Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala Ndogo ya Morogoro, imewahukumu kifungo cha maisha jela watuhumiwa wawili baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.
Hukumu hizo zilitolewa Juni 13, 2024 na Jaji Sedekia Kisanya katika kesi mbili tofauti kesi ya kwanza, Mahakama hiyo imemhukumu kifungo hicho Musa Kipemba, aliyekutwa akisafirisha mifuko 81 iliyokuwa na bangi kilo 1,591.55.
Mwingine ni Banzi Ramadham ambaye Julai 26, 2023 eneo la Rhumba mkoani Morogoro alikutwa akisafirisha bangi kilo 213. 05.
Watuhumiwa hao walidaiwa kutenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 15(1) (a) na (3) (iii) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 kama ilivyofanyiwa marejeo 2019 na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Kifungu hicho kilisomwa pamoja na aya ya 23 ya jedwali la kwanza la sheria na vifungu vya 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Kuratibu, Sura ya 200 (EOCCA).
Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023, iliyokuwa ikimkabili Musa, alidaiwa Desemba 6, 2020 katika, Barabara ya Morogoro – Dar es Salaam, alikutwa akisafirisha mifuko 81 iliyokuwa na kilo 1,591.55 za bangi.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikamatwa mwaka mmoja na nusu baada ya kufanya kosa hilo, Juni 2, 2022, katika ofisi za uhamiaji, Kurasini, Dar es Salaam alikokuwa ameomba hati ya kusafiria.
Katika kesi hiyo, Jamhuri ilikuwa na mashahidi 10 na vielelezo 12, ikiwamo mikataba miwili ya ajira kati ya Soud Industries Limited na Musa.
Ilidaiwa kuwa siku ya tukio, askari wa usalama barabarani, wakiendelea na ukaguzi katika eneo la seminari ndogo, walipata taarifa ya siri kuwa gari lenye namba T486 DSU, likiwa na trela lililosajiliwa kwa namba T275 BXB, lilikuwa na bangi.
Ilidaiwa mahakamani kuwa baada ya gari lililofanana na maelezo hayo likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam, kukaribia eneo hilo lilisimamishwa kwa ajili ya ukaguzi.
Wakati ukaguzi ukiendelea, ilidaiwa mtuhumiwa aliomba kwenda kujisaidia katika kichaka cha jirani lakini akatoweka na kutelekeza gari eneo la tukio katika treka la gari hilo alilokuwa amebeba majani katika magunia.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa sampuli za majani hayo zilichukuliwa hadi kwa mkemia kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) mjini Dodoma na vipimo vilionyesha ilikuwa ni bangi.
Wakati huohuo, mmiliki wa gari hilo, Kampuni ya Soud Industries Limited, kupitia kwa ofisa wao aliyetoa ushahidi mahakamani hapo, alikuwa akifuatilia magari yote kwa kutumia mfumo wa Utrack Africa.
Alidai baada ya kuona gari hilo limesimama kwa muda mrefu Kituo cha Polisi Morogoro, walitoa taarifa kwa uongozi wa kampuni hiyo uliotuma madereva waliokuwa karibu nao ambao baadaye walithibitisha kukamatwa kwa gari hilo na polisi.
Baada ya kuwasilisha nyaraka kampuni ilibainika hawahusiki na bangi hiyo.
Kampuni hiyo ilirejeshewa gari na trela hilo kwa masharti ya kutofanya safari za nje ya nchi na kubadilisha mwonekano wake.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama iliridhisha kuwa upande wa Jamhuri ulithibitisha kosa hilo dhidi ya mshitakiwa pasipo kuacha shaka na kumhukumu kifungo cha maisha jela hasa baada ya kukutwa akisafirisha kiasi kikubwa cha dawa hizo za kulevya.
“Kwa kuzingatia zaidi kiwango kikubwa cha bangi iliyohusika katika kesi hii (kilo 1591.55), Mahakama inaona inafaa kutoa adhabu ya juu kama ilivyowekwa na sheria. Hukumu hii inalenga kuwazuia wengine na kusisitiza uzito wa makosa ya dawa za kulevya,” ameeleza Jaji
Mahakama iliagiza kwamba kwa kuwa hakuna dalili ya wamiliki wa gari na trela kuhusika katika kutenda uhalifu, inaamriwa gari hilo lenye namba za usajili T 486 DSU na trela lenye namba za usajili T275 BXB kurejeshwa kwa wamiliki wao halali.
Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 14560/2024, Banzi alikuwa anadaiwa kusafirisha kilo 213.05 za bangi.
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na jopo la mawakili watano wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Monica Matu na katika kuthibitisha kosa hilo walikuwa na mashahidi sita na vielelezo vinane.
Ilidaiwa siku ya tukio, usiku wa kuamkia Julai 26, 2023, maofisa kutoka DCEA walikuwa wakiendesha operesheni maalumu ya dawa za kulevya eneo la Kisaki mkoani Morogoro.
Ilidaiwa kuwa wakiwa kwenye magari ya doria, walipokea taarifa kutoka kwa mtoa taarifa aliyejifanya mnunuzi wa dawa za kulevya kuwa kuna biashara ya bangi ilipangwa kufanywa katika Kijiji cha Rhumba Chini.
Baada ya kupata taarifa hizo, waliweka mtego katika eneo hilo lenye misitu lisilo na makazi ya watu na lisiloweza kufikiwa na gari na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa amekaa juu ya mifuko yenye majani hayo na baada ya uchunguzi wa kimaabara yalithibitika kuwa ni bangi.
Akijitetea chini ya kiapo, Banzi alidai anaishi Kijiji cha Mkokolo, Kata ya Singisa, Morogoro, alianza kwa kukanusha kosa lililokuwa likimkabili na kudai usiku wa kuamkia Julai 25, 2023 akiwa amelala, aligongewa na watu watatu waliomkamata na kupeleka Kituo cha Polisi Morogoro.
Alidai kutojua kabisa kuhusu magunia saba ya bangi yanayodaiwa kupatikana katika milki yake na kuwa hana hatia, hivyo aliiomba Mahakama imuondolee kosa aliloshitakiwa nalo.
Aidha, upande wa utetezi ulidai kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulikuwa na dosari kubwa, hivyo kushindwa kuthibitisha kesi hiyo pasipo shaka.
Katika kufikia uamuzi wake, Mahakama itazingatia kwa kina hoja zinazotolewa na pande zote mbili huku ikianza na kanuni ya msingi ya kisheria katika kesi za jinai.
Hukumu hiyo iliangalia masuala muhimu iwapo mtuhumiwa alisafirisha kilo 213.05 za bangi na kunaswa kwa dawa za kulevya kama kulizingatia kanuni za kisheria, iwapo mshtakiwa ameibua shaka yoyote kuhusu kesi ya mwendesha mashtaka.
Jaji alieleza kuwa, kupitia ushahidi wa shahidi wa pili na sita, kupitia kwa mtoa taarifa, mtuhumiwa alikamatwa eneo la Rhumba Chini akiwa amekaa juu ya mifuko saba iliyokuwa na bangi, akisubiri kumuuzia mtoa taarifa na kupitia hati ya ukamataji aliyosaini mtuhumiwa kwa dole gumba.
Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Mahakama iliona upande wa mashtaka umethibitisha, upekuzi na ukamataji ulifanyika kwa mujibu wa sheria na umetoa mashahidi wa kuaminika na vielelezo, vimethibitisha shitaka dhidi ya mshitakiwa bila kuacha mashaka yoyote.
Mahakama hiyo ilimtia hatiani Banzi kwa kusafirisha dawa za kulevya na kumhukumu kifungo cha maisha jela.