Muleba. Familia ya Baraka Lucas aliyekutwa amekufa, mwili ukielea juu ya maji katika Ziwa Victoria, imegoma kuuzika ikitaka Jeshi la Polisi kueleza chanzo cha kifo chake.
Lucas (20), mwili wake umekutwa ziwani katika Kisiwa cha Goziba wilayani Muleba, mkoani Kagera.
Kijana huyo aliyekuwa akifanya kazi ya kubeba dagaa wabichi katika mwalo kisiwani hapo, mwili wake ulikutwa ziwani Juni 12, 2024.
Taarifa zinasema Lucas alikamatwa akiwa baa na mwenzake aliyekuwa akiishi naye aliyetajwa kwa jina moja la Yoro Juni 9, 2024 saa 7.30 usiku wakati askari kutoka Kituo cha Polisi Goziba wakifanya doria.
Mkazi wa Goziba, Peter Samwel (28), ambaye ni jirani wa Lucas alisema Juni 10, 2024 alipata taarifa kutoka kwa Yoro kuwa wasimtafute Lucas kwa kuwa alikamatwa na polisi waliokuwa doria.
Yoro ameeleza kwamba aliwakimbia askari waliobaki na Lucas.
“Yoro, kijana wa Kigoma ambaye walikuwa wakiishi chumba kimoja aliniambia walikamatwa saa saba usiku wakiwa kwenye baa, walipokaribia kituo cha polisi aliwakimbia mwenzake akabaki na alipigwa na askari,” amedai.
Samwel amedai walikwenda kituo cha polisi Jumanne jioni kumjulia hali na kumpelekea chakula lakini walipofika kituoni walijibiwa vibaya na askari waliokuwa hapo.
Amedai walipohoji waliambiwa mtu wanayemtafuta amedhaminiwa, hayupo kituoni hapo.
“Tulijibiwa vibaya, tukajiuliza kwa nini wanatujibu vibaya na kama amedhaminiwa kina nani wamemdhamini? Tukarudi nyumbani, Jumatano kukawa na taarifa kuna mtu ameopolewa majini, tulipofika tukakuta ni yeye na madaktari wakafika na kuanza kumpima,” alisema.
Amesema baadaye walikwenda kituo cha polisi kuandikisha maelezo walipomaliza ofisa mmoja kituoni hapo (jina linahifadhiwa kwa sasa) akaamuru mwili ukazikwe ila wananchi wakakataa kwa kuwa hapakuwa ndugu yake hata mmoja.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ishenye, Kata Goziba, Justine Mgeta amesema alipokea taarifa baada ya kupigiwa simu na kuelezwa kuna mwili umeonekana mwaloni pembezoni mwa Ziwa Victoria ukielea.
Amesema alikwenda eneo la tukio na kukuta wananchi wamejaa, akampigia simu Mkuu wa Kituo cha Polisi Goziba kumjulisha na alimjibu asubiri awasiliane na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Goziba ili aambatane naye kwenda eneo la tukio.
“Nilitafuta mtumbwi na kamba tukafika eneo mwili ulipoonekana ukielea ziwani tukauchukua hadi nchi kavu. Tukwasiliana na mkuu wa kituo cha polisi na Mganga Mkuu Mfawidhi wa Zahanati ya Goziba kuwa tayari tumeshautoa mwili majini njoo muendelee na uchunguzi,” amesema.
Amesema baada ya dakika 40 alifika mwanamke akautambua mwili kuwa wa Baraka Lucas, mkazi wa kisiwani hapo akieleza alikuwa akisomba dagaa wabichi.
Baada ya mkuu wa kituo kuwataka wananchi wakazike mwili, Juni 13 wananchi walifika kituo cha polisi wakipinga kuzika, hivyo askari waliwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi.
Hatua hiyo ilizua vurugu zilizozimwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Muleba aliyefika kisiwani hapo na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi.
Hata hicyo aliwaambia wananchi kwamba askari waliohusika watachukuliwa hatua na waliokamatwa kwenye doria kuachiwa huru.
Mwananchi aliyekuwa amekamatwa na baadaye kuachiwa huru (jina linahifadhiwa) amedai Lucas alifikishwa kituoni akiwa na majeraha kutokana na kipigo.
“Alikuwa na damu nyingi akionekana kapigwa, tulipomuuliza alisema amepigwa na askari. Aliomba maji ya kunywa, baadaye polisi na mgambo walimpeleka Zahanati ya Goziba. Mgambo baadaye akatuambia ameambiwa arudi,” amedai.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Bukoba, Dk Sophia Mosha alithibitisha mwili wa Lucas umeifadhiwa katika hospitali hiyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Daniel Yusuph alisema taarifa kuhusu tukio hilo ziliwafikia Juni 12, 2024 saa saba mchana.
Amesema mwili wa marehemu baada ya kuopolewa na kufanyiwa uchunguzi na wataalamu kutoka Zahanati ya Goziba, kama ilivyo kawaida baada ya uchunguzi kukamiliaka Jeshi liliamuru mwili kuzikwa.
Hata hivyo, amesema ndugu walikataa kupokea mwili na kuanzisha vurugu.
Katika kuwatuliza amesema walitumia mabomu ya machozi.
“Ndugu walikataa mwili wa marehemu na kuanzisha vurugu, Jeshi likalazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya,” alisema.
Kaimu Kamanda Yusuph amesisitiza jeshi halitasita kuwachukulia hatua hata kama ni watumishi wake iwapo waliohusika na kifo cha Lucas.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Goziba, Msafiri Ngwesa alisema Yoro aliyeshuhudia kuhusu Lucas akikamatwa na kupigwa na polisi amepotea na wamemtafuta kila mahali hajapatikana.
Mkazi wa eneo hilo (jina limehifadhiwa) amesema Yoro aliyekuwa akiishi chumba kimoja na Lucas tangu siku walipokamatwa hajaonekana tena.
Paschal Ibrahim (29), baba mdogo wa Lucas akizungumza na Mwananchi Juni 14, amesema mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa jioni ya Juni 9, 2024.
Amesema alipata taarifa kuwa kijana wake amekamatwa na maofisa wa polisi.
Ibrahim amesema Juni 11 alifika kituoni yeye na wenzake kumpelekea chakula ambako walimkuta askari wa kike wa Jeshi la Akiba (mgambo) waliyemuomba wazungumze na ndugu yao.
Amesema mgambo alifungua mlango wa kwanza na wa pili, Lucas hakuonekana akawaambia huenda amedhaminiwa.
Amedai walilazimishwa kumzika ndugu yao baada ya kubainika kuwa alifariki dunia,alipokataa ndipo vurugu zikaanza.
“Nililazimishwa kuzika mwili wa mwanangu ila sikuwa tayari kwa sababu polisi wanatakiwa kusema ilikuwaje aliyekuwa mahabusu akutwe ziwani akiwa amekufa? Hata kama Serikali itasema kuwa azikwe mimi siko tayari na familia haiko tayari, tunataka aliyehusika ndio ashughulike na msiba huo,” alisema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Goziba, Msafiri Ngwesa amedai licha ya Kituo cha Polisi Goziba kujengwa kwa fedha za wananchi zitokanazo na mapato ya ndani kisiwani hapo, maofisa wa kituo hicho wamekuwa wakiwatishia kuwaua wanaposhindwa kulipa Sh200,000 wakihusishwa na kosa lolote kisha kuwekwa mahabusu kwa wiki mbili bila kudhaminiwa.
“Tumeshalalamika sana Serikali iwahamishe kutokana na vitendo ambavyo ni vya uvunjifu wa amani, wametunyanyasa,” amedai Kichele Warioba, mjumbe wa Serikali ya Kijiji Goziba.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Yusuph akizungumzia malalamiko hayo amesema: “Ukweli sina taarifa kamili kuhusu hayo, tunashukuru kwa kutujulisha ngoja tufuatilie zaidi.”