ZAIDI ya vijana 12,000 kutoka Wilaya ya Songwe mkoani Songwe wamepata fursa ya ajira katika migodi ya wachimbaji wadogo na wa kati baada ya Serikali kugawa vitalu 19 kwa wachimbaji hao ili kuhochea ukuaji wa uchumi pamoja na kupunguza migogoro na uhalifu katika jamii ya wachimbaji. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).
Akizungumza na MwanaHALISI Online leo Jumamosi Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo mkoa wa kimadini Songwe, Emmanuel Kamaka amesema upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji ilikuwa ni changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili.
Amesema baada ya Serikali kusikia kilio chao, hivi karibuni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alifika mkoani humo na kuwagawia vitalu 19 kati ya 35 walivyoomba.
Naye Emmanuel Jimmy ambaye ni mchimbaji mdogo amesema ameishukuru Serikali kwa kuwapatia vitalu hivyo hasa ikizingatiwa wachimbaji wadogo wanachangia zaidi ya asilimia 50 ya pato la taifa kupitia sekta ya madini.
Afisa madini mkazi mkoani Songwe, Lugangiza Malembo amesema upatikanaji wa vitalu hivyo 19 umeongeza chachu ya kujituma kwa wachimbaji wadogo ambao kwa sasa watakopesheka kwa kuwa wamepatiwa leseni.
Mkuu wa wilaya ya Songwe, Solomon Itunda amesema serikali imesikia kilio chao cha muda mrefu hivyo wachimbaji hao vijana watajikita kuchimba na kujiingizia kipato hali itakayowaondoa katika vitendo vya uhalifu.