Moshi. Wakati mamia ya waombolezaji wakishiriki mazishi ya mama wa Frateri, Levina Massawe (58) aliyefariki dunia siku 16 baada ya mwanaye, Rogassian Masawe kudaiwa kijinyonga, vilio na simanzi vimetawala kwenye mazishi hayo.
Ibada ya mazishi ya mama huyo ambayo imefanyika katika Parokia ya Umbwe, imehudhuriwa na mapadri zaidi ya 30.
Levina ambaye alifariki dunia Juni 9, 2024, siku 16 baada ya maziko ya mwanaye, amezikwa katika makaburi ya familia yaliyopo Kijiji cha Umbwe Onana, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Frateri huyo ambaye alizikwa bila taratibu za kanisa Mei 25, 2024, alidaiwa kujinyonga kwa kutumia mshipi Mei 20, 2024 akiwa kwenye nyumba ya malezi ya Magamba iliyopo wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga huku akiacha ujumbe wa maandishi kwa mama yake mzazi ukisema: “Mama usilie nimeshindwa kufikia malengo, ninajua nimewakwaza wengi.”
Hata hivyo, wakati wa mazishi ya Frateri huyo, yaliyofanyika nyumbani kwao Mei 25, 2024, mama mzazi, aliugua gafla na kulazwa Hospitali ya KCMC na hakuweza kushiriki mazishi ya mwanaye kwa mshituko alioupata hadi naye alipofariki dunia na hakuweza kuona kaburi la mwanaye.
Akihubiri katika ibada ya mazishi iliyofanyika katika Parokia ya Umbwe, Padri Godfrey Massawe ambaye ni ndugu wa familia hiyo, amesema kifo cha mama huyo ni pigo kubwa kwa familia kwa kuwa ni takribani siku 21 zimapita tangu wamzike mtoto wake.
“Tunasikitishwa na namna ya mazingira ya kifo hiki, natambua kwamba kuna maswali mengi ambayo tumejiuliza na tunajiuliza na leo ni takribani wiki tatu tukiwa na tukio kama hili la kifamilia kwa ajili ya kumpumzisha mpendwa wetu.
“Tuseme nini? Tuna mengi ya kumwambia Mungu, kuzungumza na ya kusema kwa wale ambao ni wazee kama mimi na wengine ambao ni marehemu watarajiwa kama mimi basi, hii ni njia yetu sote lakini msiba huu ni mkubwa na umetusikitisha sana,” amesema Padri Massawe.
“Levina umelala usingizi wa amani, umelala usingizi wa milele nenda mama, kwa sababu lazima tuende, nenda kwa sababu lazima tukufuate, ndugu na jamaa tunakuja kila mmoja kwa wakati wake.”
Akitoa shukrani kwa ndugu jamaa na marafiki, mtoto wa marehemu, Padri Andrea Massawe amesema kupata misiba miwili kwa wakati mmoja ndani ya familia ni pigo kubwa ambalo halielezeki.
“Huu msiba wa mama ulikuwa ni mgumu kweli, msiba wa Rogassian (Frateri) tulikuwa hatujaukubali na kuupokea lakini tukapigiwa tena, lakini tunaamini ni mapenzi ya Mungu, Mungu aendelee kutufariji na tutasimama.
“Nawashukuruni sana kwa wale waliotukimbilia na kutuombea katika kipindi hiki kigumu sana tunachopitia, tumekuwa na kipindi kizito mno, nimevunjika vunjika, lakini tutasimama kiimani, tunawashukuru sana mliotukimbilia, nimejitahidi kujizuia lakini nashindwa, tutasimama kwa imani na Mungu atatusimamia,” amesema Padri Andrea.
Akisoma historia ya marehemu, mmoja wa wanafamilia, amesema mama yao huyo alikuwa akisumbuliwa na tatizo la sukari na presha tangu mwaka 2010 na alipopata taarifa za msiba wa mwanaye aliugua ghafla hadi umauti ulipompata.
“Mama alianza kusumbuliwa na tatizo la sukari na shinikizo la damu mwaka 2010, Mei 25, alianza kuugua baada ya kupokea taarifa za kifo cha mtoto wake, Rogassian Hugo Massawe na kukimbizwa Hospitali ya KCMC,” amesema.
Amesema baada ya kulazwa KCMC, afya yake iliendelea vizuri na Mei 31, 2024 alipata nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani na ilipofika Juni Mosi, 2024, hali yake ilibadilika tena ghafla na kurudishwa KCMC na ilipofika Juni 9, 2024, alifariki dunia.
“Mama Levina atakumbukwa kwa upendo, upole, ukarimu, ucha Mungu wake na ucheshi kwa watu wote, tunaomba Mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa waombolezaji waliokuwepo msibani hapo, Verediana Masawe amesema familia hiyo imepata pigo kubwa na ambalo sio la kawaida na kwamba inahitaji neema ya Mungu kukabiliana nalo.