Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kusikitishwa na baadhi ya wakuu wa mikoa na wa wilaya kupuuza utekelezaji wa waraka wa Serikali unaoelekeza na kusisitiza uzingatiaji wa sheria na kanuni wakati wa kutumia mamlaka yao ya kukamata watu.
Amesema licha ya waraka huo uliotolewa mwaka 2023 na Katibu Mkuu Kiongozi Moses Kusiluka, bado kuna wakuu wa mikoa na wa wilaya wanaendeleza ubabe wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Rais Samia amesema hayo Juni 15, 2024 Ikulu jijini Dodoma wakati wa kupokea taarifa ya mkakati wa utekelezaji wa mapendekezo ya kamati ya Tume ya Haki Jinai.
“Nikimnukuu makamu mwenyekiti wakati ananipa muhtasari, aliniambia wakati wa kikao chao na wakuu wa wilaya, mmoja alithubutu kusimama na kusema mimi ni mwakilishi wa Rais hapa, kwa hiyo lolote lililopo huku ni la kwangu, hata nikihisi mahakama imeamua sivyo, mimi nitatengua,” amesema.
“Sasa nadhani bado hatujakaa vizuri, hivyo huenda elimu zaidi inahitajika au kuna usugu wa aina fulani unahitaji kushughulikiwa. Nielekeze kuwa waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi uzingatiwe na ufanyiwe kazi vizuri, lazima kila mmoja ajue taratibu za kazi zake na mipaka yake, kila nafasi ina mipaka yake,” amesema Rais Samia.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais kukemea ubabe, mtangulizi wake, Rais John Magufuli mwaka 2019 aliwahi kuwakemea viongozi hao kwa kuwaweka rumande raia.
Akizungumza wakati wa kuapisha majaji na wakuu wa wilaya wawili Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli wakati huo alisema kuna masuala mengine yanaweza yakapata ufumbuzi kupitia njia ya mazungumzo kuliko kumweka mtu ndani.
“Wakuu wa wilaya mna mamlaka yenu lakini myatumie vizuri, ni kweli sheria imewapa mamlaka lakini ni muhimu kuyatumia vizuri mamlaka yenu, bahati nzuri hili limeshasemwa sana na watu wengi nami narudia, wakuu wa wilaya mtumie mamlaka yenu vizuri,” alisema Rais Magufuli.
Alisema kumweka mtu rumande kisha kumtoa pasipo kumpeleka mahakamani hakumfanyi mhusika kujifunza.
“Mtu unamweka ndani kisha unamtoa eti amejifunza, amejifunza wapi si ungempeleka hata mahakamani, kuna masuala mengine yanaweza yakaleta athari nzuri kwa maongezi, kuliko hata kumweka mtu ndani,” alisema.
Mapendekezo ya haki jinai
Rais Samia amesema utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki jinai umepewa kipaumbele kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa wizara zote ikiwemo ya Katiba na Sheria, ambayo inatakiwa kutunga sera ya Taifa ya haki jinai.
Hatua hiyo inaonyesha kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na kuyatumia kuleta mageuzi chanya kwenye mfumo wa haki jinai.
“Faraja yangu ni kwamba yale yaliyokuwa yakinikereketa rohoni, sasa yanachukua sura mpya ya mabadiliko katika kutenda haki ndani ya nchi yetu,” amesema.
“Wajibu wa kuimarisha haki za raia kama zilivyoelezwa kwenye Katiba ya nchi si suala la hiari, bali linapaswa kufanyiwa kazi ipasavyo. Sote tunalazimika kusimama katika upande wa haki, suala la haki halina mbadala ndiyo maana tunaendelea kuchukua hatua hizi. Ninaelewa baadhi ya taasisi zetu zinasuasua katika kutekeleza mapendekezo ya tume, ambayo yanalenga kuleta mabadiliko,” amesema.
Rais Samia amesema: “Mabadiliko haya yanapaswa kuwa kwenye utendaji na fikra na mawazo yetu, haya ni mabadiliko makubwa, naelewa kila mabadiliko yanakuwa na upinzani na wakati mwingine watu wanakuwa na hofu.”
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti, Balozi Ombeni Sefue ameshauri miundombinu ya taasisi za haki jinai ipewe kipaumbele katika maeneo ya kiutawala.
“Huko tuendako wakati wa kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala ikiwemo mikoa na wilaya, Serikali ihakakikishe yanakuwapo majengo ya kutosheleza mahitaji ya taasisi za haki jinai,” amesema.
Balozi Sefue amesema, “Majengo hayo ni pamoja na vituo vya polisi, magereza, shule za kurekebisha watoto, mahakama, ofisi ya Taifa ya mashtaka na miundominu ya kisasa ya kuhifadhia vielelezo. Hatutakuwa tunawatendea haki wananchi kwa kuanzisha maeneo mapya ya utawala ambayo hayakidhi mahitaji hayo muhimu kwa ajili ya utawala bora.”
Amesema pendekezo hilo ni matokeo ya tathmini iliyoonyesha utendaji bora na ufanisi wa taasisi za haki jinai, ni sehemu ya msingi katika utawala bora na utoaji haki.
Balozi Sefue amesema kamati inapendekeza kuwapo mpango mahususi wa kuongeza bajeti ya taasisi za haki jinai katika miaka mitano mfulululizo ya kutekeleza mkakati huo ili kupunguza upungufu ulipo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa majengo na ununuzi wa vitendea kazi.
Amesema bajeti ambayo inatolewa kila mwaka kwa taasisi za haki jinai ni pungufu sana ya mahitaji halisi.
“Kamati ilithibitisha hali hiyo kwa kufanya uchambuzi na tathmini za ugharimiaji shughuli za taasisi husika za haki jinai katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita 2021 hadi 2023. Kwa miaka mingi bajeti iliyokuwa inatolewa kwa taasisi hizi ilikuwa chini ya mahitaji halisi,” amesema.
Amezitaja taasisi hizo ni mahakama, ofisi ya Taifa ya mashtaka, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Amesema katika kipindi hicho cha miaka mitatu taasisi hizo sita zilipokea jumla ya Sh1.99 trilioni na uchambuzi uliofanywa na kamati umebaini mahitaji ya rasilimali fedha zitakazohitajika ili kutekeleza ipasavyo mapendekezo ya Tume ya Haki jinai.
Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amewataka watendaji wa Serikali kutilia maanani taarifa ya tume hiyo kwa kuwa Tume zilizopita taarifa zake hazikutekelezwa kwa ufanisi.
Ametoa mfano wa Tume ya Jaji Bomani ya mwaka 1996 ambayo ilitoka na taarifa ya maboresho ya sheria mbalimbali lakini kutokana na bajeti kubwa ya Dola 286 milioni za Marekani, utekelezaji wake ulikuwa wa mafungu-mafungu na haukukamikika.
Profesa Juma ametaja pia Tume ya Msekwa ya mwaka 1977, huku akisema Tume ya Haki Jinai ya sasa imekuja na mikakati ya utekelezaji wa mapendekezo yake na amewataka watendaji kuifanyia kazi.
“Huu ni wakati tukiupoteza hatutaupata tena,” amesema.
Amesema jambo linalotakiwa ni utashi wa umiliki wa mapendekezo ya tume kwa kuwa yametokana na wananchi wenyewe, tofauti na zamani ripoti zilibaki kwa Rais mwenyewe.
Profesa Juma amewataka watendaji wa taasisi za haki jamii na wale wa Serikali kuwa na mtazamo chanya na kuacha mambo ya kunga’ng’ania sheria za zamani.
Spika Dk Tulia Ackson amesema Bunge liko tayari kurekebisha sheria zitakazopelekwa kuhusu haki za watu.
Amesema Bunge liko kwenye mchakato wa bajeti ya Serikali, hivyo yaliyoelezwa na Tume bado yana nafasi ya kujadiliwa.
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema kama eneo la utawala bora halijawekwa vizuri, hata Dira ya Maendeleo iwe bora kiasi gani, haiwezi kulifikisha Taifa kwenye safari yake.