Lindi. Watu wawili wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia kwa kunyongwa na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Mnimbila kilichopo Kata ya Kilangala mkoani Lindi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Ijumaa Juni 14, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori amesema tukio hilo lilitokea Juni 13, 2024 saa moja jioni katika Kitongoji cha Likahakwa, Kijiji cha Mnimbila wilayani hapa.
Kamanda Imory amewataja waliofariki dunia kuwa ni Muhidini Mangunga (69) na mtoto wake, Ramadhani Muhidini (10) aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kitomanga.
“Wauaji walimuua Muhidini kwa kumnyonga shingoni kwa kutumia shati lake na kumpigwa na kitu chenye ncha kali kichwani kisha kufunikwa na majani makavu shambani kwake.
“Pia, mtoto wake, Ramadhani alinyongwa shingoni kwa kutumia waya wa umeme wa sola na mwili wake kutupwa vichakani,” amesema Kamanda Imory.
Kamanda huyo wa polisi amefafanua kuwa mwili wa Muhidini ambaye ni baba wa Ramadhani, umekutwa ukiwa umelazwa kifudifudi huku umefunikwa na majani.
Pia, kamanda amesema mwili wa Ramadhani umekutwa ukiwa umetupwa vichakani pembeni na njia ya kuelekea mashambani akiwa na waya shingoni.
Majirani ambao hawakutaka kutaja majina yao wamesema marehemu hao hawakuonekana nyumbani kwao kuanzia Juni 12, 2024 na ilipofika Juni 13, 2024 wananchi waliamua kufanya msako kwa kuzungukia maeneo ya jirani na nyumba ya familia hiyo kuwatafuta, ndipo walipokuta miili hiyo shambani kwao.
“Ilipofika Juni 13, tulianza kufanya msako kwa kuzunguka mashambani na maeneo ya jirani kwao na kukuta miili ya marehemu hao ikiwa imefunikwa na majani shambani kwao,” amesema mmoja wa mashuhuda hao.
Miili ya marehemu hao imefanyiwa uchunguzi na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kitomanga, Dk Kasinge Mwemezi na kubaini vifo hivyo vimetokana na kukosa hewa baada ya kunyongwa.
“Sababu ya vifo vya hawa marehemu ni kukosa hewa baada ya kunyongwa na miili tumeikabidhi kwa ndugu zao kwa ajili ya utaratibu wa mazishi,” amesema Dk Mwamezi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limewataka wananchi kuacha mara moja kujichukulia sheria mkononi na kuishi kwa kuwekeana visasi.