CCM Geita yapata pigo, diwani wake afariki

Geita. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita kimepata pigo baada ya Diwani wa Kamena,  Peter Kulwa  kufariki dunia.

Diwani huyo alikuwa akisumbuliwa na kisukari kwa muda mrefu.

Kulwa amekuwa diwani wa tatu kupoteza maisha tangu kuanza kwa baraza la madiwani kwa kipindi cha 2020/24 akitanguliwa na aliyekuwa Diwani wa Bugalama, Masalu Luponya na Diwani wa viti maalumu Kata ya Bukoli Rehema Omary waliofariki mwaka 2021.

Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Geita, Charles Kazungu amethibitisha kutokea kwa kifo hicho Juni 13, 2024  wakati akipata matibabu katika Hospitali ya Kamanga iliyopo Jijini Mwanza.

“Ni kweli diwani wetu wa Kamena ameondoka kwenye maisha haya ni huzuni kwetu kwa chama na familia kikubwa ni kuendelea kumuombea apumzike salama,”amesema Kazungu.

Diwani wa Bukoli, Faraji Seif amesema wamepata pigo kwao kwa Kulwa aliyekuwa na busara na kiongozi akisiliza wakubwa na wadogo.

“Alikuwa mzee ambaye kwa sisi vijana alikuwa kiongozi mwenye busara akisema jambo hakurupuki kusema tumekosea, alikuwa kiongozi mwenye busara anayesikiliza zaidi kabla ya kusema na alikuwa akitoa ushirikiano na kushauri atakumbukwa sana kwa busara zake,”amesema Seif.

Kuhusu taratibu za mazishi, Seif amesema bado maandalizi yanaendelea kwa ushirikiano wa familia na halmashauri.

Related Posts