Tangulia Chifu Ferdinand Kamuntu Ruhinda

TAIFA liko msibani. Usiku wa juzi Ijumaa, saa 3:00 usiku alifariki dunia mmoja wa Watanzania walioweka alama ya pekee katika historia ya taifa letu, Balozi Chifu Ferdinand Kamuntu Ruhinda (1938-39).

Balozi Ruhinda anayetoka katika familia ya uchifu ni Mwandishi wa Habari kitaaluma na mwanadiplomasia.

Alipata elimu yake ya uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Nairobi na akapata mafunzo ya uandishi wa habari ndani na nje ya Tanzania.

Kabla hajaingia katika medani ya diplomasia miaka ya mwanzo ya 1980, aliwahi kuwa Mhariri Mkuu wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD -sasa TBC Taifa).

Alihudumu Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, baadaye akateuliwa Balozi wa Tanzania nchini Canada (1983 -1988) na China (1989 -1992) kabla ya kustaafu.

Kwetu sisi wana tasnia ya habari kwa jumla, Mzee Ruhinda ni nguzo na moja ya mihimili mikuu na ithibati ya ustawi wa vyombo vya habari Tanzania.

Anao urathi (legacy) mkubwa kwanza katika kampuni ya magazeti ya serikali ya Daily News na Sunday News ambayo yanaendeshwa na kampuni ya Tanzania Standards Newspapers (TSN) alikowahi kuwa Mhariri Mtendaji wake.

Ruhinda anao urathi pia katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo ambako pia alipata kufanya kazi hadi akafika wakati akawa ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya magazeti hayo ya Uhuru Publications Ltd baada ya kustaafu utumishi wa umma.

Alikuwa pia nguzo kuu wakati Tanzania iliporuhusu kuanzishwa kwa vyombo binafsi vya habari na akafanya kazi akiwa miongoni mwa waanzilishi wa kampuni ya Business Times Ltd walipoanzisha magazeti ya Business Times na Majira miaka ya mwanzo ya 1990.

Mzee Ruhinda ndiye mwanzilishi kinara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) akishirikiana na Rostam Azizi mwaka 2000 ikiwa ni zao la kampuni binafsi ya awali ya Media Communications Ltd.

Naam. Kama kuna jambo linanipa fahari kubwa katika maisha yangu ya uandishi wa habari ni kupata kufanya kazi na Balozi Ruhinda, nikiwa ndiye mwajiriwa wa pili katika Idara ya Uhariri ya Media Communications Ltd baada ya Muhingo Rweyemamu Desemba 1999 tena baada ya kufanyiwa usaili naye.

Kama kuna mtu mmoja aliyepitia kwake nilipata fursa ya kumfahamu kwa ukaribu zaidi Rais Benjamin Mkapa ambaye ukaribu wao ulipita misingi ya urafiki wa kawaida na kuwajengea ushirika mkubwa wa kuaminiana, basi mtu huyo ni Mzee Ruhinda.

Kupitia kwa Mzee Ruhinda, nikajifunza namna na maana ya kuwa kiongozi, kufikiri tofauti na zaidi kujua maana halisi ya ustaarabu na utu wema.

Kupitia kwake nilijua maana halisi ya mtu asiye na makuu ambaye pamoja na kuwa mwandani (confidant) wa mtu mwenye mamlaka makubwa kama Rais Mkapa hakujikweza, hakuwa na maringo au majivuno na alikataa kila cheo cha kisiasa au kiserikali zaidi ya kujijengea ushawishi, hadhi, ustawi wake wa kibiashara na zaidi kuanzisha chombo cha habari akilenga kwa kauli yake mwenyewe kuimarisha misingi ya uandishi unaozingatia weledi na uliotukuka.

Kupitia kwa Ruhinda ndiko nilikopata wasaa na fursa ya kuanza kufanya kazi kwa karibu zaidi naye kwani mara kadhaa tukikutana ofisini kwake na baadaye Vodacom kati ya 2001 na 2003 alikonihamishia kufanya kazi kama mshauri wa mawasiliano kutoka katika chumba cha habari kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Kupitia kwa Ruhinda ndipo nilipojua haswa uhusiano wa taasisi za dola vikiwamo vyombo vya ulinzi na usalama na vyombo vya habari na Ikulu na wamiliki wa vyombo vya habari, kwani kwa kuwa kwake na imani binafsi kwangu alinipa kwa sehemu tu nafasi ndogo ya kushiriki katika baadhi ya mikutano iliyofikia maamuzi mazito.

Kupitia kwa Mzee Ruhinda nilijifunza unaweza ukawa mtu mwenye mamlaka makubwa, hadhi ya kipekee, heshima na ushawishi usioweza kuelezeka kitaifa pasipo kuwa na madaraka yawe ya kuchaguliwa au kuteuliwa.

Kupitia kwake nilijifunza namna alivyokuwa ana ushawishi na pengine ukaribu mkubwa nyuma ya urais wa Ben Mkapa na ndiye mtu pekee ambaye kwa zaidi ya mara tatu nilipata kumsikia mimi mwenyewe akizungumza na Mkapa kwa simu na kumkosoa na wakati mwingine kuendesha gari lake mwenyewe hadi Ikulu alikokwenda kueleza dukuduku lake na wakati mwingine karipio la dhahiri kwa Rais na Mkapa binafsi akakiri kukosea na mara moja kati ya hizo, Mkapa akaenda kumwomba radhi mtu aliyemkosea.

Ninaweza kutaja hapa mifano miwili, wa kwanza ukiwa ni ule wa mahojiano ambayo Rais Mkapa aliyafanya na mtangazaji maarufu wa CNN, Tim Sebastian ambayo yaliishia kwa Mkapa kutoa kauli za kuhamaki na kunasa katika mtego wa maswali magumu.

Wakati mahojiano hayo ya Mkapa yakirushwa kwa mara ya kwanza, tulikuwa ofisini na Mzee Ruhinda tukiyafuatilia.

Mara tu baada ya mahojiano hayo kumalizika, Ruhinda aliyekuwa akizungumza kwa utulivu hata anapokuwa amekasirika, alieleza kusikitishwa sana na namna Mkapa alivyohamaki na kupoteza haiba ya utulivu na ukomavu kama mwanahabari.

Saa chache baadaye aliinua simu na kupiga kwa wasaidizi wa Rais na akaunganishwa na Mkapa.

Hakusubiri wala kumung’unya maneno na akamweleza mshangao wake wa namna alivyonaswa katika mtego wa kukasirishwa na maswali ya Tim Sebastian ilihali yeye mwenyewe akiwa ni mwanahabari.

Mfano wa pili ni siku Rais Mkapa alipokuwa akipokea Ripoti ya Tume ya Rais Jaji Kisanga ambako pia Rais alionyesha kukerwa sana na ripoti ile na akairarua mbele ya Jaji na wajumbe wenzake kwa maneno makali akisema eti walikuwa wamefanya kazi ambayo wala haikuwa sehemu ya hadidu rejea zao.

Kama kuna siku nilimwona Ruhinda akiwa amekasirishwa na Mkapa basi ni hiyo kwani alitueleza namna alivyojivunjia hadhi ya urais na akakasirika kwa jambo ambalo hakupaswa kulikasirikia, kwani Jaji na timu yake walikuwa wametekeleza wajibu wao ipasavyo.

Basi Ruhinda alipiga simu kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Apson Mwang’onda na akaomba apate fursa ya kwenda kuonana na Rais akitueleza bayana mimi, mhariri wangu Muhingo Rweyemamu na Meneja wa Fedha, Basil Herri tuliokuwa ofisini kwake, alikuwa anakwenda kumshauri Mkapa aombe radhi. Akaenda Ikulu.

Nakumbuka siku niliyokuja kukutana naye baada ya safari yake ya Ikulu nilimuuliza swali juu ya majibu ya Rais Mkapa kuhusu ushauri wake.

Ruhinda ambaye nilikuwa nikimwita baba kwa sababu tu ya kuzaliwa kwake mwaka mmoja na baba yangu mzazi Norman Absalom Kapyela, alinijibu moja kwa moja ‘mwanangu, Mkapa alimpigia simu Jaji Kisanga na kuomba radhi’. Huyo ndiye Ferdinand Ruhinda.

Hakika nilimfahamu Mkapa halisi kupitia kwa Mzee Ruhinda ambaye kupitia kwake ndiye aliyenipa heshima na fursa adhimu ya kumsikia, kumsikiliza na wakati fulani hata kusafiri naye kwa

Maelekezo mahususi ya zaidi ya kihabari wakati wa kampeni yake ya urais mwaka 2000 na baadaye nje ya nchi wakati akiwa katikati ya kipindi chake cha pili cha urais.

Alikuwa ni Ruhinda tena aliyeshiriki kufungua milango kwangu ya kuuona urais wa Amani Abeid Karume Zanzibar mwaka 2000 hata kabla mchakato rasmi haujaanza.

Katika kilele cha kukamilika kwa huo mchakato, tulisafiri kwa pamoja na Ruhinda kwa ndege ndogo ya kukodi kwenda na kurudi Dodoma tukitokea Dar es Salaam, tukiwa miye, Rostam Azizi, Muhingo Rweyemamu na msaidizi maalum wa Karume.

Tuliporejea, wala sikushangaa kuona Karume akiwa ameshapitishwa kuwa ndiye mgombea wa urais wa CCM Zanzibar katika mazingira magumu sana, maana nilijifunza mengi kwa kusikia na kusikiliza safari yoote ya kufanikisha matokeo yake.

Ilikuwa ni hivyo hivyo pia wakati wa mchakato wa kumrithi Rais Benjamin Mkapa na kupitia kwa Mzee Ruhinda ndiko nilikojua hasa njia ambayo hatimaye Mkapa angetoa dokezo la mgombea ambaye angetaka awe mrithi wake.

Nilibaki na siri hii moyoni hadi vilipokaribia vikao viwili vya uteuzi vya Kamati Kuu na Halmashauri ya Taifa ya CCM siku nilipoamua liwalo na liwe nikatumia uhariri wangu na taarifa za ndani na za uhakika nilizokusanya kutoka katika mazungumzo yasiyo rasmi ya mara kwa mara na Mzee Ruhinda nikaandika kile kilichomkera sana sana Ruhinda.

Huku nikijua nilikuwa sina kibali au ridhaa yake nilieleza namna Rais Mkapa alivyokuwa amepanga mapema kwa makubaliano na kina Ruhinda.

Kichwa cha habari katika gazeti la Mwananchi Jumapili kilichomkasirisha sana Mzee Ruhinda akapiga simu kwangu kueleza kusononeka kwake lakini zaidi kunikosoa kwa kuandika jambo ambalo aliniambia halina ukweli wowote kilisomeka; “Dokezo la Mkapa kutoa Mgombea Urais CCM 2005”.

Kwa kuwa nilikuwa nikijua nilichoandika nilikuwa nina hakika nacho na pili kilitokana hasa na kile nilichokisikia mara kadhaa kwake mwenyewe niliomba radhi na mchakato ulipoanza na Mkapa akatoa dokezo kwa namna ile ile nilivyoandika, nilirudi kwa Mzee Ruhinda na kumueleza nilikuwa nina faraja sana moyoni nilichoandika kilitokea.

Mzee Ruhinda alitabasamu na akaishia kuniambia kosa langu kubwa lilikuwa kuandika jambo sahihi kwa wakati usio sahihi. Tulielewana kwa sababu kuu mbili, andiko langu lililomkera lilimfurahisha sana mshirika wake kibiashara katika kampuni ya Mwananchi Communications, Rostam Azizi.

Naweza nikaandika kwa kujiamini kabisa alikuwa ni Mzee Ferdinand Ruhinda aliyenipa fursa adhimu ya kushiriki kikamilifu kifikra na siyo kimkakati katika mchakato wa awali wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 na akaniwezesha pia kuwa na taarifa nyingi na za ndani za kisiasa, kiuongozi na kimkakati za kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ambao hatimaye Jakaya Kikwete alikuja kuwa mteule wa CCM kwenye kinyang’anyiro cha urais na baadaye akashinda urais kwa kishindo. Nyuma ya safari hiyo alikuwapo Ferdinand Ruhinda.

Ni dhahiri nikiwa mwanahabari, kupitia kwa Mzee Ruhinda nilipata fursa adhimu iliyonisaidia kuongeza uelewa wangu wa mambo mengi ambayo vinginevyo nisingepata kuyajua.

Kupitia kwa Ruhinda nilifanya kazi na kuwafahamu kwa karibu, kwa mapana na marefu, kwa amani na shari, kwa wema na ubaya, Apson Mwang’onda, Abdulrahman Kinana, Rostam Azizi, Tryphon Rutazamba, Jenerali Ulimwengu, Salvatory Rweyemamu, Anna Muganda, Georgia Mutagahywa, Leticia Kaijage, Dk. Harrison Mwakyembe, Isaac Mruma, Muhingo Rweyemamu na Theophil Makunga.

Kupitia kwa Ruhinda nilijifunza namna halisi ya kuwa mwandishi mwenye weledi katika kuchambua mambo kwa kina na katika misingi ya haki hasa aliponiunganisha na Mzee Mkapa wakati fulani na kukosoa mtazamo hasi niliokuwa nao kuhusu hatua ya Serikali kuibinafsisha iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Kwa kweli nina mengi zaidi ya hayo ya kueleza kuhusu Kamuntu Ferdinand Ruhinda.

Apumzike kwa AMANI Chifu Ruhinda kama alivyokuwa akiitwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akionyesha kutambua kuzaliwa kwake katika ukoo wa kichifu.

Related Posts