NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Same Jimson Mhagama kuhakikisha Mhandisi yeyote ambaye atazembea kwenye usimamizi wa mradi ukawa chini ya kiwango mtaalam huyo awajibishwe kufanya maboresho kwa gharama zake kwenye huo mradi na sio Halmashauri kuingia gharama za maboresho yake.
Ameeleza hayo akiwa kwenye ziara yake ya kukagua miradi ya Elimu Jimbo la Same Mashariki ambapo amesema kwenye ziara zake za ukaguzi wa miradi kwenye maeneo mbalimbali amebaini uwepo wa nyufa kwenye baadhi ya majengo na kumsisitiza Mhandisi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha miradi yote itakayoanza kutekelezwa kuanzia sasa hataki kusikia habari ya nyufa.
“Mimi niliomba wataalam kutoka Mkoani wapitie baadhi ya majengo yetu kama sampo waangalie kwanini kwenye baadhi ya majengo kuna nyufa kubwa sasa kuna maelekezo ambayo wameyatoa naomba sana yale maelekezo yafanyike kwenye maeneo yote ambayo majengo yake yameonekana yananyufa lakini pia yazingatiwe kwenye ujenzi wa majengo mapya ambayo yatajengwa”
Aidha amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha kiasi cha shilingi Milioni mia tatu arobaini na nane na lakin tano (348,500,00) kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ambazo zimetumika kujenga Jengo la Utawala, Madarasa 7, Matundu 12 ya vyoo, Madarasa 2 ya awali na Kichomea taka kimoja,
Pia amempongeza Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Anne Kilango kwa jitihada zake za kuwapambania wananchi pamoja na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo kwenye Jimbo lake.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mbwana Singo amesema mradi uliibuliwa kwa lengo la kuondoa adha kwa wanafunzi waliokuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilometa 7-10, ujenzi wake umetekelezwa na Halmashauri kwa fedha za BOOST kupitia mkandarasi Master Construction Co. Ltd ambapo umewezesha wanafunzi 433 kusajiliwa kusoma kuanzia darasa la awali mpaka darasa la saba.