Prisons Queens waipania WRCL | Mwanaspoti

LIGI ya Mabingwa wa Mikoa kwa Soka la Wanawake (WRCL) inatrajiwa kuanza Jumatano jijini Dodoma, huku Tanzania Prisons Queens imesema wapo tayari kupambania nafasi ya kupanda daraja la kwanza.

Ligi hiyo inashirikisha timu 19 kutoka baadhi ya Mikoa, ambapo timu mbili za juu zitapanda Daraja la Kwanza kwa ajili ya msimu ujao kutafuta nafasi ya kucheza Ligi Kuu.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Laurent Malambi alisema pamoja na ugeni wao katika ligi hiyo, lakini matarajio yao ni kufanya vizuri kutokana na maandalizi waliyofanya ikiwamo mechi za kirafiki na usajili.

Alisema baada ya kumaliza ligi ya Mkoa wa Mbeya, timu hiyo haikupata ushindani kutokana na kucheza mechi mbili, akieleza kuwa wachezaji sita walioongezwa eneo la beki, kiungo na ushambuliaji watafanya kweli.

“Tunaenda kwa tahadhari na nidhamu kuwaheshimu wapinzani, lakini matarajio yetu ni kufanya vizuri na kupanda daraja, upungufu uliokuwapo sehemu ya ufundi tumefanyia kazi” alisema Malambi.

Kocha huyo aliongeza, hawawezi kuogopa mpinzani kwani wamejiandaa kukutana na yeyote, huku akiwaomba wadau na mashabiki kuisapoti timu hiyo ili kufikia malengo.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa timu hiyo, Ajabu Kifukwe alisema uongozi utaipa sapoti Prisons Queens kuhakikisha wanapanda daraja la Kwanza kwani lengo ni kuona wanacheza Ligi Kuu.

“Sisi tunafurahishwa na maendeleo ya timu na uongozi tuko tayari kuwekeza kwa soka la wanawake kuhakikisha tunacheza Ligi Kuu, bado ni wageni ila uwezo na uzoefu tunao” alisema Kifukwe.

Related Posts