Kesho itajulikana ni nani atacheza Ligi Kuu Bara msimu ujao kati ya Biashara United ya Mara na Tabora United, ambazo zitamenyana katika mchezo wa marudiano kuwania kucheza ligi hiyo, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora kuanzia saa 10:00 jioni.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Karume, Musoma, wenyeji Biashara United walishinda kwa bao 1-0 la mkwaju wa penalti lililofungwa na Herbert Lukindo dakika ya 99.
Kocha wa Biashara United, Amani Josiah, alisema baada ya kuwa na mtaji wa bao 1-0, jambo la msingi watakalolifanyia kazi ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake kujiamini na kujiandaa vyema ili kucheza bila hofu na ikiwezekana washinde ugenini.
Alisema mechi hiyo haijaisha watawatengeneza wachezaji kichwani namna ya kuukabili mchezo huo na kutumia ubora wa eneo la ushambuliaji kupata bao la ugenini na kujilinda vizuri ili kupata matokeo yatakayowapeleka Ligi Kuu.
“Jambo la kwanza kabisa kwenye mechi inayofuata inabidi tuongee na wachezaji sana kuhusu suala la saikolojia, Tabora United wataweka nguvu kubwa nyumbani. Tunahitaji kujilinda vizuri na kusaka bao la ugenini ikiwezekana sisi ndiyo tutangulie,” alisema Josiah
“Tulipata ugumu ambao tuliutegemea kwa sababu tunacheza na timu ya Ligi Kuu lakini tulikuwa bora ndani ya dakika 90 tumetengeneza nafasi na kuikamata mechi. Nilifurahishwa na kiwango cha vijana wangu kwa sababu huenda mechi kama hii wangekuwa na presha kubwa,”
Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala, aliseam kalbu yao imekuwa na mwendelezo wa matokeo yanayowaumiza mashabiki lakini akawataka kuwa wavumilivu na kuungana ili kushinda mchezo huo na kuibakiza timu Ligi Kuu.
“Mashabiki wetu tunawaambia bado haijaisha tuna dakika 90 za nyumbani ambazo tunapaswa kuzitumia vizuri ili timu yetu isishuke. Tuangalie cha kufanya kwenye uwanja wetu wa nyumbani tutetee timu yetu ibaki Ligi Kuu,” alisema Mwagala.