Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na mikoa hawafuati waraka uliotolewa na Serikali unaoelekeza uzingatiaji wa sheria na kanuni katika utekelezaji wa mamlaka yao ya ukamati badala yake wanaendeleza ubabe. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Waraka huo namba moja uliotolewa mwaka 2023 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka ulielekeza wakuu hao wa mikoa na wilaya namna ya kutekeleza mamlaka yao.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Ikulu Chamwino jijini Dodoma katika hafla ya kupokea Taarifa ya Kamati ya kuunda Mkakati wa utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

“Pamoja na waraka kutolewa mwaka jana, bado kuna wakuu wa mikoa na wilaya wanaendekeza ubabe kule walipo.

“Mwenyekiti wa kamati (Balozi Ombeni Sefue) wakati ananipa briefing ameniambia katika kikao chao na wakuu wa wilaya na mikoa, mmoja alisimama na kusema mimi ni mwakilishi wa rais hapa lolote linalotokea hapa ni la kwangu…  sasa nadhani bado hatujakaa vizuri,” amesema.

Amesema wakuu hao wa mikoa au wilaya aidha, elimu inahitajika kwao zaidi kutambua mipaka yao au kuna usugu unaohitaji kushughulikiwa.

Amesema ili waraka huo uzingatiwe lazima wajue taratibu za kazi zao na mipaka yao iwe ni watendaji wa serikali za mitaa au serikali kuu.

Related Posts