Serikali yazungumzia nishati safi ya kupikia

Dar es Salaam. Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis   amesema ajenda ya nishati safi ya kupikia inalenga kuokoa mazingira na kuiondoa Tanzania katika athari zaidi za mabadiliko tabianchi.

Khamis amesema bado kuna watu wanaamini ili upike chakula kizuri ni lazima upike katika kuni na mkaa na wanaona kukata miti ni haki yao.

Akizungumza kwenye Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi linalofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo Ijumaa, Juni 14, 2024 amesema ni lazima watu wafundishwe namna ya kulinda mazingira na kutumia nishati mbadala badala ya kuni na mkaa.

“Kuna watu wanadhani kukata mti siyo kosa bali sehemu ya wajibu wao na ukiwauliza kwa nini wanasema watapikaje. Wanaamini ili chakula kiive lazima mtu atumie kuni au mkaa, ili apike chakula kizuri lazima atumie kuni na mkaa, hivyo hatuwezi kufanikisha kampeni ya nishati safi kama watu hawajaelimishwa vya kutosha,” amesema Khamis.

Ametoa kauli hiyo ikiwa tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameweka lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya wanawake wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.

Khamis amesema athari za ukataji miti hazionekani kwa siku moja huku akieleza kuwa, mtu anaweza kukata miti miaka 10 athari yake ikaonekana miaka 100 ijayo.

Kuhusu namna gani mazingira yanaathiriwa Khamis amesema zaidi ya asilimia 80 ya shughuli za kibinadamu zinachangia uhatibifu wa mazingira ikiwamo shughuli za viwanda, mifugo, kilimo, kazi za uchimbaji madini.

“Shughuli hizi zinaathiri vitu vingi mfano vyanzo vya maji, bado kuna changamoto kwa baadhi ya watu kutiririsha maji machafu kwenye vyanzo vya maji jambo linaloathiri ikolojia ndani ya vyanzo vya maji,” amesema Khamis.

Amesema watu wanafanya shughuli katika vyanzo vya maji licha ya kuwapo kwa sheria ya kuwataka shughuli hizo zifanyike kuanzia mita 60, lakini bado wanalima kwenye vyanzo vya maji jambo linalofanya viuatilifu na sumu zinazotokana na kilimo kuingia katika vyanzo vya maji.

“Maziwa, mito inaanza kukauka vyanzo vingi vimeanza kukauka kwa sababu ya shughuli za kibinadamu, kuna watu wanafuga, watu wanafanya shuguli zao za madini za uchenjuaji wanaingiza maji katika vyanzo vya maji, baadaye tunakuja kujiuliza wapi magonjwa kama kipindupindu yanatoka wapi,” amesema Khamis.

Khamis amesema ni vyema watu wakafundishwa namna ya kulinda vyanzo vya maji ikiwa ni hatua ya kukabilina na mabadiliko tabianchi.

Kuhusu misitu amesema Serikali imetoa maelekezo ya halmashauri nchini ipande miti milioni 1.5 kila mwaka, lakini changamoto iliyobainika ni kukosekana kwa ufuatiliaji.

Hata hivyo, ameonesha bado kuna kulegalega katika usimamizi wa sheria za mazingira jambo linalofanya mazingira yaendelee kuwa machafu.

“Watu wa NEMC (Baraza na Usimamizi wa Mazingira) tusaidieni watu wafuate sheria, hatusimamii sheria zetu, kama tunasimamia vizuri sheria za mazingira miji itakuwa safi, tofauti na sasa utaweka kontena la taka watu watakuja watatupa nje kwa sababu hatusimamii sheria,” amesema Khamis.

Naibu waziri huyo, ametumia nafasi hiyo kuomba wadau mbalimbali wa mazingira kufanya kongamano la mazingira visiwani Zanzibar ili watu wajifunze namna ya kulinda mazingira.

“Tupange tukafanye kitu hiki upande wa Zanzibar kwa sababu shughuli za uchumi wa buluu zinaleta maendeleo makubwa, lakini upande mwingine zinaleta changamoto hasa katika upande wa mazingira katika bahari ambako zinafanyika,” amesema Khamis

Related Posts