Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na viongozi wa Ujerumani, Italia, Uingereza, Canada na Japan ni miongoni mwa watakaohudhuria mkutano huo wa kilele wa siku mbili utakaofanyika kwenye eneo la mapumziko lenye milima la Buergenstock nchini Uswisi.
India, ambayo iliisaidia Moscow kukabiliana na vikwazo vya uchumi vilivyowekwa na mataifa ya Magharibi, inatarajiwa pia kutuma ujumbe kwenye mkutano huo, huku Uturuki na Hungary, ambazo zimedumisha mahusiano na Urusi licha ya vita vyake nchini Ukraine, zitakilishwa na mawaziri wao wa mambo ya nje.
Serikali mjini Ankara imesisitiza kuwa ili kupata matokeo chanya katika mjadala wa kutafuta namna ya kuvimaliza vita nchini Ukraine, ni vyema kuandaa mkutano utawaowajumuisha wahusika wote katika mzozo huo mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa barani Ulaya tangu kumalizika kwa Vita Vikuu Vya Pili Vya Dunia.
Soma pia: Zelensky aishukuru Ufilipino kuelekea mkutano wa amani
Licha ya miezi kadhaa ya harakati za ushawishi wa Ukraine na Uswisi, mataifa mengine kama China ambayo ni mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Urusi hayatoshiriki mkutano huo utakayo yakutanisha takriban mataifa 90 na mashirika kadhaa.
Rais Zelenskiy amesema hapo jana akiwa mjini Berlin kuwa kitendo cha kuandaa mkutano huo tayari ni matokeo ya kuridhisha lakini akaafiki kuwepo kwa changamoto ya kudumisha msaada wa kimataifa wakati vita vikiingia sasa katika mwaka wake wa tatu. Urusi imeutaja mkutano huo kuwa ni “upuuzi” mtupu kwa kuwa haikualikwa.
Changamoto katika uandaaji wa mkutano huo
Wanadiplomasia wanaofuatilia kwa karibu tukio hilo wanasema waandaaji wa mkutano huo wamejitahidi kuweka usawa kati ya kulaani vitendo vya Urusi na kupata washiriki wengi zaidi. Rasimu ya mwisho ya tamko la mkutano huo itazingatia bila shaka vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, na pia kuheshimishwa kwa maazimio na sheria za kimataifa.
Soma pia: Zelenskiy awataka viongozi wa dunia kumuunga mkono
Washiriki ambao hawatokubaliana na tamko hilo watakuwa na uwezo wa kujiondoa. Wizara ya mambo ya nje ya Uswisi haikuzungumzia chochote kuhusu hilo lakini ikasisitiza kuwa lengo la mkutano huo ni kuandaa mazingira ya kufanyika “mchakato wa amani katika siku zijazo” ambao utaishirikisha pia Urusi na pia kuamua ni nchi gani inayoweza kuwa mwenyeji wa mkutano kama huo.
Wanadiplomasia kadhaa wamesema Saudi Arabia ni miongoni mwa mataifa yanayopendekezwa huko Mashariki ya Kati ili kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa amani. Siku ya Jumatano, Zelensky alifanya ziara nchini Saudi Arabia kujadiliana suala hilo na Mwanamfalme Mohammed bin Salman.
Mkutano huo utafikia malengo yake?
Awali, wazo la mkutano huu wa kilele lilikuja baada ya Zelenskiy kuwasilisha mwishoni mwa mwaka 2022, mpango wa amani wenye vipengele 10, lakini vitakavyozingatiwa zaidi katika mkutano huo ni pamoja na hitaji la dhamana ya usalama wa chakula, usalama wa miundombinu ya nyuklia, uhuru wa safari za baharini, masuala ya kubadilishana wafungwa na kurejeshwa kwa watoto wa Ukraine waliopelekwa Urusi.
Soma pia: Zelensky akerwa na viongozi kutohudhuria mkutano wa Uswisi
Mtaalam wa siasa za Ulaya Mashariki katika chuo cha St Gallen nchini Uswisi Ulrich Schmid, anasema hadi sasa mkutano huo umekosa mwelekeo kutokana na baadhi ya washiriki kuwa na ukaribu na Moscow lakini pia kutohudhuriwa na China.
Schmid anahoji ikiwa katika mazingira hayo, amani ya kweli inawezekana na kuongeza kwamba ikiwa rais wa Urusi Vladimir Putin atasalia kuwa madarakani, basi itakuwa vigumu kufikia azma hiyo.
Jana Ijumaa Putin alisema Urusi itasitisha mara moja mapigano na kuanzisha mazungumzo ya amani ikiwa Ukraine itaachana na malengo yake ya kujiunga na Jumuiya ya kujihami ya NATO na kuondoa wanajeshi wake katika mikoa minne ya Ukraine iliyonyakuliwa na Urusi. Lakini Kyiv imekuwa mara kadhaa ikisisitiza kuwa suala la uhuru wa mipaka yake kamwe haliwezi kujadiliwa.
(Vyanzo: RTRE,APE)