Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti ameipongeza Serikali kwa kuitengea Sh1 bilioni Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu JK Nyerere ili kuanza ujenzi wa makumbusho kubwa ya kiongozi huyo mkoani Dodoma.
Fedha hizo ni sehemu ya bajeti ya mwaka 2024/25 iliyoombwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuboresha makumbusho ya Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwake Ununio jijini hapa, Kimiti amesema baada ya kuanzisha taasisi hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, waliiomba Serikali ichangie shughuli zake.
“Kwanza tunashukuru kwamba Serikali imetoa Sh1 bilioni kujenga kumbukumbu ya Nyerere tena pale Dodoma, ambapo ndio makao makuu ya nchi. Miaka miwili iliyopita, tuliomba ile makumbusho iliyopo Butiama ihame kwa kuwa kule ni pembeni watu wengi hawawezi kufika kirahisi kama ilivyo Dodoma,” amesema.
Amesema makumbusho yatakayojengwa mkoani Dodoma yatakuwa na jengo litakalowekwa picha na kazi za Mwalimu Nyerere na za viongozi waliofanya naye kazi.
Mbali na jengo hilo, amesema wameomba Serikali iwapatie eneo la ukubwa wa ekari 300 ili kuweka kazi alizokuwa akizifanya Mwalimu Nyerere.
“Kwanza kutakuwa na jengo lenyewe, ofisi na hoteli ili watu wakifika waweze kulala palepale. Baba wa Taifa alikuwa ni mpenzi wa kilimo hivyo kutakuwa na mashamba darasa ya mazao kama pamba na kahawa na mabwawa ya kufuga samaki,” amesema.
Ameendelea kueleza kuwa eneo hilo litakuwa na mahali pa burudani ili watu wakija waburudike na pia wameomba ekari 100 ili kuweka wanyama.
Kuhusu makumbusho ya Butiama, Kimiti amesema yatabaki kuwa makumbusho ndogo na kazi zake nyingi zitahamishiwa Dodoma.
Amesema katika suala hilo wameishirikisha familia ya Mwalimu Nyerere akiwamo Chifu wa Wanzagi ambaye aliafiki.
Kimiti amewataka Watanzania kuchangia ujenzi wa makumbusho hiyo, kwani bado bajeti haijakamilika.
Kuhusu siku ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ya Oktoba 14 kila mwaka, amesema familia ya kiongozi huyo imeomba sherehe ziwe zinafanyika katika tarehe yake ya kuzaliwa yaani Aprili 23, kila mwaka na siku ya kifo chake iwe ni ya maombi.
“Familia ya Mwalimu Nyerere waliomba sherehe iwe siku ya kuzaliwa Aprili 23, 1922 na siku ile ya kifo iwe ya kumwombea tu,” amesema.
Mbali na Makumbusho hayo, Mzee Kimiti amesema wanahamasisha pia kila mkoa uwe unafanya makumbusho ya Mwalimu Nyerere kwa kukumbuka kazi alizofanya katika mikoa hiyo.
Katika hatua nyingine, Kimiti amesema matukio ya ukosefu wa maadili yanayolalamikiwa miongoni mwa wateule wa Rais yanasababishwa na wanaopeleka majina ya uteuzi kutotimiza wajibu wao.
Kauli ya Kimiti imekuja wakati kukiwa na maoni tofauti kuhusu mabadiliko anayofanya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wateule wake muda mfupi baada ya kuwateua.
“Rais hawajui watu wote hawa anaowateua, sisi tunaopeleka au kupendekeza majini hatumsaidii, tunampelekea tu na wengine kwa sababu ni marafiki wa mtu fulani. Zamani kulikuwa na vetting (uchunguzi) sio mtu mmoja anaweza kupeleka majina yote,” amesema alipoulizwa swali kuhusu maadili ya viongozi.
Amesema katika uteuzi huo, watu wenye sifa mbalimbali wanapaswa kuchunguzwa na kupimwa uwezo wao kabla ya kuteuliwa kwenye nafasi husika.
“Ndio maana zamani ukiteuliwa kwa sababu vetting imefanyika unakaa miaka mingi. Siku hizi ndio hao unaona wanafanya madudu ya ajabu, miezi miwili mitatu umetenguliwa, miaka mmoja miwili umetenguliwa. Ujue kuna makosa yanafanyika, wanamwingiza Rais wetu kwenye matatizo,” amesema Kimiti.
Ametoa mfano wa nchi nyingine bila kuzitaja, akisema wanashindanisha nafasi kwa kuangalia uwezo wa watu.
“Kuna nafasi ya mkuu wa mkoa mahali fulani, sio kuteua tu, kwanza unaangalia mkoa ule wa namna gani? Hali yake, nani anafaa? Watu wawili watatu unawaangalia. Sio kusema tu Kimiti Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Dar es Salaam inataka aina ya watu, tofauti na mtu utakayempeleka Rukwa, Lindi na Mtwara. Wakorofi wote wako hapa (Dar es Salaam).”
Akifafanua zaidi kuhusu maadili, Kimiti aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, amesema mwaka 1995 alikutana na Mwalimu Julius Nyerere mkoani humo na katika maongezi yao, alimuuliza kwa nini hajachukua fomu ya kugombea urais ilihali kuna wagombea 17 waliokuwa wamejitokeza?
“Mwalimu aliniuliza, umeshafanya kazi ya uwaziri, umeshakuwa mkuu wa Mkoa tena ile mikoa mikubwa, Kilimanjaro, Mbeya, Kagera na kote umefanya vizuri mpaka ukapata zawadi ya utumishi, mbona hukuomba?
“Nikamwambia, Baba wa Taifa sikufichi, kwanza mkoa wenyewe unavyonitoa jasho, nikiona majukumu niliyonayo na niliyopewa na Serikali sijayatekeleza je, nchi nzima si nitakufa? Kwa sababu ukishaonja uongozi inakusaidia kujua majukumu yaliyo mbele yako. Ndio maana sikutaka kukimbilia. uongozi sio jambo la kukimbilia.”
“Mwalimu akasema kwa nini wengine wanakimbilia? Mimi nimekaa pale miaka 26 hakuna kitu ni matatizo tu, unakwenda mahali fulani hawana maji, wengine barabara mbaya, wanakimbilia kutafuta nini ikulu?”
Alipoulizwa kuhusu hatua ya baadhi ya makada wa CCM kumchangia fomu rais kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2025, Kimiti amewataka makada hao kuelekeza michango yao kwa wenye uhitaji, kwani rais hashindwi kujichangia fomu ya urais atakapogombea.
Kwa nyakati tofauti baadhi ya wanachama wamekuwa wakimchangia Rais Samia fedha za kuchukua fomu ya urais.
“Mimi nasema Rais hawezi kukosa hela ya kuchangia. Kama ni kuchangia changieni kitu cha maendeleo. Wananchi wana shida nyingi, changieni wasiojiweza, changieni wenye ulemavu, hilo linawezekana.”
“Sidhani kama hata Rais mwenyewe analiafiki. Kimsingi, hata kama mnamkubali ni ninyi wenye kujipanga ya kumsaidia mbele ya safari. Si suala la kuchangia tu, mmejipanga vipi ili afanikiwe?
“Kinachotakiwa ni kushinda, mnashinda kwa kumchangia mtu hela? Hapana. Mnashinda kwa mipango na mbinu mnazoziandaa kumfikisha huko, tena wakati mwingine hata hamzisemi, mnakwenda chini kwa chini kimyakimya,”amesema.