Maxime amvuta Nizar Dodoma Jiji

BAADA ya Dodoma Jiji kufikia makubaliano na aliyekuwa Kocha wa Singida Black Stars, Mecky Maxime ili kuinoa timu hiyo msimu ujao, tayari amependekeza jina la Nizar Khalifan ili akawe msaidizi wake ndani ya kikosi hicho cha walima Zabibu.

Mwanaspoti linatambua licha ya Maxime kutotangazwa hadi sasa ila tayari amesaini mkataba wa miaka miwili huku akiwa anasubiria utambulisho rasmi baada ya kuachana na Singida iliyomwajiri kocha wa zamani wa Simba, Patrick Aussems.

Mmoja wa viongozi wa timu hiyo aliliambia Mwanaspoti, baada ya kumalizana na Maxime kwa sasa mazungumzo yamehamia kwa Nizar.

“Maxime amempendekeza Nizar ili akawe msaidizi wake ingawa bado mazungumzo yanaendelea kwa sababu sio suala la haraka na isitoshe muda wa kufanya maamuzi bado upo, wakati utakapofika tutaweka wazi,” alisema mmoja wa kiongozi wa kikosi hicho.

Wakati hayo yakiendelea ila bado uongozi wa Dodoma Jiji hauhitaji kumpoteza kirahisi kocha msaidizi wa timu hiyo, Kassim Liogope kutokana na uhusiano mzuri aliokuwa nao kuanzia kwa viongozi na wachezaji kijumla licha ya mapendekezo hayo ya Maxime.

Kwa upande wa Nizar alipotafutwa na Mwanaspoti kuhusu taarifa hizo alisema, kwa sasa yupo mapumziko ingawa muda sio mrefu mashabiki zake watafahamu atakapokwenda, kwani nia yake kubwa ni kuendelea kutumikia mpira wa miguu nchini.

Nizar aliyewahi kucheza klabu mbalimbali zikiwemo, Yanga, Mtibwa Sugar, Singida United, Mwadui, Vancouver Whitecaps ya Canada na Philadelphia Union ya Marekani, kwa sasa yupo huru baada ya msimu uliopita kuachana na Singida Fountain Gate.

Related Posts