MABOSI wa Yanga wakiendelea kumfuatilia kwa ukaribu Phillipe Kinzumbi wa TP Mazembe ya DR Congo aliyedaiwa kusaini kwa mabingwa wa Morocco, Raja Casablanca, lakini wanapiga hesabu kali mpya katika kusuka safu ya ushambuliaji ikidaiwa imeanza mazungumzo kumbeba Mfungaji Bora wa zamani wa Ligi Kuu Bara, George Mpole.
Ishu ya Kinzumbi bado ni tetesi tu, kwani menejimenti yake imesema zilizotangazwa ni habari za mtandaoni na hakuna ukweli, hasa baada ya mabosi wa Yanga kuingiwa presha kwani walikuwa wakimpigia hesabu za kutaka kumvuta aje kuungana na Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua waliamshe kikosini.
Mwanaspoti imethibitishiwa na mmoja wa wanaomsimamia mchezaji huyo akidai dili bado halijakamilika na lolote linaweza kutokea, lakini sio kweli kama tayari keshamwaga wino wa miaka miwili Raja.
Achana na ishu ya Kinzumbi, mabosi hao wa Yanga wameanza kuzungumza na George Mpole aliyesaliwa na mkataba wa miezi sita katika klabu ya FC Lupopo ya DR Congo aliyojiunga nayo mara baada ya kutwaa Kiatu cha Dhahabu kama Mfungaji Bora wa Ligi Kuu msimu wa 2021-2022 akifunga mabao 17.
Mpole jana alikuwa jijini Mbeya katika mechi ya hisani, lakini Yanga inamtaka kwa nia ya kuboresha safu ya ushambuliaji kwa msimu ujao, huku kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama akitajwa katika dili hilo.
Hesabu za Yanga kumtaka Mpole zinatokana na mchakato wa kutaka kumsajili Chama ambaye mabingwa hao wa Tanzania wanamhitaji pia kwa msimu ujao na inaona kabisa ina nafasi kubwa ya kumbeba Mzambia huyo hivyo kulazimika kumtema mmoja ya wachezaji wa kigeni na wenyewe wamelenga washambuliaji.
Yanga inaona ili kupata nafasi ya Chama itahitajika kumpunguza mmoja kati ya Joseph Guede na Kennedy Musonda na baada ya kumpisha Chama basi watafute mshambuliaji mzawa mwenye makali na Mpole ametajwa ndiye mtu sahihi.
Mabosi wa juu wa Yanga, wanaamini katika kiwango cha Mpole na tayari wameshapiga hodi FC Lupopo wakiongea na tajiri wa klabu hiyo, Jacques Kyabula Katwe juu ya kuangalia uwezekano wa kumrudisha nchini.
“Tunapambana na ishu ya nafasi, hatutaki kusajili wachezaji wengi lakini kama tutampata Chama ina maana tutapunguza mtu mmoja kati ya washambuliaji wawili wa kigeni, kama tutamuondoa mmoja basi lazima turudishe mtu mwingine wa eneo hilo,” alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga aliyeongeza;
“Hapa ndani kuna washambuliaji wawili Waziri Junior ni mzuri lakini tunafahamu klabu ambayo atakwenda na nje ya hapo hakuna namna labda tumrudishe Mpole hapa nchini yule anaweza kuja na kufanya kitu tofauti.
Katibu Mkuu wa Lupopo, Donat Mulongoy amelithibitishia Mwanaspoti juu ya simu ya mabosi wa Yanga wakimhitaji Mpole akisema wao hawana shida na watakubaliana kama walivyomuuza beki Chadrack Boka.
“Mpira ni pesa, unaona tulifanya nao biashara ya Boka, atakuja hapo Tanzania na hata George (Mpole) naye wanamtaka wameshaongea nasi (Yanga) mara moja, tunasubiri wakija vizuri tutawapa kwa kuwa hapa kwetu hajabakiza mkataba mrefu,” alisema Mulongoy.