Dar es Salaam. Walimu wapatao 47 wa halmashauri nne za Mkoa wa Lindi wamehitimu shahada (diploma) ya Usimamizi na Utawala wa Elimu (Dema) iliyofadhaliwa na Mradi wa Foundations for Learning (F4L), wakisoma kwa miaka mwili kwa njia ya mtandao na darasani.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Juni 15, 2024 na Taasisi ya Maendeleo ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, Afrika Mashariki (AKU-IED EA) imesema mafunzo hayo yaliendeshwa kwa mtandao na shule zilipofungwa kwa nyakati tafoati walikutana katika Taasisi ya Wakala wa Maendeleo ya Usimamizi wa Elimu (Adem) Bagamoyo mkoani Pwani.
AKU-IED EA imeshirikiana na Adem katika kufanikisha mafunzo hayo yaliyoshirikisha wakuu wa shule halmashauri za Lindi Mjini, Mtama, Nachingwea na Ruangwa.
Miongoni mwa mambo waliojengewa uwezo katika mafunzo hayo ni mbinu za kufundisha na kujifunza, hasa katika maeneo ya ufundishaji masomo ya Kiingereza na hisabati, ujumuishaji wa kijinsia na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Mkuu wa AKU-IED EA, Profesa Jane Rarieya, amesisitiza kuhusu kanuni kuu zinazoongoza programu ya Dema akikazia suala la umuhimu wa usawa wa kijinsia.
“Usawa wa kijinsia siyo tu kuhusu kufikia uwiano wa idadi, ni kuhusu kuunda mazingira kila mtu bila kujali jinsia anahisi kuthaminiwa, kuheshimiwa na kupewa nguvu ya kufikia uwezo wao kamili,” amesema Profesa Rarieya.
Profesa Rarieya amesema kukamilika kwa programu ya Dema kunaashiria sura mpya kwa walimu hawa nchini.
“Tutaendelea kuunga mkono Wizara ya Elimu nchini kwa kuwawezesha walimu kupata ujuzi wa karne ya 21 unaohitajika kwa mabadiliko ya elimu nchini na zaidi,” amesema Profesa Rarieya.
Mahafali ya kuhitimu programu yamefanyika Nachingwea yakiambatana na maonyesho ya wahitimu, walioshiriki hadithi zao za mafanikio kuhusu programu ya Dema, wakisema imekuwa na mabadiliko katika nafasi za uongozi na ukuaji binafsi.
Walimu hao walionyesha namna ya walivyokabiliana na changamoto zinazokabili shule zao, ikiwa ni pamoja na masuala kuandika mapendekezo kwa ajili ya kutafuta rasilimali, ubunifu wa kuunda kona za kujifunzia katika darasa la awali, ujumuishaji wa kijinsia na ushirikishwaji na ujumuishaji mzuri wa Tehama katika ufundishaji na ujifunzaji.
Mwalimu Onesmo Samuel anayefundisha Shule ya Msingi ya Mnara wilayani Ruangwa, alipata fursa ya kuwasilisha jalada lake kupitia mtandao wa Zoom kutoka jijjni Arusha.
Katika jalada lake hilo lilionyesha safari ya mabadiliko ya programu yao ya stashahada.