MTU WA M PIRA: | Mwanaspoti

KUNA mambo mengi yanaendelea ndani ya Simba. Ilianza na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kujiuzulu. Baadaye akaja Mwenyekiti Salim Abdallah Muhene ‘Try Again’. Ni historia.

Ni muda mrefu hatujaona viongozi wa Klabu hizi kubwa nchini wakiwajibika baada ya mambo kwenda ndivyo sivyo. Kina Try Again na wenzake wanapaswa kupongezwa.

Baada ya hapo ikaja taarifa ya mwekezaji Mohamed Dewji ‘MO’ kurejea ndani ya Bodi ya Wakurugenzi. Anarejea kama mwenyekiti. 

Na hapa ndipo shida ilipoanzia. Huko mitandaoni yakaanza maneno mengi. Kwa nini Mo anarejea? Anarudi kama nani? Kwani katiba inasemaje?

Baadaye yakaja maneno, hata kama anarejea lakini Mwenyekiti wa Bodi awe Murtaza Mangungu? Yanatoka wapi haya? Inachekesha sana.

Katiba ya Simba inasema vyema kabisa. Mwenyekiti wa Bodi anatoka upande wa Mwekezaji. Haijalishi Katiba ilikosewa ama la, ila inampa mwekezaji nguvu kubwa.

Pamoja na upande wa Simba kutoa wajumbe sawa na mwekezaji, bado kuna mamlaka makubwa amepewa mwenye pesa zake. Kwa nini? Kwa sababu yeye ndiye anatoa pesa.

Huu upande wa kina Mangungu na wenzake wanatoa kiasi gani kwa mwaka pale Simba? Hakuna. Wanajivunia tu nembo ya klabu. Wanaamini fedha za wadhamini ni zao. Ila kuna uhalisia gani?

Kina Mangungu wanawakilisha wanachama wanaopaswa kulipa ada kila mwaka kuchangia klabu yao. Simba ina wanachama wangapi hadi leo? Inachekesha. 

Ni kweli upande wa wanachama Simba una asilimia kubwa katika uwekezaji. Wana 51%. Ila wako wangapi? Wanachangia nini kwenye timu? Hakuna!

Ukweli ni kwamba wakati Dewji anatoa Sh20 bilioni, wanachama wanapaswa kuwa wengi na kuchangia klabu yao kila mwaka.
Hii ndio kazi ya Mangungu na wenzake. Kuhamasisha wanachama wengi zaidi. Kuhamasisha walipe ada zao. Ndio namna hisa zao zitafanya kazi. Wanafanya hivyo? Sijaona.

Wanachofanya ni kutegemea fedha za udhamini na mwekezaji kuendesha timu. Ni fedha nyingi ila hazitoshi. Zinapaswa kujaziwa na zile za wanachama.

Inachekesha hadi leo Simba ina wanachama wasiofika 10,000 nchi nzima. Inawezekanaje? Timu yenye mashabiki zaidi ya Milioni 15 inakuwaje na idadi ya wanachama sawa na Mbuzi wa Mmasai mmoja huko Longido?

Kituko zaidi ni zimekuja kauli Simba inaweza kwenda bila mwekezaji. Ni kichekesho! 
Nani anakumbuka maisha ya Simba kabla ya Dewji kuwekeza? Yalikuwa yanatia huruma. Simba ilikuwa tu kama Tabora United ama Mashujaa? Haikuwa na uhakika na chochote.

Hawakuwa na uhakika wa wachezaji wa kusajili. Hawakuwa na uhakika na mishahara wala kula yao. Hawakuwa na ushindani kwenye ligi. Walishika hadi nafasi ya nne. 

Walikuwa wakipata fedha kiduchu katika udhamini wao. Mashindano ya Afrika walishiriki mara chache na wala hawakuwa na maajabu. Simba ilitia huruma sana. 

Hapa ndipo Dewji aliamua kuwekeza. Bajeti ya Simba wakati ule haikuwa inafika Sh2 Bilioni kwa mwaka. Sasa inafika Sh20 Bilioni. Amewatoa mbali kama wana wa Israel kutoka Misri kwenda Kaanani.

Kwa nini hatuheshimu alichofanya Dewji? Ni kiburi, jeuri ama kujisahau? Inashangaza sana.
Kama kabla ya mwekezaji Simba ikiwa na mashabiki wote hao ilishindwa kujiendesha tena kwa bajeti kiduchu, utaweza leo ambapo washindani wao Yanga wamepitisha bajeti ya Sh24.5 Bilioni? Nimekaa pale natazama. Haiwezekani.

Kuna watu kwa masilahi yao wanataka kuirejesha Simba zama za mawe. Zama za umasikini. Zama za kuombaomba. Kutia huruma. Inafikirisha.

Ukweli ni Simba na Yanga zilipofika sasa zinahitaji nguvu ya wawekezaji. Unawezaje kulipa mishahara ya zaidi ya Sh7 Bilioni kwa mwaka bila mwekezaji? Ni ngumu. Ni kama kunywa supu na vitumbua.

Hizi timu zinahitaji wawekezaji kwa sasa. Tena wawekezaji wanaotoa fedha nyingi.
Kinachopaswa kufanywa na wanasimba sasa ni kumsisitiza Dewji atoe fedha zaidi ya GSM Ili kushindana na Yanga. 
Ndio njia pekee ya kuwarejesha kwenye ushindani. Haya mengine ni porojo tu.

Related Posts