WANANCHI WAMPA TANO MBUNGE BASHUNGWA KUFANIKISHA UJENZI BARABARA YA BUGENE-KASULO-KUMUNAZI

Na Mathias Canal, Karagwe-Kagera

Wakazi wa Kijiji Cha Nyakahanga wilayani Karagwe Mkoani Kagera wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja.

Wameipongeza Wizara ya Ujenzi Kupitia Wakala ya Barabara Tanzania -TANROADS kwa kuwajengea barabara inayounganisha wilaya ya karagwe na Ngara kupitia hifadhi ya Burigi Chato ya Bugene-Kasulo- Kumunazi (Km 128.5), kipande cha Bugene-Burigi Chato (Km 60).

Mradi huo unatekelezwa kwa miezi 30 na Mkandarasi wa kampuni ya China Road and Bridge Cooperation ya China (CRBC) kwa gharama ya TSh. Bilioni 92.84 ambapo hadi hivi sasa mradi umefikia asilimia 41.9

Regina Berra, Ni Mkazi wa Kijiji Cha Nyakahanga Wilayani Karagwe, ameeleza kuwa awali barabara hiyo ilikuwa katika hali mbaya na kupelekea adha hasa kwa watumiaji wa vyombo vya moto, lakini Kutokana na matengenezo yaliyofanyika chini ya Wakala ya Barabara Tanzania TANROADS barabara hiyo Sasa imeanza kupitika vizuri na wanategemea itakamilika kwa kiwango Cha lami.

“Barabara hii ilikuwa na Hali mbaya,Sasa hivi kwakweli tunaona mabadiliko mazuri na kwa sisi tunao tembea tunajisikia vizuri, kama Mungu akitusaidia barabara hii ikakamilika kama ilivyopangwa kuwekwa lami kwakweli tutatembea vizuri” Amesema Regina

Naye Thabit Hamis, Mkazi wa Kijiji hicho amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mradi huo wa Ujenzi wa Barabara kwani kipindi Cha mvua ilikuwa ni vigumu watu na magari Kupita hali iliyosababisha kupoteza muda mwingi wakiwa barabarani.

“Zamani tulikuwa tunatembea kwa masaa manne lakini baada ya mkandarasi kuanza tu mradi huu, sasa tunatembea kwa masaa mawili na hapo bado haijakamilika na kuwekwa lami” Amesema Thabit

Sambamba na hilo Mzee Protus Kasimbazi pamoja na Nelson Kasenene wamemshukuru Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe Innocent Bashungwa kwa kufanikisha utatuzi wa kadhia hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.

Nelson ameeleza awali Miundombinu ya barabara haikuwa katika hali nzuri ukizingatia yeye ni Afisa usafirishaji maarufu (bodaboda) anasema ilikuwa ikimuwia vigumu katika biashara yake hususani kwa abiria kwa sababu ya umbali mrefu ukiambatana na vumbi jingi barabarani hivyo kupelekea kukosa kipato inavyotakiwa lakini kwa Sasa barabara inapitika vizuri na kipato chao kwa Sasa kimeongezeka.

Related Posts