Dar es Salaam. Asilimia 80 ya vijana waliohojiwa katika utafiti wa ulinzi na usalama mitandaoni wamesema hawapo salama.
Hayo yamebainika leo Jumamosi Juni 15, 2024 katika mdahalo wa vijana na matumizi ya mitandao ulioenda sambamba na uzinduzi wa ripoti ya utafiti uliyofanywa na Shirika la Mulika Tanzania linalojishughulisha na masuala ya vijana.
Ofisa Uchechemuzi na Mawasiliano wa shirika hilo, Whitness Satory amesema vijana katika maoni yao wamekuwa wakitishwa na kudhalilishwa katika utumiaji huo wa mitandao, hivyo wengine kuogopa kuitumia.
“Kwa upande wa vijana wa kike wamesema wao ndio waathirika wakubwa kwa kuwa picha zao za utupu zimekuwa zikisambazwa na nyingine wakiwa faragha,” amesema Whitness.
Whitness amesema malengo ya utafiti huo imetokana na kuwepo ongezeko la vijana wanaotumia mitandao na kutaka kujua usalama wao, vikwazo wanavyopitia na kupeleka maoni hayo kwa mamlaka ili kujua namna gani wanazofanyia kazi.
Katika maoni yao, Michael Ndaki ametaka elimu zaidi namna ya kuwaripoti wanaowadhalilisha wenzao.
Kwa wanaotishwa, amesema wameishia kupata msongo wa mawazo kwa kutojua nini cha kafanya wanapofikwa na hali hilo.
Awali, akizungumza katika mdahalo huo, Ofisa Tehama Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Irene Kahwili amewataka vijana wanaodhalilishwa mitandaoni kuripoti polisi ili hatua zaidi ziweze kuchukiliwa.
“Kumekuwepo na tabia za watu kuja kuripoti TCRA pale wanapodhalilishwa mitandaoni, naomba niwambie hilo ni kosa kama makosa mengine ambayo yanapaswa kuripotiwa polisi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka Kitengo cha Makosa ya Kimtandao, Alpha Assey, amewashauri vijana kuchagua lugha na vitu vya kuandika mitandaoni ili wasije wakajikuta wanaingia matatizoni.
“Hapa naomba nisisitize sio kila kinachopostiwa mtandaoni sio lazima utoe maoni yako unaweza ukachambua kwamba unafaa kulitolea maoni au la na kwa lugha gani ili baadaye usije ukajikuta unaingia matatizoni kwani hakuna utoaji maoni usiokuwa na mipaka,” amesema Assey.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto, vijana pia wamekiri kuwepo kwa fursa katika mitandao ya kijamii lakini wamesema changamoto bado ipo katika bei za vifurushi na uimara wa upatikanaji wa mtandao.
Marry Mbago amesema hali hii inaweza kuwakosesha fursa hizo vijana wengi hasa waliopo vijijini ambao vipato vyao ni vya chini sio kwao tu bali hata kwa wazazi na walezi wanaowategemea.