuzi wa kina wa utetezi.
Amesema hakimu angezingatia ushahidi wa utetezi angeona kwamba ushahidi alioutumia kumtia hatiani mrufani ulikuwa ni wa kuambiwa na ulikanushwa barabara na utetezi wa mrufani.
“Katika utetezi wake mrufani alisema kama mwathirika angekuwa ameingiliwa kinguvu, uke wake ungechanika na asingeweza kutembea sawasawa kwa kuzingatia umri wake,” amesema Jaji Mugeta.
“Ninakubaliana na hoja hii. Mtoto wa miaka sita hawezi kuingiliwa kingono na mtu mzima akabakia salama. Katika ushahidi wake daktari (SM4) alisema uke haukuwa na michubuko.”
Jaji Mugeta amesema kuwa, ameshindwa kumwamini mtoto huyo kuwa aliingiliwa na baba yake na asimweleze mama yake na kwamba kitendo cha mama yake kusimama dhidi yake kinaashiria kuwa mtoto huyo alisema uongo.
“Kwa umri wake na kwa kuzingatia mazingira ambayo tuhuma iligunduliwa, ushahidi wake unapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari. Rufaa hii ina mashiko, imeshinda. Mahakama ya chini ilipotoka katika kuchambua ushahidi na kumpata mrufani na hatia,” amesema Jaji Mugeta na kuhitimisha:
“Kwa sababu hiyo hatia hiyo nimeifuta na adhabu yake nimeibatilisha. Mrufani aachiliwe huru mara moja isipokuwa kama kuna sababu nyingine, tofauti na amri ya kesi hii, ya kuendelea kumshikilia gerezani.”