Arusha. Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde ameuagiza Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), kuhakikisha kandarasi ya kuweka uzio katika shamba la mbegu lililopo eneo la Ngaramtoni, wilayani Arumeru inatangazwa haraka.
Amesema hiyo inaweza kuwa dawa ya kusaidia kumaliza au kuepusha migogoro ikiwemo ya uvamizi wa shamba hilo.
Silinde ametoa maagizo hayo leo Jumapili Juni 16, 2024 alipolitembelea shamba hilo na mengine yanayozalisha mbegu na kumilikiwa na Serikali katika maeneo ya Ngaramtoni na Tengeru mkoani Arusha.
Amemuagiza Mtendaji Mkuu wa ASA, Dk Sophia Kashenge kuhakikisha kandarasi hiyo inatangazwa mapema ili kuepusha wavamizi.
“Hili shamba liko mjini sana, bila kulilinda utafanya watu au wavamizi waingie katika haya mashamba na baadaye inatuletea kazi sisi kama Serikali kuja kuwatoa na kusababisha migogoro,” amesema Silinde.
Aidha, Silinde amesema kutokana na shamba hilo kutegemewa katika uzalishaji wa mbegu na kuhakikisha usalama wa chakula, ameitaka ASA kuzingatia maelekezo ya wizara ili kufikia malengo ya kuzalisha mbegu za kutosha hapa nchini.
Kwa upande wake, Dk Sophia amesema kandarasi ya kuweka uzio katika shamba hilo lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 600 ilishatangazwa.
Amesema moja ya vipaumbele vyao ni kulilinda shamba hilo pamoja na miundombinu yake ikiwemo ya umwagiliaji.
Dk Sophia amesema katika miaka ya nyuma, mashamba hayo ya mbegu yalikuwa yakivamiwa kwa kasi ndiyo maana wakaamua kuja na mpango wa kuweka uzio katika mashamba yote 15 ya mbegu.
Amesema hadi sasa mashamba mawili ambayo likiwa la mbegu Kilimi Nzega na Msimba Kilosa yameshawekewa uzio na mpango wa kuweka katika mengine unaendelea.
“Hapa Ngaramtoni tuna shamba lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 600 na hadi sasa tunalima kwenye hekta 550 na kama mlivyoona tunaweka miundombinu ya umwagiliaji, tutajitahidi kuilinda,” amesema.
Kuhusu umwagiliaji, Dk Sophia amesema ni shamba la Tengeru pekee lililowekwa miundombinu ya umwagiliaji iliyosambazwa shamba zima na wanatarajia kuongeza uzalishaji wa mbegu hizo.
Mjumbe wa bodi ya ASA, Josephine Amolo amesema maagizo ya naibu waziri yatekelezwa ili kuhakikisha uhakika wa chakula nchini unaongezeka.
“Ukiangalia kwa sasa tunazidi kuwa na mafanikio na tutajitahidi kuhakikisha hadi ifikapo mwaka 2030 Tanzania inajitosheleza ili tusiagize baadhi ya mbegu nje ya nchi kama tunavyofanya sasa,” amesema.