Dar es Salaam. Ili kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa watoto, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, imeunda mabaraza 102 katika mitaa yake.
Kupitia mabaraza hayo watoto katika mitaa husika wanakutana na kujadiliana kwa pamoja kuhusu changamoto zinazowakabili na kupatiwa elimu ya namna ya kukabiliana nazo.
Hayo yameelezwa leo Jumapili ya Juni 16, 2024 na Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtimika katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Shule ya Msingi na Awali ya Longquan Bodhi.
Mbali na mabaraza hayo, amesema changamoto za watoto zimekuwa zikitatuliwa kupitia madawati ya jinsia polisi na ngazi ya jamii.
“Tumekuwa tukipata ushirikiano wa kutosha kupitia mabaraza ya watoto na tunajitahidi kupunguza matatizo ya unyanyasaji,” amesema Mtinika.
Meya huyo ameipongeza Jumuiya ya Budha kwa kusaidia watoto yatima 200 kutoka vituo 15 vya maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambao wamepatiwa vyakula na vifaa vya shule.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Budha Tanzania, Xian Hong amesema ni muhimu jamii kutambua haki ya elimu kwa kila mtoto.
“Watoto wa Afrika wengi wanakatisha masomo yao na kusababisha kutojifunza ipasavyo, kuna elimu ya kimwili ambayo inasaidia ujuzi na stadi mbalimbali na elimu ya roho inasaidia kujifunza tabia njema na maadili mema,” amesema Hong.
Naye, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jane Shao amesema jumla ya watoto 200 kutoka vituo 15 vya watoto yatima kutoka jijini humo wamepewa msaada wa vyakula na vifaa vya shule.
“Hapa shuleni tunao watoto 20 ni yatima wanasomeshwa na jumuiya ya Budha ambao wamepatiwa misaada ya vyakula na vifaa mbalimbali tunawashukuru sana,” amesema Jane.