Utekaji wagombea waibuka mjadala kanuni za uchaguzi

Dodoma. Wadau wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa wametoa angalizo kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea, wakitaka uchunguzi wa mazingira ya uwepo wa mgombea mmoja.

Hili limeelezwa wakati Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikiwa imetoa rasimu za kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba, mwaka huu.

Angalizo wamelitoa Juni 14, 2024 kwenye mkutano wa viongozi wa dini, asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali wa kujadili rasimu ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2024.

Mkutano huo umeandaliwa na Tamisemi na kuhudhuriwa pia na Naibu Mawaziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange na Zainab Katimba.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima ametaka uwazi uwepo wakati wa uteuzi wa wagombea.

Amesema inapotokea kuna mgombea mmoja, mazingira yaangaliwe ili isije ikawa mtu amejenga mazingira ya kubaki pekee yake.

“Tuliona chaguzi zilizopita watu wanatekwa, wanafichwa na mengine kama hayo ambayo si ya uadilifu, sasa mazingira hayo pia yaangaliwe nadhani kwenye wizara kuna utaratibu utakaotumika,” amesema.

Askofu wa Kanisa la Baptist Tanzania, Anthony Mlyashimba amesema uchaguzi uliopita ilizuka tabia ya kutekana na wasimamizi kujificha wakati wa urejeshaji fomu za wagombea.

“Labda na yenyewe ingezungumzwa, pawe na uwazi kuwa msimamizi akijificha basi nini kifanyike,” amesema.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani, Askofu Israel Maasa ameshauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kujizatiti kiasi cha kutokutumiwa na wagombea.

“Wakati mwingine unaona mgombea ana mkutano lakini anakamatwa asubuhi na kupelekwa Takukuru lakini anakaa hadi mkutano unaisha anaachiwa. Sisi kama watu ambao tunashughulika na amani unakuta hilo jambo linapoteza amani. Tungeomba Takukuru kabla ya kumkamata mgombea watumie muda kujiridhisha,” amesema.

Amesema kwa kumkamata mkutano huharibika na huwaondolea amani wanachama.

Ameshauri viongozi wa dini kuwa sehemu ya waaangalizi wa uchaguzi huo, jambo ambalo litasaidia kujibu kelele ambazo zinaweza kujitokeza baada ya uchaguzi.

Unyanyasaji na ukatili wa kijinsia

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Women in Social Entrepreneurship (Wise), Astronaut Bagile, amesema kanuni zinaenda kuwakaba wanaokejeli, matusi na vitisho kwa wanawake, jambo ambalo lilikuwa ni kikwazo kwa wengi.

“Niwahamasishe wananchi wajitokekeze kupiga kura muda utakapowadia na wenye nia na maono ya kuwa viongozi wajitokeze kwa sababu Serikali imeweka mazingira mazuri kwa kila mtu kwa nafasi yake kwa kundi tofauti aweze kushiriki kuwania nafasi za uongozi,” amesema.

Mtaalamu wa Usawa wa Kijinsia wa UN Women Tanzania, Stella Manda amependekeza kuainishwa ni makosa gani ya unyanyasaji wa jinsia yanayokatazwa kupitia kanuni hizo.

Awali, akifungua kikao hicho, Naibu Waziri wa Tamisemi, Dugange amesema sheria ya Serikali za Mita inampa dhamana waziri mwenye mamlaka za mitaa kuandaa kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ajili ya kusimamia uchaguzi huo.

“Kanuni hizo zitawasilishwa kwenu kwa ajili ya kupata maoni. Nimeona nianze kwa kutoa ufafanuzi huu ambao mara nyingi maeneo mbalimbali tumekuwa tukipata hoja za wadau kuwa ni namna gani mamlaka hii inahusika na uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” amesema.

Dk Dugange alisema rasimu wanazozitolea maoni zimeshirikisha maoni yaliyoliyowasilishwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Alisema ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametaka uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024, kuwa huru na haki na kwamba rasimu hiyo imezingatia maoni ya wadau.

“Ni dhamira ya Serikali na Rais Samia na ameelekeza maandalizi ya kanuni hizo yanawezeshwa uchaguzi wa mwaka 2024 kuwa uchaguzi huru n awa haki,”alisema.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Tamisemi, Kadeti Mihayo alisema taasisi zitakazotoa elimu ya uraia zitatoa kwa gharama zao na pia kutakuwa na waangalizi wa ndani wa uchaguzi ambao wataomba kufanya hivyo.

Related Posts