Iringa. Tatizo la wanandoa kushindwa kupeana tendo la ndoa limetajwa kuleta madhara kazini kutokana na wafanyakazi wengi kwenda kazini wakiwa na hasira na chuki zinazotokana na kutoridhishwa kimwili.
Mkuu wa dawati la jinsia mkoani Iringa, Elizabeth Swai amesema migogoro mingi inayotokea maeneo ya kazi inatokana na wanandoa kutotimiza wajibu wao wa kupeana tendo la ndoa.
Swai ameyasema hayo leo Jumapili Juni 16, 2024 mjini Iringa alipokuwa akifungua semina kwa watumishi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa.
Amesema tatizo hilo linawakumba hasa wanawake na huwafanya wengi wao kwenda kazini wakiwa na chuki inayotokana na kutotimiziwa haja ya tendo la ndoa.
“Mtu asipotimiziwa kwa kutokupewa inaleta madhara hata kazini hasa wanawake wanakuwa na hasira sana,” amesema Swai.
Aidha, ametoa rai kwa wanandoa wajitahidi kuwajibika katika kupeana tendo la ndoa kwa sababu linapunguza kwa kiwango kikubwa migogoro ndani ya ndoa inayochangia matukio ya kujeruhiana na hata vifo.
Amesema kwa mwanaume akiwa na uhitaji na mwanamke akimnyima tendo la ndoa akili huwa zinaruka, hali inayosababisha achukue sheria mkononi kwa kufanya vitendo vya ukatili kwa mwenza wake.
“Mjitahidi sana kuwajibika kwa kupeana, msinyimane, kwa sababu linapunguza sana migogoro ndani ya ndoa. Mwanaume akiwa na uhitaji wa mwanamke halafu umnyime, akili huwa zinawaruka na kujikuta wanafanya ukatili,” amesema Swai.
Pia, amegusia suala la kuongezeka kwa matukio ya ubakaji wa wafanyakazi wa ndani aliyodai kufanywa pia na wanaume kwenye familia.
“Kuna ongezeko kubwa la akina baba kuwabaka wafanyakazi wao wa ndani. Ni aibu baba mwenye nyumba ukashitakiwa na mfanyakazi wa ndani, muwaheshimu wale ni sawa na watoto wenu,” amesema Swai.
Pamoja na mambo mengine, ametumia jukwaa hilo kuwasihi wanandoa kujitahidi kujikinga na ukatili wa kingono.
Kwa upande wake, Kaimu rais wa Mkwawa, Profesa Deusdedit Rwehumbiza amewakumbusha wafanyakazi kujenga tabia ya kujiongeza kila wanapopokea masuala mbalimbali ya ukatili.
Katika hatua nyingine, Mhadhiri wa Kitivo cha Elimu na Stadi za Mitalaa, Eunice Ndomondo amesema semina hiyo ina umuhimu hasa kwenye masuala ya ukatili ambayo yanazidi kuwa mengi kila kukicha.
Amesema katika eneo la vyuo vikuu kuna wanafunzi ambao walimu wanaweza kutumia mamlaka waliyonayo kuwafanyia ukatili. Ndomondo amesema katika mazingira ya elimu, mwalimu anaweza kutumia nafasi aliyonayo kufanya ukatili wa kingono kwa wanafunzi.
Mapema akizungumza na wanahabari, Mratibu wa eneo la jinsia na elimu jumuishi wa chuo hicho, Vincent Cosmas amesema huwa wanatoa semina mbalimbali kwa wafanyakazi na wanafunzi kupitia mradi wa elimu ya juu kwa ajili ya mageuzi ya elimu (Hit).
Amesema mradi huo utagharimu zaidi ya Sh20 bilioni na unakwenda kuongeza tija kwa wanafunzi chuoni hapo.