Ukaguzi wa haki za wafanyakazi viwandani waja

Kimbiji. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Serikali ina mpango wa kuanza ukaguzi viwandani na maeneo yaliyoajiri watu kuangalia mikataba na uhusiano ya watumishi na waajiri wao kuanzia Julai mwaka huu.

Chalamila ametoa kauli hiyo jana Ijumaa Juni 14, 2024 alipohudhuria sikukuu ya wafanyakazi ya Kiwanda cha Lake Cement Company Limited kinachozalisha saruji za nyati kilichopo Kimbiji wilayani Kigamboni Dar es Salaam.

“Yapo  maeneo wafanyakazi wamekuwa wakirushiwa matusi, wakipigwa hivyo tutaanza mwezi ujao opereshi maalumu kuangaliia uhusiano wa watumishi na waajiri kazini,” amebainisha Chalamila.

Pia, amegusia mkakati wa Serikali ya mkoa huo kuwa na mpango wa kufuatilia wawekezaji kurejesha uwajibikaji wa kijamiikwa mujibu wa sheria.

Aidha, akizungumza kuhusu kiwanda hicho kilichoajiri wafanyakazi 900, amesema Serikali itaendelea kukishika mkono kwakuwa kinachangia uchumi wa nchi kupitia kodi.

Vilevile, amekisihi kiwanda hicho kuwakumbatia wafanyakazi wake kwa kuwaongezea mishahara pamoja na kikipata faida kiweze kurejeshe kwa wafanyakazi wake.

“Wafanyakazi lazima wapate faida ya kiwanda kwa kuwa katika hali ya kawaida hawakopesheki hivyo lazima wagawiwe kidogo na wao,” amesema.

Chalamila amesema lazima kuwe na mnyororo ambao wafanyakazi na waajiri kila mmoja amuheshiku mwenzake kwasababu wafanyakazi katika viwanda huwa wanamaisha magumu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ya Lake, Biswajeet Mallick amesema kiwanda kiko kwenye upanuzi ambapo kitaongeza uzalishaji kutoka tani 600, 000 hadi milioni moja kwa mwaka.

“Tutaendelea kutengeneza ajira kwa Watanzania, kwa sasa tuna wafanyakazi 300 wa kudumu na 600 wenye mikataba isiyo ya muda mrefu.

“Mbali na kuajiri tumeendelea kurudisha kwa jamii ikiwamo kujenga madarasa, mabweni na kuweka umeme hospitali na polisi kata pamoja na kupanda miti zaidi ya 1,000 kila baada ya muda kwa lengo la kulinda mazingira yetu,” amesema mkurugenzi huyo.

Katika sherehe hiyo wafanyakazi waliokaa miaka kumi na wale waliokaa miaka mitano wamepewa zawadi ikiwamo magodoro pesa na mifuko ya saruji ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango na umuhimu wao.

Emile Mbabilanyi,  mfanyakazi wa kiwanda hicho aliyedumu kwa miaka 10 amesema Serikali inatengeneza mazingira mazuri ya wawekezaji na Watanzania wanapata ajira.

“Kilichobaki Serikali iweke kima kimoja kwa wafanyakazi wa chini kulingana na hali halisi ya maisha na mfumuko wa bei za bidhaa ikiwamo vyakula,” amesema Mbabilanyi.

Related Posts