Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa nchi hiyo kuanza muhula wa pili madarakani. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Uchaguzi huo wa rais umekuja baada chama cha Ramaphosa cha African National Congress, ANC, kuingia makubaliano na vyama vingine kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Ramaphosa amechaguliwa kwa wingi mkubwa wa kura katika kikao cha kwanza cha bunge jipya la nchi hilo kilichofanyika jana Ijumaa mjini Cape Town ikiwa ni wiki mbili zimepita baada ya kufanyika uchaguzi.
Amepata kura 283 dhidi ya mwanasiasa machachari Julius Malema anayeongoza chama cha mrengo mkali wa kushoto cha Economic Freedom Fighters aliyeambulia kura 44.
Ramaphosa mwenye umri wa miaka 71 amepata ushindi huo kwa kuungwa mkono na chama cha pili kwa ukubwa nchini humo cha Democratic Alliance na vyama vingine vidogo.
Vyama hivyo vilifikia makubaliano ya kuunda seriali ya pamoja na ANC kufuatia chama hicho tawala kukosa wingi wa viti bungeni katika uchaguzi uliofanyika tarehe 29 Mei mwaka huu.