Hofu inazidi kuongezeka kuhusu uwezekano wa kutokea vita kamili kati ya wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon na Israeli.
Tangu shambulio lililofanywa na Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023, ambalo liliua takriban watu 1,200, hali katika mpaka wa Israel na Lebanon imezidi kuwa ya wasiwasi.
Mapema mwezi Juni, mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliripoti kuwa Israel ilirusha mabomu ya fosforasi kulenga miji ya Lebanon. Jambo ambalo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Wakati huo huo, Hezbollah ilirusha zaidi ya maroketi 160 ndani ya Israel, ili kulipiza kisasi dhidi ya Israel kwa kuwaua makamanda wao wawili.
Soma pia: Kundi la Hezbollah ladai kuishambulia Israel kwa roketi
Hali hii imezusha wasiwasi kwamba machafuko kwenye mpaka yanaweza kugeuka kuwa vita kamili.
Viongozi wa siasa kali Israel wataka Hezbollah kushambuliwa
Kutokana na mvutano huo uliopo kwenye mpaka, wanasiasa kadhaa wenye msimamo mkali wa Israel, tayari wamesema hadharani kwamba Israel inapaswa kushambulia Hezbollah.
Uchunguzi wa maoni wa hivi majuzi ulionyesha kuwa zaidi ya asilimia 60% ya raia wengi wa Israel wanakubaliana na msimamo huo.
Soma pia: Watu 37 wauawa Gaza katika shambulizi la Israel
Haijulikani ikiwa vita vikubwa zaidi vitazuka. Juhudi za sasa za kidiplomasia za kimataifa zinalenga kuzuia hilo.
Wataalam wengi wanahoji kuwa wakati Israel inapoendelea na operesheni zake za kijeshi huko Gaza, haitakuwa busara ya kimkakati kwake kufungua uwanja mwingine wa vita na Hezbollah.
Isitoshe, wanahoji kuwa Hezbollah, kundi ambalo nchi kadhaa ikiwemo Marekani na Ujerumani zimeliorodhesha kuwa kundi la kigaidi, lina uwezo, silaha na nguvu zaidi kuliko Hamas ambalo pia limeorodheshwa kuwa la kigaidi huko Gaza.
Mzozo wa Israel na Hamasumeendelea kuwa pasua kichwa na changamoto kubwa katika Mashariki ya Kati.
Wakaazi wa mpakani waingiwa wasiwasi
Wakati wimbi la karibuni zaidi la mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wenye makao yake nchini Lebanon, Hezbollah, yalipoanza, Malak Daher, mwanamke kutoka Lebanon alitarajia lingedumu kwa siku chache tu.
Soma pia: Blinken ataka suluhisho la kidiplomasia kati ya Israel na Lebanon
Lakini mapigano kati ya Hezbollah, na majeshi ya Israel bado hayajamalizika. Kwa hakika, katika wiki chache zilizopita, inaonekana kuwa yameongezeka.
Mamlaka ya Lebanon inasema kumekuwa na zaidi ya vifo 375 nchini humo tangu Oktoba 2023, wakiwemo raia 88, kutokana na mashambulizi ya Israel.
Jeshi la Israel kwa upande wake limesema wanajeshi wake 18 na raia 10 wameuawa kufuatia mashambulizi ya Hezbollah.
Soma pia: UN yaishtumu Israel kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, Hamas kwa uhalifu wa kivita
Maelfu wakimbia mpaka wa Israel na Lebanon
Wakati huo huo, makumi ya maelfu ya raia, karibu 100,000 wa Lebanon na zaidi ya 60,000 Waisraeli, wanaoishi pande zote mbili za mpaka wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano.
Daher, mwenye umri wa miaka 30, ambaye alihamishwa kutoka mji wa kusini wa Mais al-Jabal, ulioko karibu na mpaka wa Lebanon na Israel ambako mapigano yamejikita, amesema ni vigumu sana kuwa mbali na maisha yako, “unahisi kama maisha yako yamesimama.
Soma pia: Vikosi vya Israel bado vyaushambulia mji wa Rafah
Baada ya vita viwili vya 1996 na 2006 ambavyo havikumalizika, vikosi vya Israel na Hezbollah vimekuwa vikifanya mashambulizi ya ‘nipige nikupige’ katika himaya ya kila upande, lakini bila ya kutokea vifo vingi.
Daher alinusurika katika vita vya mwaka 2006 kusini mwa Lebanon kati ya Israel na Hezbollah.
Lakini anapokadiria machafuko ya wakati huo na ya sasa, anaona ya 2006 kama si kitu, ikilinganishwa na mzozo wa sasa.