Dar es Salaam. Miaka 22 tangu itungwe Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inayoelekeza upatikanaji wa majisafi na salama uwe ndani ya mita 400 kutoka kwenye makazi ya wananchi, utekelezaji wake haujafikia kiwango cha kujivunia.
Hayo yamebainika eneo la Mbezi Msumi, wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam, ambako baadhi ya wakazi wale wanatumia saruji na majivu kutakasa maji ya kunywa.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa takribani miezi mitatu katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam umebaini uwapo wa wananchi wanaotaabika kupata huduma ya maji wakilazimika kuchimba madimbwi, kuteka maji machafu na kuyatakasa kwa kutumia saruji au majivu.
Hayo yakibainika, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) inaeleza kati ya wakazi milioni 5.38 wa Mkoa wa Dar es Salaam,asilimia 93 wanaishi maeneo ambayo yana mtandao wa majisafi.
Akizungumza na Mwananchi Machi 16, 2024, Latifa Kidegwa mkazi wa Msumi anasema wanakabiliwa na shida ya maji kwa muda mrefu kwa kuwa eneo hilo hakuna kabisa mradi wa Dawasa.
“Tunateseka hasa sisi wanawake, tunatembea umbali mrefu kusaka maji ambayo tunachota kwenye mifereji. Hata yakipatikana yanakuwa machafu,” anasema.
“Awali tulikuwa tunachimba dimbwi kwenye mfereji hapa jirani, lakini sasa eneo hilo limejengwa, hivyo tunanunua maji ya chumvi Sh200 kwa ndoo. Ukitaka majisafi ya Dawasa inabidi utembee umbali wa kilomita mbili hadi tatu,” anasema.
Anasema baadhi ya watu wenye huduma ya maji ya Dawasa hawauzi wakisema ni kwa ajili ya matumizi yao binafsi.
“Vinginevyo tunasubiri magari ya maji kutoka Mbezi. Tunauziwa Sh500 kwa ndoo na Sh600 kwa dumu moja,” anasema.
Juliet Rutagwerela, mkazi wa eneo hilo anasema wanapochimba madimbwi ya maji hulazimika kutumia saruji kuyatakasa.
“Maji yamejaa tope na takataka zinazotoka barabarani ili yawe safi tunatumia saruji au majivu kuyatakasa. Hakuna kipimo, kwa jinsi hiyo tunaweza kupata matatizo kiafya,” anasema.
Oktoba 6, 2021, gazeti la Mwananchi liliripoti kuhusu kero ya maji kwa wakazi wa Mbezi Makabe na Mbezi Msumi wakieleza kutumia saruji kutakasa maji, hali inayoendelea hadi sasa.
Beatrice Mwakafusa anasema, “Ombi langu kwa Serikali itekeleze ahadi ya kutupatia maji. Tangu mwaka juzi tumekuwa tukiwalilia viongozi kuhusu kero hii, baadhi ya maeneo yamefikiwa na huduma ya maji, lakini sisi bado tunakunywa ya kisima.”
“Saruji huwa inatumika kwa ajili ya ujenzi, lakini sisi tumejiongeza tunatumia kusafirshia maji. Shabu (aina ya chumvi inayotumika kusafisha maji machafu) pia inatumika, lakini huku kwetu haipatikani kwa wingi, hivyo tunalazimika kutumia saruji,” anasema.
“Kama unataka kufua na huna maji, basi unatumia maji haya ya visima, kilo moja ya saruji Sh500 inaweza kusafisha pipa zima,” anasema.
Alipoulizwa kuhusu matumizi ya dawa ya klorini anasema, “klorini haiwezi kutakasa maji, inaua wadudu tu, kwa hiyo sisi tunatumia saruji kusafisha maji ili yafae kufulia na kuogea. Zamani tulikuwa tunakunywa kabisa, lakini sasa hivi tunashukuru maji yamesogea angalau tunaweza kutuma pikipiki kwa ajili ya maji ya kunywa.”
Ofisa lishe mtafiti wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Maria Ngilisho anasema njia bora ya kuchuja maji machafu ni kuyaacha kwa muda mrefu kwenye chombo ili yatuame, kisha yachotwe ya juu.
“Kuna njia ya kuacha maji yatuame kwa muda kama ni usiku kucha, kisha unachota nusu ya chombo, hapo yatakuwa safi, lakini siyo salama kwa kunywa. Ili yawe salama, unaweka dawa kwa kipimo maalumu kuua vijidudu,” alisema.
“Saruji imetengenezwa na kemikali ambazo zinaweza zisiwe salama kwa mwili. Hata kama madhara hayatajionyesha mara moja, lakini usalama wake uko shakani,” alisema.
Kwa mujibu wa mtandao wa Britannica, saruji huwa na kati ya asilimia 35 hadi 40 ya chokaa, asilimia 40 hadi 50 ya alumini, asilimia 15 ya oksaidi za chuma na asilimia sita za madini ya silica.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi Msumi, Ismail Mbinda anasema wamekuwa wakifuatilia Dawasa kwa muda mrefu ili kupatiwa maji.
“Kati ya mashina 22 ni matatu pekee yenye maji ya Dawasa. Shina moja lina nyumba 150,” anasema.
“Baadhi ya wananchi waliofungiwa maji na Dawasa ndio wanaowauzia wenzao kwa Sh100 kwa ndoo, lakini mtu hawezi kutoka kwa mfano Darajani ukaenda kununua maji Msumi A (umbali wa kilomita tatu), kwa sababu kule ni mbali. Ni lazima anunue abebe kwa pikipiki na alipie,” anasema.
“Kwa kiasi kikubwa watu wanategemea maji ya kwenye mitaro, wanafulia, wanaoga na matumizi mengine. Watu wenye hela wananunu ndoo Sh500 na walio jirani na maji ya Dawasa wananunua Sh100 kwa ndoo,” anasema.
Mbinda anasema Serikali imejenga matangi ya maji maeneo ya Mshikamano na Goba.
“Mpango kazi wa sasa ni maji kutoka Goba kuja Msumi, maji kutoka Tegeta A kuja Msumi na maji kutoka Mbopo pia yatakuja na mengine yatatoka Msakuzi kuja huku,” anasema.
“Watakapotekeleza tutakuwa na majibu kwa wananchi, lakini siwezi kusema ni lini,” anasema.
Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu anasema: “Kuna maeneo kweli hayana maji kama Msumi Center, lakini Msumi A mabomba tayari na baadhi yao maji wanayo. Kati na Mwisho hakuna maji kabisa.”
Mtemvu anasema kuna mradi utakaomaliza kabisa kero hiyo ambao upembuzi umeshafanyika.
Mbali na wasio na huduma, baadhi ya wananchi waliounganishiwa maji wamelalamika kutoyapata.
Christina Masele, mkazi wa Kimara King’ng’o anasema licha ya kuunganishiwa huduma na Dawasa hawapati maji kwa utaratibu unaoeleweka.
“Tunapata shida ya maji, kwa mfano kuanzia mwishoni mwa Januari mwaka huu hadi Machi hatukuwa na maji kabisa kwenye mtaa wetu. Tulikuwa tunatumia ya mvua. Kuna nyumba moja pale mtaani ndiyo iliyokuwa na maji,” anasema.
Mbali ya utoaji huduma kutokuwa za uhakika, analalamikia ankara kubwa akisema Mei, 2024 alipata ya Sh100, 000 licha ya maji kutoka kwa takribani wiki moja pekee.
“Nina kiwanja kingine ambacho hatujajenga lakini tumeweka bomba, mwezi huu (Mei) imekuja Sh40, 000 wakati hakuna mtu anayetumia maji kwa sababu bomba tumelifunga,” anadai.
Anadai alipofuatilia Dawasa kuwasilisha malalamiko alielezwa tatizo liko kwao.
Juma Kibeku, mkazi wa Mtaa wa Kwa Mkuwa wilayani Ubungo, anasema licha ya ratiba za Dawasa kuonyesha watapata maji Jumatano na Jumapili, haizingatiwi.
“Siku nyingine yanatoka Jumatano, siku nyingine hayatoki na hata hiyo Jumapili pia inategemea. Siku nyingine ukirudi jioni unaambiwa yametoka Ijumaa mchana. Kwa hiyo tunategemea maji ya visima vya watu binafsi,” anasema.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu anasema japo ratiba zipo, bado kuna changamoto zinazokwamisha utekelezaji.
“Unaweza kupanga ratiba, leo maji yafike kwako, lakini kuna watu wananifanya niweze kufikisha maji kwako, lazima niyasukume na ninatumia umeme. Kwa hiyo ni lazima nizalishe na nisambaze na kusiwe na changamoto yoyote,” anasema.
“Umeme ukikatika mtamboni na siyo kwamba Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) wamekata. Kwa hiyo, unakuwa na changamoto ya saa moja, unahitaji saa nane kurudi kawaida,” anasema.
“Lakini hizo saa nane kulikuwa na mtu anatakiwa apate maji, unakuta mgawo umeshahama, kwa hiyo kuna hiyo changamoto,” anaeleza.
Anasema ratiba zitaendelea kutumika wakati changamoto zikiendelea kushughulikiwa.
“Kuna changamoto huwa zinatokea ghafla, kwa mfano bomba limepasuka. Kwa hiyo, kama hakutakuwa na changamoto yoyote ratiba lazima iwepo,” anasema.
Anatoa mfano, kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua, Dawasa imetumia zaidi ya Sh4.5 bilioni kurudishia kilomita 56 za mabomba yaliyosombwa na maji.
Kuhusu maji mkoani Dar es Salaam, Kiula anasema kuna miradi 15 ya majisafi na usafi wa mazingira inayotekelezwa ambayo imetengewa Sh175.2 bilioni katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.
“Ni kweli kuna ufinyu wa bajeti, kwa kuwa bado mahitaji ya uwekezaji ni makubwa katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii ndani ya nchi yetu,” anasema.
Akiwasilisha bungeni hotuba ya bajeti ya Wizara Maji, Waziri Jumaa Aweso alitaja miradi inayotekelezwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni wa maji Mshikamano utakaonufaisha watu 179,476.
Mwingine ni mradi wa ufungaji wa pampu saba kwenye visima na tatu kwenye kituo cha kusukuma maji Kimbiji; ujenzi wa tangi, bomba kuu la kusafirisha maji na kituo cha kusukuma maji Kimbiji –Kigamboni, mradi wa maji Mkuranga, mradi wa maji Kimbiji, na mradi wa Pugu na Gongo la Mboto.
Mingine ni ya maji Kibamba hadi Kisarawe- Mlandizi –Chalinze- Mboga.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 7, 2024 alipotembelea miradi ya maji Dar es Salaam, Waziri Aweso alikiri kuwapo changamoto ya maji, akaitaka Dawasa izitatue mapema ili wananchi wapate maji.
“Dar es Salaam pamoja na wananchi wa Pwani wanachohitaji ni maji, hizi changamoto zilizopo ndani tuzishughulikie haraka, sababu zifike mwisho. Maelekezo niliyoyatoa na bodi nitakaa nayo, hizi changamoto za kiufundi zirekebishwe haraka, ili wana Dar es Salaam wapate maji, kwa sababu mitambo yetu yote ina uwezo, kikubwa usukumaji wa maji yapelekwe kama yanayohitajika,” alisema.
Wakati Serikali ikiendelea kutekeleza miradi, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya 2022/23 imebaini ucheleweshaji wa miradi kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Uhakiki wangu wa miradi inayoendelea katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam ulibaini ucheleweshaji katika utekelezaji wa miradi iliyopangwa,” inaeleza ripoti hiyo.
“Mradi wa upanuzi wa laini ya Ubungo Msakuzi Kaskazini, ikijumuisha ukanda wa Kitopeni na ukanda wa Mshikamano haikutekelezwa kwa asilimia 53 na 69 mtawalia,” imesema ripoti ya CAG.
Miradi 37 ya upanuzi ya ukanda wa Magomeni iliyopangwa haikufanyika. Kati ya miradi 36 ya kubadilisha mitambo ni mitatu pekee ilikamilika.
Itaendeleo kesho tukiangazia kero hii ya maji inavyowanufaisha watu wengine.