Haya ndiyo madhira yawakumbayo watoto

Dar es Salaam. Wakati leo Tanzania ikiungana na nchi nyingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, bado kuna changamoto nyingi zinazozorotesha ustawi wa watoto.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na ukatili, malezi duni, mimba za utotoni, mmomonyoko wa maadili, na nyinginezo.

Japokuwa zipo sheria na kanuni mbalimbali zinazolinda haki za mtoto, matukio ya uvunjifu wa haki hizo yameendelea kuripotiwa.

Hali hii inahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, jamii na wadau mbalimbali kuhakikisha watoto wanalindwa na wanapata haki zao zote za msingi.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na siku hii, Ofisa Ulinzi na Utawala wa Haki za Watoto wa Shirika la Save The Children, Mathias Busungu anasema changamoto mojawapo inayoendelea kutishia ustawi wa mtoto ni vitendo vya ukatili wa kingono.

Busungu anasema hatari zaidi ni kuwa matukio mengi yanayoripotiwa yanafanywa na watu wa ndani au karibu na familia.

Anasema ongezeko la matukio hayo linachangiwa na jamii kukosa elimu ya kutosha juu ya sheria zinazotoa ulinzi na ambazo zinazuia utendaji wa matukio pamoja na tatizo la afya ya akili ambali licha ya kusumbua wengi halijapewa kipaumbele.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi anasema mwamko wa elimu nchini umeongezeka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Anasema ongezeko hilo linachagizwa na mambo mbalimbali ikiwemo mwamko wa jamii kuhusu masuala ya elimu pamoja na uwepo wa sera ya elimu bila malipo.

Hata hivyo, Rebeca anasema changamoto iliyopo ni katika kuhakikisha watoto walioandikishwa wanaendelea na masomo hadi kufika elimu ya juu.

“Sababu zinazochangia watoto kushindwa kufikia ngazi ya juu ya elimu ni pamoja na hali duni ya baadhi ya familia, utumikishwaji wa watoto, ndoa pamoja na mimba za utotoni,” anasema.

Anasema wakati mwingine familia ndizo huwasukuma watoto hao waingie kwenye ajira wakiwa na umri mdogo kwa lengo ya kupata fedha ili kujikimu wao binafsi pamoja na mahitaji ya familia.

Akizungumzia suala la mimba za utotoni, Rebeca anasema bado jamii haiwezi kuzungumzia ustawi wa mtoto kama bado kuna watoto wa kike wenye umri mdogo bado wanaendelea kuingia katika mahusiano ya kingono yanayowaweka hatarini kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi na mimba katika umri mdogo.

Anasema pia ndoa za utotoni ni tatizo kubwa linalosababisha wasichana kutotimiza ndoto zao hususani za kielimu huku chanzo kikitajwa ni hali duni ya maisha, mila na desturi pamoja na ukosefu wa elimu.

Gyumi anagusia pia changamoto ya malezi na kusema inasababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo wazazi kutingwa na shughuli za kila siku huku watoto wakibaki wanajilea wenyewe au wasaidizi wa kazi.

Anasema kitendo cha watoto kujilea wenyewe kinapunguza ulinzi wa mtoto hivyo kumuweka katika hatari ya kufanyiwa pia vitendo vya kikatili.

“Kama tunazungumza ulinzi wa mtoto lakini hapati namna nzuri ya kulelewa, kujifunza, kupata maadili kutoka kwa wazazi wake hili halijakaa sawa.

“Kuna haja ya wazazi kutafakari upya kuhusu suala la malezi kwa watoto huku akishauri kuanzishwa kwa programu za malezi, itakayolenga kuwasaidia wazazi wa sasa kujifunza jinsi ya kulea.” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anasema kutetereka kwa taasisi ya familia kunachangia kwa kiasi kikubwa tatizo la mmomonyoko wa maadili.

Anasema katika utafiti uliofanywa na kituo hicho mwaka 2020 ulionyesha asilimia 50 ya watoto na vijana wasio na maadili wametokana na familia zilizovunjika, wazazi kuachana au migogoro katika ndoa.

“Ili kuondokana na hali hiyo, kuna haja serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kuboresha programu ya malezi chanya kwa wazazi ili waweze kushughulikia suala la malezi kuanzia ngazi ya familia na isimamiwe kwa sheria ya mtoto ipasavyo.

“Kuna watu wamewatelekeza watoto wao na kuwafanya kushindwa kupata mahitaji yao muhimu ya kimwili na kiakili, wakibainika wachukuliwe hatua ili kupunguza idadi ya watoto wa mitaani pia itajenga hofu hata kwa wengine wanaofikiria kufanya hivyo.”

Anasema ili kuweza kudhibiti utokeaji wa matukio hayo ni vyema elimu iendelee kutolewa katika jamii kwani kuna watu wengi bado hawajui sheria, hali inayopelekea kuongezeka kwa matukio hayo.

“Watoto nao pia wanapaswa kuelimishwa kukataa ukatili na kutoa taarifa pale wanapoona dalili zozote za kutokea kwa vitendo hivyo,”anasema.

Pia anasema mbali na utolewaji wa elimu vilevile mfumo wa upatikanaji wa haki iweze kuimarishwa zaidi pamoja na ulinzi wa watu wanaotoa taarifa juu ya matukio ya ukatili yanapojitokeza.

“Hii inawapelekea baadhi ya familia za waathirika wa matukio hayo kuamua kumaliza masuala hayo nyumbani jambo ambalo linarudisha nyumba mapambano dhidi ya matendo hayo,”anasema.

Vilevile alishauri kuwepo kwa sheria maalum kwa ajili ya vitendo vya ukatili majumbani kwa ajili ya kuwalinda watoto, wanawake pamoja na wanaume wanaofanyiwa vitendo vya kikatili.

“Kwa sheria ya mtoto imejitahidi sana kwa asilimia 95 kuwalinda watoto dhidi ya masuala ya kikatili, lakini tunatamani kuwepo na sheria maalum dhidi ya ukatili majumbani,”anasema.

Mwanasaikolojia Charles Nduku anasema mtoto anakuwa kulingana na malezi anayoyapata katika familia na jamii kwa ujumla hivyo moja kati ya sababu ya vijana kujihusisha na vitendo vya uhalifu na kutokuwa na nidhamu ni makosa katika malezi yaliyofanyika tangu akiwa mdogo.

Anasema vitendo vya utovu wa nidhamu na mmomonyoko wa maadili ikiwemo uhalifu vinavyofanywa na mtoto kwa wazazi wake vinaweza kuwa moja kati ya matokeo ya malezi yasiyosahihi.

Mwanasaikolojia Charles Mhando anasema moja ya mambo yatakayo saidia kurudisha maadili katika jamii ni wazazi na walezi kurudi katika nafasi yao na kutekeleza majukumu yao bila kujali msaada wanaopokea kutoka kwa watoto.

Anasema suala la kurekebisha maadili kwa vijana haliwahusu wazazi pekee, bali jamii nzima na kuongeza kuwa kufanya hivyo kutasaidia kupungua vitendo vya utovu wa nidhamu katika jamii.
Pia anashauri kuwa kuna haja ya kutoa elimu kwa wazazi wanaochipukia au wale tarajali juu ya masuala ya malezi kwa watoto.

“Elimu kuhusu malezi zianze kutolewa mapema ikiwezekana hata katika kipindi cha ujauzito au pale mama anapojifungua wanavyopelekwa kliniki pamoja na kupewa elimu ya lishe na mambo mengine wapewe elimu ya malezi ili ajue mapema ni kwa namna gani anatakiwa kuishi na kumlea mtoto kadri anavyokuwa”anasema.

Related Posts