Wanajeshi wanane wauawa kwenye mlipuko Israel

Gaza. Wanajeshi wanane wa Israel wameuawa katika mlipuko uliotokea kusini mwa Gaza jana Jumamosi Juni 15,2024, Jeshi la nchi hiyo (IDF) limesema vifo hivyo ni mojawapo ya hasara kubwa zaidi katika vita yake na wanamgambo wa Hamas.

Kwa mujibu wa IDF, wanajeshi hao wameuawa wakati gari la kivita la Namer walilokuwa wakisafiria kulipuka karibu na mji wa Rafah ulioko kusini mwa Gaza, ambapo wanajeshi wanapigana vikali mitaani.

“Gari limeharibiwa vibaya sana na waliokuwemo wamefariki, mlipuko huo umesababisha ugumu wa kutambua na kupata miili,” Jeshi la Israel limesema likinukuliwa na AFP.

Msemaji wa jeshi hilo, Daniel Hagari amesema mlipuko huo unaonekana ulikuwa wa kilipuzi kilichotegwa katika eneo hilo au kutoka kwenye kombora la kifaru.

Pia imeelezwa vifo hivyo ni miongoni mwa hasara kubwa zaidi kwa jeshi tangu ilipoanza mashambulizi yake ya ardhini huko Gaza Oktoba 27, 2023 na kusababisha vifo 306.

Tovuti ya Times of Israel ya nchini humo imewataja miongoni wanajeshi hao kuwa ni Sajenti Eliyahu Moshe Zimbalist (21), Sajenti Itay Amar (19), Sajenti Stanislav Kostarev (21) , Sajenti Au Blumovitz (20), Sajenti Oz Yeshaya Gruber (20) na Kepteni Wassem Mahmoud (23).

Imeeleza wanajeshi wote walihudumu katika Kikosi cha 601 cha Combat Engineering Corps walikuwepo kwenye mlipuko wa gari hiyo ya kivita ya Namer (CEV) na hakuna aliyenusurika.

Taarifa zaidi zimeeleza wanajeshi hao walikuwa wakirejea kambini kupumzika jana saa tano asubuhi baada ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya Hamas usiku kucha huko Kaskazini-Magharibi mwa kitongoji cha Tel Sultan cha Rafah.

Mpango wa kusitisha mapigano

Umoja wa Mataifa umesema takriban watu milioni moja wamekimbia Rafah tangu mwanzoni mwa Mei mwaka huu wakati Israel ilipoanza operesheni za ardhini katika mji huo kuwasaka wanamgambo wa Hamas.

Katika hatua nyingine,  viongozi wa kundi la G7 la nchi zilizoendelea kiuchumi walitoa wito katika mkutano wao uliofanyika nchini Italia Ijumaa Juni 14,2024 wa kupitishwa bila vikwazo misaada ya kibinadamu kwa raia huko Gaza.

Related Posts