Mahujjaji wakusanyika Arafat katika kilele cha Hajji – DW – 15.06.2024

Ibada katika viwanja vya Mlima Arafat, unaojulikana kama kilima cha rehema, inachukuliwa kuwa kilele cha Hija. Mara nyingi ni jambo la kukumbukwa zaidi kwa mahujaji, wanaosimama bega kwa bega, miguu kwa miguu, wakimwomba Mungu rehema, baraka, mafanikio na afya njema. Mlima huo uko karibu kilomita 20 (maili 12) kusini-mashariki mwa Makka.

Maelfu ya mahujaji walitembea kwenda mlimani hapo katika giza la alfajiri. Kwenye miteremko ya kilima hicho cha miamba na eneo jirani, wengi waliinua mikono yao katika ibada huku machozi yakiwatoka.

“Kwa hakika ni jambo kubwa. Ni siku bora zaidi kwa Waislamu katika mwaka huu, na hisia bora zaidi ambayo mtu yeyote anaweza kupata,” alisema Hussein Mohammed, hujjaji kutoka Misri, alipokuwa akisimama kwenye miteremko ya mawe alfajiri. “Ni mahali pazuri zaidi kwa mtu yeyote anayetarajia kuwa (hapa) siku hii na wakati huu.”

Inaaminika Mtume Muhammad SAW alitoa hotuba yake ya mwisho, inayojulikana kama Hotuba ya kuaga katika mlima huo mtakatifu miaka 1,435 iliyopita. Katika khutba hiyo, mtume alitoa wito wa kuwepo usawa na umoja miongoni mwa Waislamu.

Saudi Arabia Makka| Ibaada ya Hajji
Kisimamo cha Arafat ni ukumbusho kwa Waislamu juu ya Siku ya Kiyama, watakaposimamishwa mbele ya Mola kujibu yale waliyoyatenda katika maisha yao ya duniani.Picha: Mohamed Abd El Ghany/REUTERS

Soma pia: Waislamu milioni 1 wahudhuria ibaada ya Hajji Mecca

Ali Osman, hujjaji Mhispania, alizidiwa wakati akishuka chini ya kilima cha rehema. Alisema alihisi kwamba alipata nguvu za kiroho na kimwili kwenye eneo hilo takatifu. “Mahali hapa, asante Mungu, (panatoa) nguvu nzuri sana,” alisema. “Nimekuja hapa, namshukuru Mungu. Ni mara yangu ya kwanza. Natumaini kuja tena siku zijazo.”

Mmoja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani

Hajj ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani. Ibaada hiyo ilianza rasmi Ijumaa wakati mahujaji walipoondoka kutoka Msikiti Mkuu wa Makka hadi Mina, uwanda wa jangwa nje kidogo ya jiji hilo. Mamlaka nchini Saudia zinatarajia idadi ya mahujaji mwaka huu kuzidi milioni 2, ikikaribia viwango vya kabla ya janga la UVIKO-19.

Hijja ni moja ya Nguzo Tano za Uislamu. Waislamu wote wanatakiwa kufanya ibada hiyo ya siku tano angalau mara moja katika maisha yao ikiwa wana uwezo wa kimwili na wa kifedha.

Ibada hiyo kwa kiasi kikubwa ni ukumbusho wa simulizi za Quran kuhusu Nabii Ibrahim, mtoto wake Nabii Ismail na mama yake Ismail Hajar, au Abraham na Ishmael kama wanavyotajwa kwenye Biblia.

Makka Saudi Arabia| Ibaada ya Hajji
Katika viwanja vya Arafat, mahujjaji hushinda siku nzima wakiomba msamaha Mwenyezi Mungu na kuwasilisha matatizo kwake.Picha: Amr Nabil/AP Photo/picture alliance

Hijja ya mwaka huu imefanyika chini ya kiwingu cha vita kali katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na Hamas, ambavyo vimesukuma kanda ya Mashariki ya Kati kwenye ukingo wa vita vya kikanda kati ya Israel na washirika wake kwa upande mmoja na makundi ya wapiganaji yanayoungwa mkono na Iran kwa upande mwingine.

Soma pia:Ibada ya Hijjah yaanza leo Ijumaa huko Makkah 

Wapalestina katika Ukanda wa pwani wa Gaza hawakuweza kwenda Makka kwa ajili ya Hijja mwaka huu kwa sababu ya kufungwa kwa kivuko cha Rafah mwezi Mei, wakati Israel ikiendeleza mashambulizi yake ya ardhini hadi kwenye mji wa kusini wa Rafah kwenye mpaka na Misri.

Katika juhudi za kuzuia maandamano yanayoweza kutokea au matamshi kuhusu vita wakati wa Hajj, viongozi wa Saudi walisema hawatavumilia kuingiza siasa kwenye hijja. Kanali Talal Al-Shalhoub, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa jioni kwamba serikali ya Saudia “haitaruhusu jaribio lolote la kugeuza maeneo matakatifu (ya Makka) kuwa uwanja wa maandamano.”

Tahadhari ya joto kali

Wakati wa mwaka ambapo Hajj hufanyika hutofautiana, ikizingatiwa kuwa imepangwa kufanyika kwa siku tano katika wiki ya pili ya Dhu al-Hijjah, mwezi wa mwisho katika kalenda ya mwandamo ya Kiislamu. Ibada nyingi za Hajji hufanyika nje kukiwa na kivuli kidogo sana.

Inapoangukia katika miezi ya kiangazi, halijoto inaweza kuongezeka hadi zaidi ya 40 za Selsiasi. Wizara ya Afya imetahadharisha kuwa hali ya joto katika maeneo matakatifu inaweza kufikia 48 C na kuwataka mahujaji kutumia miavuli na kunywa maji zaidi ili kuwa na maji ya kutosha mwilini.

Saudi Arabia, Makka | Mahujjaji katika Mlima wa Rehema.
Hijja ya mwaka imefanyika katika mazingira ya joto kali.Picha: Ahmed Yosri/REUTERS

Wengi wa mahujaji katika Mlima Arafat walibeba miavuli, wakati wengine waliketi kwenye kivuli cha miti na majengo machache karibu na kilima cha rehema. Na, kama huko Mina na Msikiti Mkuu, vituo vya kupozea kwenye barabara zinazoelekea mlimani na katika maeneo ya jirani yake vilikuwa vinawanyunyizia mahujaji maji ili kuwasaidia kukabiliana na joto, ambalo tayari lilikuwa limepanda hadi 47 C kwenye Mlima Arafat, kulingana na Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Saudi Arabia.

Baada ya ibada ya Jumamosi katika Mlima Arafat, mahujaji watasafiri kilomita chache hadi eneo linalojulikana kama Muzdalifa kukusanya kokoto ambazo watatumia katika upigaji mawe mfano wa nguzo zinazowakilisha shetani huko Mina. Wengi hutembea kwa miguu, huku wengine wakitumia mabasi.

Mahujaji waelekea Mlima Arafat Makka

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Kisha mahujjaji hurejea Mina kwa siku tatu, zinazosadifiana na na sikukuu ya Eid al-Adha, ambapo Waislamu wenye uwezo wa kifedha duniani kote huchinja mifugo na kuwagawia watu masikini nyama hiyo. Baadaye, wanarudi Makka kwa ajili ya mzunguko wa mwisho wa Kaaba, unaojulikana kama Tawaf ya kuaga.

Mara baada ya Hajj kumalizika, wanaume wanatarajiwa kunyoa vichwa vyao, na wanawake kukata kidogo kwenye nywele zao kwa ishara ya mwanzo mpya. Wengi wa mahujaji kisha wanaondoka Makka kuelekea mji wa Madina, ulio umbali wa kilomita 340, kuzuru kaburi la Mtume Muhammad SAW, ambalo ni eneo takatifu.

Kaburi hilo ni sehemu ya msikiti wa Mtume ambao ni miongoni mwa maeneo matatu matakatifu zaidi katika Uislamu, pamoja na Msikiti Mkuu wa Makka na Msikiti wa Al Aqsa mjini Jerusalem. 

 

Related Posts