Kilosa. Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka amesema katika kupambana na changamoto ya ukatili kwa watoto, Serikali wilayani humo imefanikiwa kuzuia uozeshwaji wa watoto wa kike walio chini ya miaka 14 takribani wanane.
Amesema watoto hao walipangwa kuozeshwa na wafugaji wa jamii ya Kimasai kwa mahari ya ng’ombe.
Akizungumza na Mwananchi Digital jana Jumamosi Juni 15, 2024, katika uzinduzi wa mradi wa ‘hakuna marefu yasiyokuwa na mwisho’ unaoratibiwa na Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT) unaopinga ukatili kwa watoto, Shaka amesema wilaya yake imekuwa na changamoto ya ukatili unaoendelea kutafutiwa ufumbuzi.
“Kwenye wilaya yetu kuna changamoto ya ukatili kwa watoto na tumefanikiwa kuudhibiti kwa kiasi kikubwa, katika kupambana na hilo, tumefanikiwa kusitisha ndoa za watoto wanane na sasa wanaendelea na masomo chini ya uangalizi wa Serikali ya wilaya yetu,” amesema Shaka.
Hata hivyo, amesema mkakati uliopo sasa ni kuhakikisha vitendo vya udhalilishaji, ukatili na adhabu kali kwa watoto vinakomeshwa kwenye jamii.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wanakuwa na jamii inayojitambua na kupinga vitendo hivyo bila woga.
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo amesema changamoto ya ukatili imekuwa kubwa kwenye mikoa mbalimbali nchini, jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa.
Kwa upande wake, Hanna Rando mtaalamu wa masuala ya kijinsia kutoka KKKT, amesema kila mtoto anayo haki ya kuishi bila kujali umri wake.
Naye Joseph Meliyo mkazi wa Kilosa ambaye asili yake ni jamii ya wafungaji wa kimasai amesema jamii hiyo imekuwa ikikosa elimu ya kuzuia ndoa za utotoni, akiiomba Serikali kuendelea kutoa elimu hiyo.