Hatimaye michuano ya mataifa barani Ulaya Euro 2024 inaanza kutimua vumbi mjini Munich. Wenyeji Ujerumani wataanza Euro 2024 dhidi ya Scotland, mwanzo wa safari ambayo mabingwa hao mara tatu wa Ulaya wanatumai itakuwa mwanzo wa safari ya kuelekea fainali ya michuano hiyo huko Berlin mnamo Julai 14.
Soma zaidi. Michuano ya Kombe la EURO 2024 kufungua pazia leo Ujerumani
Ujerumani ambayo katika michuano mitatu iliyopita wamekuwa na matokeo mabaya pamoja na kuishia katika hatua ya makundi kwenye Kombe la Dunia la 2018 na 2022 leo wanayebeba matumaini ya Wajerumani kuirejesha imani kwa kupata ushindi katika mechi yao ya ufunguzi. dhidi ya Scotland.
Kocha wa Ujerumani Julian Nagelsmann anayo kazi ya ziada ya kukiongoza kikosi cha Die Manschaft katika kundi A linalozijumiuisha timu za Hungary na Uswizi. Kikosi cha Ujerumani kinaongozwa na mchanganyiko wa wakongwe kama Toni Kroos, Ikay Gundogan ambaye pia ni nahodha na Manuel Nuer lakini pia wapo vijana wadogo kama Florian Wirtz na Jamal Musiala ambao wanatarajiwa kutamba katika michuano hii.
Julian Nagelsmann: Tuko tayari kwa michuano
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Kocha wa Ujerumani Julian Nagelsman amesema ”Ni kweli lipo shinikizo kwa sababu ya mashindano yenyewe lakini muhimu kwetu ni kushinda mechi hii muhimu na wachezaji wetu wako tayari kuyasaka matokeo bora kuliko mashindano yaliyopita hasa ukizingatia tuko nyumbani”.
Kwa upande mwingine kocha wa Scotland, Steve Clarke amesema kuwa wanajua wanachotakiwa kukifanya uwanjani hii leo na kwamba hawaiogopi Ujerumani ingawa wanatanguliza heshima kwa wapinzani wao Ujerumani hii leo.
Soma zaidi. DFB yamuunga mkono Nagelsmann kwa kuendelea kuwa na imani na Neuer
Michuano ya Euro 2024 ni michuano ya pili kwa Scotland tangu 1998. Walirejea kwenye mashindano ya Euro 2020 lakini walimaliza mkiani mwa kundi, na kuambulia pointi yao moja pekee katika sare ya 0-0 dhidi ya England.
Mchezo wa ufunguzi utachezwa katika uwanja wa Allianz Arena nyumbani kwa Bayern Munich kuanzia majira ya saa saa nne za usiku kwa saa za Afrika ya Mashariki.