*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imeandaa mpango wa mageuzi ya sekta ya mifugo ambao utasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo nchini.
Ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kubuni mbinu na mikakati ya kuondokana na ufugaji usio na tija na kuwezesha kufuga kisasa.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Juni 16, 2024 Kibaha, Pwani wakati akifunga Maonesho na Mnada wa Mifugo kwa mwaka 2024.
“ Wizara msichoke wala msiache kuwapa elimu wafugaji wetu, lazima tukubali kuwa wamekuwa hivyo kwa miaka mingi mabadiliko lazima yatokee na lazima tujue kuwa maeneo mengi yanayohitaji ardhi yanaongezeka ikiwa ni pamoja na mifugo lakini ardhi haiongezeki. Hivyo, tuendelee kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa na kuwahimiza wafugaji waje kwenye maonesho kama haya ili wapate ujuzi na teknolojia itakayowasaidia”, amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Wafugaji tujue kwamba nchi na dunia inabadilika ni vizuri tukabadilika sasa kabla mabadiliko yenyewe hayatulazimisha kubadilika kama tumeamua ufugaji ni maisha yetu lazima tuamini maisha yamebadilika tuwe na mifugo yenye tija ambayo itatuletea fedha zitakazoweza kubadilisha maisha yetu.”
Ameendelea kusema “ Wafugaji msijione dhaifu wala wanyonge unaweza kukuta mfugaji ana ng’ombe 1,000 huyo huwezi kumuita masikini, ng’ombe hao wanaweza kuwa mtaji kinachohitajika ni namna gani unaweza kubadilisha maisha yako kwa kutumia hao ng’ombe ulionao.”
Vilevile, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuboresha sekta ya mifugo nchini ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya malisho ya mifugo huku akiwaasa wafugaji kuepuka kuwa na migogoro baina yao na wakulima kwa kuwa wanategemeana na migogoro hiyo inaathari kijamii na kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa ni vyema maonesho hayo ya mifugo yakafanyika kikanda ili yaweze kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili mfano mbegu bora za mifugo au kujua teknolojia za kisasa za ufugaji.
Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amewapongeza washiriki na wadhamini wa maonesho hayo ya mifugo ambayo yanalenga kutoa elimu kwa wafugaji ili kuleta tija.
“Maonesho haya ni ya muhimu na kwa mwaka huu tumeyawekea nguvu zaidi kwa kuwa yanaleta matokeo makubwa na kwa kuwa yamekuwa maelekezo ya viongozi wetu wa Serikali kuwa wafugaji wetu wasifuge kizamani. Lazima sasa ifike mahali wafugaji wetu waondokane na ufugaji wa kizamani kwa mwamvuli wa kimila, na sisi Wizara tumekuwa tukitoa elimu mara nyingi kupitia wataalamu wetu na Maafisa Ugani licha ya wafugaji hawa kuwa na mwamko mdogo wa kufuga kisasa”, amesema Mhe. Mnyeti.
Ametolea mfano kuwa wafugaji hutembea umbali mrefu kutafuta malisho na matokeo yake mifugo inafika ikiwa imechoka na kuwa Serikali imeendelea kutenga maeneo ya malisho ili kusaidia wafugaji nchini.
“ Tunatoa elimu ya kufuga kisasa kwa kunenepesha mifugo na kuuza hata ng’ombe mmoja kwa shilingi 500,000 au zaidi badala ya shilingi 200,000. Wafugaji lazima wajue ng’ombe ambaye hajafugwa kisasa, hajapata chanjo au akiugua anapewa tu dawa kiholela hawezi kuuzwa nje ya nchi kwa sababu hana ubora”, amesema Mhe. Mnyeti.
Pia, amewataka wafugaji nchini kuwatumia wataalamu wa mifugo ili waweze kupewa elimu ya ufugaji wa kisasa na wenye tija ili kubadilisha sekta ya mifugo nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze, amesema kuwa ni wakati sasa wafugaji wanatakiwa kubadilika kwa kufanya ufugaji wa kisasa kwa kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuhakikisha sekta ya ufugaji inapata mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafugaji Kibiashara Tanzania, Bw. Naweed Mulla amesema kuwa Jumuiya hiyo inalenga kuwakutanisha pamoja wafugaji, kupeana ushauri na kusaidiana kwenye changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuisaidia Serikali iweze kuwafikia kirahisi wakati wanapohitaji msaada.
“ Jumuiya hii inatusaidia sana na ningependa kuishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na watendaji wote wa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi kwa kutusaidia wafugaji ili sasa tuweze kufuga kibiashara”, amesema Bw. Mulla.
Ameeleza kuwa mtu anapotaka kufanya mambo makubwa lazima watu wengine watakosoa hivyo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aendelee kufanyakazi kwa kuwa Jumuiya ya Wafugaji Kibiashara Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ikiwa ni pamoja na kuleta mabadiliko katika sekta ya mifugo na kuwa ufugaji wa kizamani hauna tija.
Awali, Dkt. Biteko ametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ikiwemo banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Rachi ya Mbogo sambamba na kushuhudia mnada wa ng’ombe.
Maonesho na Mnada wa Mifugo kwa mwaka 2024 yaliyofanyika kwa siku tatu yalizinduliwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti.