Dar es Salaam. Hatua ya Serikali kupendekeza msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mafuta ya kupikia yanayozalishwa nchini, hatua hiyo imetajwa kuongeza hamasa ya uwekezaji katika uzalishaji, kilimo cha mazao ya mafuta na itapunguza bei ya bidhaa hiyo.
Wasindikaji wa ndani wa mafuta wameeleza kwa uhalisia wa uwezo wa viwanda walivyonavyo, wanaweza kukidhi mahitaji ya ndani na hata kuuza nje mafuta ya alizeti.
Kwa mujibu wa Chama Cha Wasindikaji wa Zao la Alizeti Tanzania (Tasupa), kwa sasa kuna viwanda 773 vya usindikaji alizeti vyenye uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.7 za mafuta hayo.
Uwezo wa viwanda vilivyotajwa na Tasupa unazidi mahitaji ya nchi, ambayo kwa mujibu wa taarifa zilizowahi kutolewa na Serikali mwaka 2021 yalikuwa tani 650,000, huku uwezo wa uzalishaji wa ndani ulikuwa tani 290,000.
Pendekezo la msamaha wa VAT katika bidhaa hiyo inayozalishwa nchini, lililotolewa juzi na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipowasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/25 jijini Dodoma.
Dk Mwigulu alisema Serikali inapendekeza msamaha wa VAT kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa ndani ya nchi kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini kwa muda wa mwaka mmoja.
“Lengo la hatua hii ni kuendeleza unafuu wa bei ya mafuta ya kula iliyopanda kutokana na mdororo wa uchumi na vita ya Urusi (Russia) na Ukraine vilivyosababisha uhaba wa mafuta hayo,” alisema.
Tanzania imewahi kupitia vipindi mbalimbali vya kupanda kwa gharama za mafuta ya kupikia na zaidi ilishuhudiwa mwaka 2022.
Katika kipindi hicho, bei ya dumu la lita 20 la mafuta hayo lilifika Sh120,000 hadi Sh130,000 kutoka Sh55,000, huku lita moja iliuzwa kati ya Sh8,000 hadi Sh9,000 kutoka Sh5,500.
Sababu ya hali hiyo, Serikali ilisema ni vita kati ya Russia na Ukraine vilivyosababisha changamoto katika mnyororo wa ugavi wa bidhaa mataifa.
Kwa upande mwingine, wanaoingiza mafuta kutoka nje Serikali imependekeza asilimia 35 au Dola 500 za Marekani kama ushuru wa forodha kwa kila tani moja ya bidhaa hiyo.
Pendekezo hilo ni tofauti na utaratibu uliopo ambapo, waagizaji hao hutozwa ushuru wa forodha wa asilimia 35 kwa kuagiza bidhaa hiyo mwaka mzima.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Tasupa, Ringo Iringo amesema kwa sasa wasindikaji wa ndani wa bidhaa za mafuta wanatozwa asilimia 18 ya VAT.
Kodi hiyo amesema inatozwa pia kwa wanaosafisha mafuta hayo baada ya kuyanunua kutoka kwa wasindikaji yakiwa ghafi.
Msamaha huo kwa mujibu wa Iringo, utapunguza bei ya mafuta yanayozalishwa nchini, kwa kuwa gharama za uzalishaji viwandani zitapungua na kuanzishwa vingine vipya.
“Awali, tulikuwa tunaogopa kuongeza uwekezaji kwenye viwanda kwa sababu kikiwa kikubwa tu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inakufuata na kukutoza VAT ya asilimia 18,” amesema.
Katika mazingira hayo, amesema wawekezaji wengi walihakikisha viwanda vyao vinabaki kuwa vidogo ilimradi visikidhi vigezo vya kutozwa asilimia 18 ya VAT.
Iringo akizungumzia ushuru kwa wanaoingiza mafuta kutoka nje amesema utafungua soko kwa wazalishaji wa ndani.
Kabla ya uamuzi huo, amesema waagizaji wa mafuta yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho kutoka nje, waliuza kwa bei ndogo zaidi, hivyo kufanya wale wa ndani wakose soko.
“Gharama za kuagiza zilikuwa nafuu kuliko kuzalisha ndani. Tulikuwa tunahamasika kuagiza mafuta kuliko kutengeneza mazingira ya kujitosheleza, hiki kilichopendekezwa sasa ni kitu sahihi,” amesema.
Mkurugenzi wa kampuni ya G & B Soap inayozalisha mafuta nchini, Godliving Makundi amesema uzalishaji utaongezeka kutatokana na gharama za uzalishaji kupungua.
“Uwekezaji utaongezeka kwa kuwa wazalishaji watatumia fedha ambazo wangepaswa kulipa kodi hiyo katika kuongeza nguvu za kuzalisha,” amesema.