Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imechukizwa na kitendo cha mtu anayehusika kutoa namba ya malipo (control number) kwa ajili ya mshtakiwa Dilipkumar Maganbai Patel, kulipa faini kuchukua mwezi mzima kutoa namba hiyo.
Patel anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 58/2016 yenye mashtaka mawili likiwamo la kusafirisha vipande 17 vya kucha za simba zenye thamani ya Sh53 milioni, bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.
Hayo yamebainika jana, Juni 14, 2024 baada ya Wakili wa Serikali, Titus Aaron kuieleza Mahakama hiyo kuwa wanasubiri namba ya kwa ajili ya mshtakiwa kufanya malipo ili waendelee na hatua nyingine ikiwamo mshtakiwa huyo kusaini mkataba waliofikia katika vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.
Patel alimuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) mwanzoni mwa mwaka huu, akiomba kukiri mashtaka yake na kuomba apunguziwe adhabu.
Hata hivyo, baada ya kuandika barua hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Amiri Msumi anayesikiliza shauri hilo, alitoa siku 30 kwa mshtakiwa huyo kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo (plea bargaining) na DPP ya kuimaliza kesi hiyo.
Baada ya kupewa muda huo, upande wa mashtaka ulianza vikao na mshtakiwa huyo na kufikia makubalinao ya kulipa faini.
“Kesi hii ipo katika vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi hii na tumeshawalisha kwa mamlaka husika majumuisho ya kikao na sasa tunasubiri kupewa namba ya malipo kwa ajili ya mshtakiwa kufanya malipo kama tulivyokubaliana katika majadiliano yetu na yeye ili tuendelee na hatua nyingine ambayo ni kusaini mkataba wake,” amedai Wakili Aaron.
Kwa kawaida mshtakiwa anapofanya majadiliano ya kuimaliza kesi yake, huwa kuna kipengele kinamuelekeza kulipa nusu ya fedha walizokubaliana katika majadiliano hayo kabla ya kutolewa adhabu na Mahakama hiyo.
Wakili Aaron baada ya kueleza hayo, mshtakiwa huyo aliomba kupewa nafasi ya kuzungumza.
Mahakama ilipompa nafasi, Patel amesema kesi yake ni ya muda mrefu na tayari ndugu zake wameshachangishana ili aweze kulipa faini hiyo lakini haelewi nini kinakwamisha.
Patel, alisema ndugu zake wamemwambia kama hatoki gerezani basi arudishe fedha walizomchangia.
“Mimi sina pesa wala baba yangu hana pesa, ni ndugu zangu tu ndio wamechangishana na kupata fedha za kunisaidia kulipa faini ili niweze kutoka, sasa wameniambia kama sitoki garezani basi nirudishe fedha zao.
“Naona hawaonyeshi dalili za kunipa hiyo namba, hivyo suala hili naiachia Mahakama. Hivyo naomba tarehe nyingine ili nije tena mahakamani,” amesema.
Patel baada ya kutoa malalamiko hayo, Hakimu Msumi amehoji upande wa mshtaka kitu gani kinachokwamisha utaoji wa namba hiyo.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Aaron amedai alishapeleka suala hilo kwa mamlaka husika kwa ajili ya kutoa namba.
Hakimu Msumi amesema anajizuia kusema vitu visivyofaa.
“Yaani hapa tunasubiri tu control number tu? Namrudisha ndani tena huyu mshtakiwa kwa sababu tu mtu anayetakiwa kutoa namba ameamua kukaa tu?
“Sisi sote tuvae viatu vya huyu mtu, ndugu zake kama alivyosema wamechangishana na wapo tayari kulipa na kiasi gani cha kulipa kinajulikana, halafu mtu mmoja anaweza kutushikilia sisi mpaka atakapoamua?” amehoji.
Hakimu amesema kwa bahati mbaya kesi hii ya Dilipkumar ni miongoni mwa kesi za muda mrefu zinazotakiwa kuisha kwa haraka.
“Na kesi hii ilishawahi kwenda hadi Mahakama ya Rufaa na ikarudishwa hapa Kisutu, yaani kutoa control number imefikisha mwezi sasa, kweli! Tuendelee kusubiri mpaka lini?
“Natamani ningekuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi ningefanya, lakini siwezi, pia ningekuwa naweza kutoa hiyo control number ningakupa,” amesema hakimu Msumi.
Hakimu Msumi amesema kuwa, hata yeye anaulizwa na wakubwa zake kwa nini kesi hiyo haiondoki?
“Kesi hii ina siku zaidi ya 3,000 tangu mshtakiwa huyu ashtakiwe mahakamani na sasa kesi hii inachelewa kutolewa uamuzi kwa sababu ya mtu mmoja,” amesema.
Amesema kutokana na hali hiyo kuna kitu kinatakiwa kifanyike nje ya Mahakama japo kuwa watakuja kulaumiana.
“Mimi sitaki kukalia haki ya mtu, hapa kuna kitu tunatakiwa kufanya nje ya Mahakama, japokuwa tutakuja kulaumiana, tutachukua na mawasiliano ya huyu mkubwa.
“Vinginevyo ninyanyuke hapa katika hiki kiti nilichokalia, kama tu mtu mmoja hataki kutoa control number, halafu mtu huyo yupo katika ofisi ya umma?” amehoji.
“Hivi tunajua kesho tunaamkaje? Kwa watu hasa wenye mamlaka?
“Hapa huyu mshtajiwa na leo namrudisha rumande kwa sababu eti kuna mtu mmoja tu, amekalia tu na hataki kutoa control number,” amesema hakimu Msumi na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 20, 2024.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kukutwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria na kujihusisha na biashara ya wanyamapori bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shtaka la kwanza, ambalo ni kukutwa na nyara za Serikali, mshtakiwa anadaiwa Novemba 19, 2016 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) ulipo jiji Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na vipande 17 vya kucha za simba zenye thamani ya zaidi ya Sh53.48 milioni bila kuwa na kibali au leseni
Shtaka la pili ni kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali, mshtakiwa Sanjiv Patel na Ashok Kumar kati ya Novemba 14 na Novemba 15, 2016 Wilaya ya Bunda iliyopo Mkoa wa Mara.
Inadaiwa siku hizo, kinyume cha sheria washtakiwa hao alihamisha vipande 17 vya kucha za Simba kwenda kwa Dilipkumar Patel, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali.
Kwa mara ya kwanza mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo, Novemba 28, 2016 akikabiliwa na mashtaka hayo.